TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday, 7 November 2013

JK: Hatutoki Jumuiya ya Afrika Mashariki

Rais Jakaya Kikwete
 Na Gazeti la Mwananchi
Dodoma:Rais Jakaya Kikwete amesema Tanzania haitajitoa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), licha kuwapo kwa vitendo alivyoviita vya ubaguzi vinavyofanywa na wakuu wa nchi za Uganda, Kenya na Rwanda.
Rais Kikwete akilihutubia Bunge jana mjini Dodoma alifichua kwamba sababu kubwa ya viongozi hao kuonekana kama wanaitenga Tanzania ni msimamo wake kuhusu masuala ya Shirikisho la Kisiasa, Uhamiaji, Ardhi na Ajira.
Rais alikuwa akirejea matukio ya hivi karibuni ya marais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Rwanda, Paul Kagame kukutana na kujadiliana kuhusu masuala kadhaa yanayohusu EAC bila Tanzania kuwapo.

“Hatuna mpango wa kuondoka, tupo na tunaendelea kuwepo na napenda niwahakikishie kwamba Tanzania haijafanya jambo lolote baya kwa jumuiya yetu au kwa nchi mwanachama mmoja mmoja na tumekuwa waaminifu na watiifu kwa jumuiya wakati wote,”alisema Rais Kikwete.
Aliwashutumu viongozi wao akisema kuwa kauli zao kwamba wanakutana kwa sababu wako tayari ni za kibaguzi kwani katika mikutano yote waliyoifanya Entebbe nchini Uganda, Mombasa – Kenya na Kigali nchini Rwanda hawakuwahi kuialika Tanzania.
“Hali hii haijawahi kuwapo na ni kwa mara ya kwanza tunaanza kuwa na makundi ndani ya jumuiya yetu; huku Kenya, Uganda na Rwanda, kule Tanzania na Burundi,”alisema Kikwete katika hotuba yake iliyochukua saa1:15 na kuongeza:
“Ikiwa itakuja kutokea jumuiya ikadhoofika au ikafa, Mungu apishilie mbali Tanzania isije ikanyooshewa kidole kwamba ndiyo chanzo cha kudhoofika huko au kufa huko”.
Alisema ataendelea kuzungumza na viongozi wa nchi hizo, na kwamba tayari ameanza ili kuhakikisha utekezaji wa mambo yote ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki unafanywa kwa kuzingatia mkataba ulioanzisha jumuiya hiyo.
Rais Kikwete alisema kwa mujibu wa mkataba huo mambo yote yanapaswa kutekelezwa kwa kuzingatia kalenda ambayo inaweka bayana mambo hayo kuwa ni Umoja wa Forodha, Soko la Pamoja, Umoja wa Sarafu na hatimaye Shirikisho la Kisiasa.
Alisema licha ya kuwapo kwa mambo hayo kwenye mkataba ambao umesainiwa na nchi wanachama, Kenya, Uganda na Rwanda wamechukua baadhi ya mambo ambayo kimsingi ni ya jumuiya na kuanza kuyaweka chini ya himaya yao.
Aliyataja mambo hayo kuwa ni Umoja wa Forodha na Shirikisho la Kisiasa ambayo taarifa zake zilipaswa kuwasilishwa katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi uliopangwa kufanyika Kampala, Uganda, Novemba 30 mwaka huu.
Kuhusu Umoja wa Forodha, Rais Kikwete alisema walikubaliana kwamba bidhaa zitozwe ushuru pale zinapoingizwa tu na baadaye kuwepo utaratibu wa nchi iliyotoza ushuru husika kwenda katika nchi ambayo bidhaa hizo zinapelekwa, lakini kabla ya utekelezaji waliwaagiza mawaziri kuandaa utaratibu mwafaka.

No comments:

Post a Comment