Mrithi wa Kiti cha Ufalme wa Uingereza, Prince Charles ambaye pia ni Mtoto wa Malkia wa nchi hiyo, Malkia Elizabeth ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua zake za dhati za kulinda wanyamapori na kupambana na ujagili dhidi ya tembo na faru.
Aidha, Prince Charles amesema
kuwa yuko tayari kuunga mkono juhudi hizo za Tanzania kwa kushirikiana na mtoto
wake, Prince William ambaye amechagua shughuli za kulinda wanyamapori na
kupambana na ujangili duniani kama moja ya shughuli zake kuu.
Moja ya hatua ambazo Prince
Charles ameamua kuchukua ni kukabiliana na soko la bidhaa kuu za ujangili duniani,
na hasa meno ya tembo na faru, na kufanya kampeni kubwa duniani dhidi ya
biashara hiyo haramu.
Prince Charles ametoa pongezi
hizo na msimamo wake wa kuunga mkono jitihada za Tanzania wakati alipokutana
kwa mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya
Mrisho Kikwete.
Viongozi hao wamekutana kwenye
Jumba la Tintagel mjini Colombo, Sri Lanka, ambako amefikia wakati wa Mkutano
wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) ambao Prince Charles
ameufungua rasmi asubuhi ya leo, Ijumaa, Novemba 15, 2013, kwenye Ukumbi wa
Mikutano wa Mahinda Rajapaksa. Rais Kikwete naye yuko Sri Lanka kuhudhuria
Mkutano huo.
Wakati wa mazungumzo hayo, Rais
Kikwete ametumia muda mrefu kumwelezea Prince Charles kuhusu hatua ambazo
zimekuwa zinachukuliwa na Serikali yake kupambana na ujagili dhidi ya tembo na
faru ikiwamo Operesheni Maalum – Operesheni Tokomeza -ambayo ilifanyika hivi
karibuni kuwasaka na kukabiliana na wafanya biashara haramu ya meno ya tembo.
Rais Kikwete amemwambia Prince
Charles kuwa pamoja na kuchunguza malalamiko yaliyotolewa na makundi mbali
mbali ya watu kuhusu operesheni hiyo ya kwanza, bado operesheni hiyo itaendelea
kwa sababu ni muhimu kulinda wanyamapori dhidi ya majangili.
“Imefika mahali ambako
tunahitaji kuchukua hatua kali. Wakati wa Uhuru wetu kulikuwepo na tembo kiasi
cha 350,000 lakini ilipofika mwaka 1989 idadi hiyo ilikuwa imepungua na kubakia
55,000. Hata hivyo, baada ya operesheni maalum na kubwa, idadi hiyo ilikuwa
imeongezeka hadi kufikia 110,000 kabla ya kuanza wimbi jipya la ujangili mwaka
2010. Operesheni lazima iendelee,”
Rais Kikwete amemwambia Prince Charles.
“Tusaidie kufunga na kuvuruga
hili soko la bidhaa za wanyampori. Operesheni ya sasa imethibitisha kuwa
mtandao wa uwindaji haramu na biashara haramu ya meno ya tembo na faru ni
mkubwa na watu wengi wanahusika, lakini kinachovuruga zaidi ni kwamba lipo soko
la uhakika la meno ya tembo.”
Prince Charles amemweleza Rais
Kikwete kuhusu hatua ambazo anakusudia kuzichukua kukabiliana na hali hiyo,
ikiwa ni pamoja na kuandaa mkutano mkubwa wa wakuu wa nchi na Serikali Februari
13, mwakani na kufanya mkutano mwingine mkubwa na vyombo vya habari kutoka pote
duniani mwakani.
“Nakusudia pia kutumia wasanii
nyota mbali mbali duniani kuendesha kampeni ya kuielimisha dunia kuhusu athari
za biashara hiyo haramu kwa sababu asilimia kubwa ya mapato ya ujangili
inasaidia kugharimia vikundi vya kigaidi duniani.”
Imetolewa na;
Kurugenzi
ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
15
Novemba, 2013
No comments:
Post a Comment