TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Tuesday, 10 September 2013

Lipuli yamshutumu Makamu Mwenyekiti SimbaKLABU inayoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza ya Lipuli ya Iringa imemshutumu Makamu Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ kwa kitendo cha ubadhirifu.Mwenyekiti wa Lipuli, Abu Changawa aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa ubadhirifu huo umetokana na Kinesi kuuza tiketi 2,000 kienyeji zilizotokana na vitabu 10 vilivyoongezwa kinyume cha vile vya awali walivyokubaliana kwenye mechi ya kirafiki waliyocheza mwishoni mwa wiki iliyopita.


Changawa alisema awali walikubaliana kuuza vitabu 30 ambapo kwa kila kimoja kilikuwa na tiketi 50 na vyote viliisha dakika 20 za kwanza za mchezo.Alisema baada ya viongozi wenzake kufanya uchunguzi walibaini kuwa tiketi zimeisha, lakini bado kulikuwa na idadi ya watu waliokuwa wakiingia uwanjani ndipo wakaanza kufanya uchaguzi wanaingiaje wakati tiketi ziliisha.Katika uchunguzi wao, alidai walibaini kuna vitabu vitano viliongezwa tofauti na vile vya mwanzo bila kushirikishana ambavyo viliuzwa kiholela. Baada ya kufuatilia, alisema akaelezwa kuwa tiketi hazijaisha isipokuwa kuna kitabu kimoja kilikuwa kimebaki.“Haiwezekani mechi moja vikauzwa vitabu vya aina mbili tofauti hilo ni jambo linalonisikitisha, kuona kiongozi mkubwa kama Makamu Mwenyekiti wa Simba, anafanya ubadhirifu, tutajifunza nini kwao sisi kama timu ndogo?” Alihoji Changawa.Alisema kitendo hicho anakifananisha na ujambazi na wao hawako tayari kuona kinaendelea kwa viongozi wa klabu kubwa kwa sababu ni fedheha.Alisema pia walikubaliana kuwa mapato yatakayopatikana kutokana na mechi hiyo baada ya kukatwa gharama mbalimbali, kile kinachobaki wagawane asilimia 50 kwa 50.Kwa mujibu wa Changawa, mapato yaliyopatikana ni Sh milioni 3.1, na hivyo baada ya makato mengine, waliondoka na Sh 700,000.Alisema kutokana na ubadhirifu, tiketi zenye thamani ya Sh milioni nne zimepotea na kudai kuwa walifikiri wangepata fedha nyingi ili kuwapa wachezaji posho, ilishindikana kutokana na kupata kiasi kidogo.“Tumebaki na lawama ndani ya klabu yetu wakifikiri kuwa tulipata fedha nyingi na tumekula, lakini ukweli ni kwamba tulifanyiwa ubadhirifu, ndio maana tumeshindwa kuwalipa wachezaji wetu posho,” alidai.Changawa aliongeza kuwa waliomba kucheza na Simba kwa sababu walikuwa wakihitaji msaada, lakini kutokana na kitendo hicho hawataki tena kucheza mechi ya kirafiki na klabu hiyo.Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Mzee Kinesi alidai kuwa yeye hakuhusika na tiketi isipokuwa Mhasibu wa Simba na yule wa Lipuli ndio walikuwa wanasimamia.Alisema shida iliyokuwepo kwa klabu hiyo yaani Lipuli toka awali walifikiri kuingiza kiasi cha Sh milioni nne, lakini haikuwezekana kwa vile kiwango walichokuwa wakitoza kilikuwa Sh 2,000, na kudai kuwa kama wangetaka hivyo wangetoza kiingilio Sh 3,000 au 4,000.Aliongeza kuwa hakuna maandishi waliyowekeana kuwa ziuzwe tiketi kadhaa, kwa vile vitabu walivyokubaliana ndivyo ambavyo vilikuwa uwanjani na si vinginevyo.Tayari Lipuli imepeleka malalamiko yao kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba, Zakaria Hans Pope na Mwenyekiti Ismail Aden Rage. Kwa mujibu wa Changawa, timu hiyo itaondoka leo kwenda Morogoro kwa ajili ya kushiriki kwenye mashindano ya Ligi ya Daraja la Kwanza yatakayoanza Septemba 14.

No comments:

Post a Comment