JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME
YA MABADILIKO YA KATIBA
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Mwili
wa Dkt. Sengondo Mvungi kuwasili Ijumaa, Novemba 15, 2013
Jumatano, Novemba 13, 2013
Tume ya Mabadiliko ya Katiba inawafahamisha wananchi
kuwa taratibu za kuusafirisha mwili wa Mjumbe wake, Dkt. Sengondo Mvungi
aliyefariki nchini Afrika Kusini zimekamilika na mwili wake unatarajia kuwasili
nchini siku ya Ijumaa, Novemba 15, 2013.
Baada ya kuwasili, mwili huo utahifadhiwa katika
Hospitali ya Jeshi Lugalo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Aidha, siku ya Jumamosi, Novemba 16, 2013 kutafanyika
Ibada ya mazishi katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu Joseph jijini Dar es
Salaam kuanzia saa 4:00 asubuhi. Baada ya misa, marehemu ataagwa katika Viwanja
vya Karimjee kuanzia saa 6:30 mchana siku hiyohiyo ya Jumamosi, Novemba 16,
2013.
Aidha, Marehemu Dkt. Mvungi anatarajiwa kusafirishwa
siku ya Jumapili, Novemba 17, 2013 kwenda Kisangara Juu, Wilaya ya Mwanga
mkoani Kilimanjaro kwa ajili ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika siku ya
Jumatatu, Novemba 18, 2013.
Dkt. Mvungi alifariki jana (Jumanne, Novemba 12, 2013)
katika Hospitali ya Millpark jijini Johannesburg
nchini Afrika Kusini alikopelekwa kwa ajili ya uchunguzi na matibabu zaidi akitokea
Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) aliokuwa amelazwa baada ya kuvamiwa nyumbani
kwake Kibamba, wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na watu waliomjeruhi
vibaya kichwani usiku wa kuamkia siku ya Jumapili, Novemba 3, 2013.
Wakati
huohuo,
Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wakiongozwa na Mwenyekiti wake Jaji
Joseph Warioba leo (Jumatano, Novemba 13, 2013) wameungana na Mheshimiwa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kufika nyumbani
kwa marehemu Dkt. Mvungi eneo la Kibamba jijini Dar es Salaam kwa ajili ya
kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu Dkt. Mvungi.
Mwisho.
Imetolewa na:
Ndg. Assaa A. Rashid,
Katibu,
Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
Dar es Salaam
+255 757 500 800 / 0717 084 252 /
0714 662 482
No comments:
Post a Comment