TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 30 September 2013

TAMWA Yataja Mambo ya Msingi ya Kuzingatiwa Katiba Mpya

CHAMA cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA) kimetaja mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika mchakato wa Katiba Mpya ili ujio wa katiba hiyo uweze kutokomeza mila kandamizi na vitendo vya kikatili kwa wanawake. 

Kauli hiyo imetolewa  jijini Dar es Salaam na mshauri wa masuala ya jinsia na mwanaharakati wa haki za binadamu, Gemma Akilimali alipokuwa akitoa mada katika kikao cha wahariri kutoka vyombo anuai vya habari nchini kilichofanyika makao makuu ya TAMWA Sinza.

Akizungumza, alisema vyombo vya habari havina budi kusimama kidete na kuhakikisha fursa ya ujio wa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa inaweza kuondoa vikwazo na mazingira ambayo yalikuwa kandamizi kwa wanawake.

“Tunataka katiba Mpya ibatilishe sheria ambazo bado ni kandamizi; iendelee kubatilisha sheria zote za ubaguzi wa jinsia, ikiwa ni pamoja na kukataza mwendelezo wa tabia, taratibu na mila zenye kubagua na kudhalilisha wanawake na watoto wa kike chini ya mfumo dume unaotawala jamii zetu,” alisema Bi. Akilimali.

Akifafanua zaidi, alisema katiba haina budi kutamka wazi kuwa elimu itolewe bila kikomo kwa jamii hiyo huku akishauri pia ibainishe kuwa nafasi za uongozi ziwe na haki sawa ili kuleta usawa katika makundi yote hasa wanawake.

Aidha alisema katiba mpya iwajibishe serikali kutekeleza mikataba yote ya kimataifa iliyoridhia kuhusu haki za wanawake ikiwa ni pamoja na kuendeleza misingi inayolinda utu wa mwanamke na uwepo wa mahakama ya kifamilia.

Mambo mengine ambayo mwanaharakati huyo alitaka yawekwe wazi katika katiba hiyo, ni pamoja na haki ya kunufaika na kumiliki rasilimali za nchi, haki za uzazi salama, haki za huduma za msingi, haki za wanawake walemavu, haki za mtoto wa kike na iwepo tume maalumu itakayo hakikisha uzingatiaji wa haki za wanawake katika nyanja mbalimbali.

Alisema madai yote hayo yamekuwa vikwazo kwa fursha nyingi kwa wanawake, hivyo vyombo vya habari vinaweza kuendeleza mjadala huo wa madai ili kumsaidia mtoto wa kike ambaye amekuwa akiminywa na mfumo uliopo kwa muda mrefu.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com

No comments:

Post a Comment