TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Saturday, 12 October 2013

BENKI ya Posta Tanzania (TPB) leo imepeleka huduma na elimu juu ya akaunti maalumu ya wanafunzi ujulikanayo kama 'Platinum Account' kwa wanafunzi wa kidato cha Tano na Sita wa Shule ya Sekondari Kibasila ya jijini Dar es Salaam. Mbali na huduma hiyo wanafunzi hao pia walifundishwa umuhimu wa kujiwekea akiba

Akizungumza kutoa elimu kwa baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo, Meneja Mkuu Ukuzaji Amana wa TPB, Paradise Nkini alisema TPB imeadhimia kutoa elimu kwa wanafunzi hasa kidato cha tano na sita ili kuwajengea mazoea ya kuanza kujiwekea akiba hali ambayo itawasaidia hapo baadaye.

Alisema kwa mipango ya sasa TPB itatoa elimu kama hiyo katika shule za sekondari ya mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na baada ya hapo elimu kama hiyo itaendelea kutolewa mikoa yote. Alisema elimu hiyo ya kujiwekea akiba kwa wanafunzi inayotolewa na benki hiyo inatolewa sambamba na huduma ya 'Platinum Account' ambayo ni akaunti maalumu kwa wanafunzi iliyoandaliwa kumudu mazingira ya mwanafunzi.

"Tumekuja pia kutambulisha akaunti yetu maalumu kwa wanafunzi ijulikanayo kama Platinum, hii imeandaliwa kwa ajili ya wanafunzi na imezingatia kipato chao...kwanza inafunguliwa kwa sh. 5,000 tu, haina makato ya kila mwezi na haina gharama za uendeshaji kama ilivyo kwa akaunti nyingine," alisema Nkini.

Aidha alisema sambamba na elimu inayotolewa kwa wanafunzi, TPB inatoa zawadi kwa baadhi ya shule zilizofanya vizuri kitaaluma na kuwazawadia wanafunzi baadhi ya vifaa vinavyowasaidia katika masomo yao.

"...Tunatoa zawadi kwa baadhi ya shule hasa zilizofanya vizuri na zile shule ambazo zinahali ngumu za vijijini, tunatoa zawadi za madaftari, tunatoa kalamu na kuwashirikisha wananfunzi waweze kuelewa benki yao vizuri," alisema Nkini akizungumza na wanahabari kwenye viwanja vya shule ya Kibasila.
 
*Imeandaliwa na www.thehabari.com

No comments:

Post a Comment