WAZIRI MKUU Mizengo Pinda ameawaonya
baadhi ya Watanzania wengi wanaokuja katika jiji la Guangzhou nchini China kwa
ajili ya kununua bidhaa mbalimbali waache kuuza hati zao za kusafiria kwa raia
wa nchi nyingine kama njia ya kujiongeza kipato.
Ametoa onyo hilo jana usiku (Alhamisi, Oktoba 24,
2013) wakati akizungumza Watanzania wanaofanya biashara na wale wanaoishi katika
jiji la Guangzhou, jimbo la Guangdong ambalo ni jiji kubwa la biashara lililoko
kusini mwa China.
Alisema kuwa wengi wa wafanyabiashara
hao wanapouza pasipoti zao wanasingizia kuwa zimepotea ndio maana kuna
malalamiko mengi kutoka kwa Watanzania wanaofika katika jimbo hilo kudai
wanaibiwa hati zao za kusafiria wakati sio kweli.
Wakati wa mazungumzo hayo, mmoja wa
Watanzania hao aliyejitambulisha kwa jina la Ambrose Lugai alisema changamoto
nyingi zinazowakabili Watanzania waishio katika jimbo hilo na moja ya tatizo
hilo ni kuibiwa kwa hati za kusafiria za Watanzania.
Bw. Lugai alisema tatizo la
wafanyabiashara wengi kupoteza pasipoti limekuwa sugu na kila siku linaongezeka
na cha ajabu linawatokea wafanyabiashara wa kutoka Tanzania tu.
“Hatuwezi kusema ni u-carelessnes,
lakini jamii ya hapa ni kutoka mataifa mbalimbali, inakuwaje pasipoti za
Tanzania tu ndio zinakuwa hot cake, naomba utusaidie namna ya kulinda hati
hizi,” alisema Bw. Lugai.
Alimwomba Waziri Mkuu awasaidie kuzungumza
na Serikali ya jimbo hilo ili Watanzania wawe wanaacha pasipoti hotelini wakati
wanapoenda mitaani, badala yake wapewe karatasi nyingine ya kuwatambulisha huko
mitaani.
Katika kujibu hoja hiyo ya Bw. Lugai,
Waziri Mkuu alisema kwamba suala hilo linamshangaza kwamba inakuwaje hati za
wafanyabiashara wa Tanzania tu ndio zinaiibiwa wakati wafanyabiashara wanaofika
kwenye jimbo hilo ni wengi kutoka mataifa mbalimbali. “Kupoteza
pasipoti ni jambo la nadra sana, sio la kawaida. Nilitegemea hili linaweza
kumtokea mtu mmoja mmoja, lakini nashangazwa kwamba hapa Goangzhou ni tatizo
kubwa.”
“Lakini taarifa nilizo nazo nyie
wenyewe wafanyabiashara mnauza hati zenu kwa Wanaigeria ili mpate fedha za
kufanyia biashara. Ndio maana nawasihi achani haya mambo, mnajifedhehesha
wenyewe na mnaifedhehesha nchi,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema kwa kuwa tatizo hilo ni
kubwa na akamtaka balozi wa Tanzania nchini China, Luteni Jenerali mstaafu Abdulrahman
Shimbo afuatilie kwa karibu kujua idadi ya watu walioibiwa hati zao za kusafiria
ili Serikali iweze kulishughulikia.
“Lakini nawaonya acheni tabia mbaya
ya kuuza pasipoti zenu kwa tamaa ya kupata vijipesa vidogo vidogo hivyo, hii ni
kuivunjia nchi heshima,” alisema.
Lakini pia alitaka jumuiya ya Watanzania
waishio China kuimarishwa zaidi ili wawe na uwezo wa kushughulikia kero zao
mbalimbali zinazowakabili wakiwa katika ugenini. Alisema ni kuimarika kwa
jumuiya hiyo tu kutawasaidia wanafunzi na wafanyabiashara kufikisha malalamiko
yao haraka serikalini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
IJUMAA, OKTOBA 25, 2013
No comments:
Post a Comment