WAZIRI wa Uchukuzi, Dk Harrison
Mwakyembe ameishutumu Mamlaka ya Mapato (TRA) kuwa ni kikwazo kwake katika
utekelezaji wa mipango mbalimbali ya kuboresha bandari ya Dar es Salaam ikiwa
nipamoja na utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).
Dk. Mwakyembe alisema watu wengi
wanaoitumia bandari ya Dar es Salaam (TPA) wanalalamikia madudu
wanayofanya TRA hasa tatizo la kufeli kwa mfumo wa mawasiliano ya
kompyuta unaotumiwa na mamlaka hiyo kutoza kodi mbalimbali.
Alitoa shutuma hizo baada ya
kutakiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ajibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Watanzania
wanaofanya biashara na wale wanaoishi katika jiji la Guangzhou, jimbo la
Guangdong ambalo ni jiji kubwa la biashara lililoko kusini mwa China.
Jana usiku (Alhamisi,
Oktoba 24, 2013)Waziri Mkuu alihitimisha ziara yake ya China kwa kufanya
mazungumzo na Watanzania wanaoishi katika jimbo hilo maarufu kwa
biashara.
Bw. Stanley Mwakipesile ambaye ni
mfanyabiashara wa Kariakoo anayefuata bidhaa zake katika jimbo la
Guangzhou, katika hoja zake alisema
utoaji wa mizigo katika bandari ya Dar es Salaam ni tatizo kubwa kutokana na
mfumo wa kutoza kodi unaotumiwa na TRA kutofanya kazi siku zingine na hivyo
kusababisha mteja kutozwa fedha nyingi.
Mfanyabiasahra huyo alisema
kutokana na kero hiyo, wafanyabiashara wengi kutoka nchi jirani wameikimbia
bandari hiyo na sasa wanatumia bandari ya Mombasa jambo ambalo alisema ni
hasara kwa nchi. “Inakuwaje kila siku pale TRA system inakuwa down? Kuna
urasimu mwingi tu pale lakini cha ajabu wakati wao ndio hawafanyi kazi, lakini
mteja anatozwa eti kachelewesha kutoa mzigo,” alisema Mwakipesile.
Dk. Mwakyembe katika kujibu hoja za
mfanyabiashara huyo alikiri kuwepo kwa tatizo hilo na akasema eneo
linalolalamikiwa sana ni TRA ni kuwatoza wateja tozo za ziada hata kipindi
ambacho watendaji wa mamlaka hiyo hawafanyi kazi kwa kisingizio cha mfumo
kutofanya kazi (system down).
“Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli
TRA ni tatizo, hasa hili la system down kwa kweli ni kero na linawaumiza
watu wengi wanaotumia bandari yetu. Ni lazima tukae tuone namna ya kutatua
tatizo hili,” alisema Mwakyembe.
Alisema licha ya kuwepo agizo
kutoka serikalini la kutaka TPA na TRA wafanye kazi saa 24, lakini watendaji
wa TRA wanafanya kazi kwa saa 12 tu na wanalala kwa siku 10 katika mwezi mzima.
Alisema wakati TRA wanaenda kulala,
mteja hahudumiwi na wanapokuja kuendelea
na kazi kesho yake, wanawatoza wateja tozo ya kuchelewesha mzigo
wakati makosa siyo ya wateja bali ni ya watendaji wa mamlaka hiyo ya
kukusanya kodi kwa Tanzania.
“Sisi TPA hatulali; lakini wenzetu
hawa wanalala, inakuwaje wanaenda kulala wakati mizigo imerundikana pale bandarini?
Kwa kweli hawa watu ni lazima tushughulike nao.
“Mimi nimesaini BRN, Rais anataka
kuona mwaka 2015 shehena inaongezeka pale, na kufikia tani 18 sasa yule atakayekaa
mbele yangu kunikwamisha mie nitampitia,” alisema Dk Mwakyembe na kushangiliwa
kwa nguvu na watanzania hao.
Hata hivyo aliwatoa hofu Watanzania
kwa bandari ya Dar es Salaam inafanya kazi vizuri na kila mwaka shehena imekuwa
inaongezeka, hali inayoonyesha kuwa batu nchi nyingi ikiwemo Zimbabwe bado
zinatumia bandari hiyo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, OKTOBA 25, 2013
No comments:
Post a Comment