TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday, 13 November 2013

Mswada wa mali katika ndoa Kenya

Na Bbc Swahili
Bunge nchini Kenya limepitisha mswada wa ugavi wa mali kati ya wanandoa baada ya kutalikiana. Mswada huo unaeleza kwamba mwanamume au mwanamke atapata sehemu ya mali aliyochuma wakati wa ndoa iwapo wataamua kuachana.
Kwa mujibu wa Bbc Swahili

Katiba ya sasa inaeleza wazi kuhusu haki sawa kati ya wanandoa kabla, wakati na hata baada ya kuvunjika ndoa. Inaeleza kwamba mali inayomilikiwa wakati wa ndoa itagawanywa nusu kwa nusu baina ya mume na mke iwapo wataachana. Wabunge wanawake nchini wanataka muongozo usalie kama ulivyo.

Idadi kubwa ya wabunge wanaume walipiga kura kwa uwingi wa kura 87 dhidi ya wabunge wanawake 28 kuibadili sheria hiyo. Mabadiliko mengine katika mswada huo ni kwamba, mali iliyo katika jina la mwanandoa mmoja sio mali ya wanandoa wote wawili. Mjadala mkali ulizuka bungeni wakati wa ilipopendekezwa kukarabati kipengee kinachoeleza aina ya mali katika ndoa.

Pendekezo lililotolewa ni kwamba mali ya ndoa ni chochote kinachoweza kubebeka na kisichoweza kubebeka kinachomilikiwa na wanandoa wote au kilichonunuliwa wakati wa ndoa.

Sehemu kubwa ya wabunge wanawake waliwashutumu wenzao wanaume kwa kupitisha mswada huo ambao wameutaja kwenda kinyume na katiba. Wameeleza kwamba katika tamaduni za Kiafrika, kwa kawaida mali yote huwa chini ya jina la mume na hivyo iwapo mswada huo utakuwa sheria, utakuwa ni kama kutowatendea wanawake haki. 

 Mswada huo unaonekana kama pigo kwa wamama wasiokuwa na ajira, lakini wanaosaidia katika kuiendeleza familia katika njia nyengine kando na za kifedha. Wabunge wanawake wanaamini kazi za nyumbani, kuitunza na kuiangalia familia, ukulima miongoni mwa majukumu mengine ya wanawake nyumbani ni sehemu ya mchango usio wa kifedha unaopaswa kujumuishwa katika sheria hiyo.

Wakati ikisubiriwa kuona iwapo rais Uhuru Kenyatta atatia saini na kuudhinisha mswada huo kuwa sheria, swali sasa ni je wakati umewadia kwa mataifa ya Afrika kuidhinisha mikataba ya kugawana mali kabla ya ndoa kama ilivyo kwa mataifa ya magharibi?

No comments:

Post a Comment