TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday, 15 November 2013

Pembe za Tembo: Watu watano wakamatwa

Picha na Bbc Swahili

 Na Bbc Swahili
 Polisi nchini Tanzania wamesema shehena ya Pembe za Tembo zilizokamatwa katika bandari ya Zanzibar ni sawa na Tembo mia tatu na watano, zikiwa na thamani ya karibu shilingi bilioni nane, sawa na karibu dola milioni tano za Kimarekani.

Watu wawili wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhusika na pembe hizo, huku maafisa wawili wa Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA, na mmoja wa Mamlaka ya Bandari pia wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kwa mujibu wa afisa habari mkuu wa jeshi la polisi Zanzibar, Inspekta Mohammed Mhina, watuhumiwa wa kesi hii watafikishwa katika mahakama jijini Dar es Salaam.

Pembe hizo zilikuwa zimefichwa kwenye kontena la urefu wa mita 40, tayari kwa kusafirishwa kwenda nje ya nchi.

Serikali ya Tanzania iko katika kampeni kamambe ya kupambana na ujangili ili kunusuru wanyama pori ambao wako hatari kutoweka kutoka na kushamiri kwa biashara ya meno ya tembo na vipusa vya faru.

Iliripotiwa kuwa wastani wa tembo 30 huuawa kila siku nchini Tanzania, hali iliyoilazimisha serikali kukabiliana na mtandao wa ujangili, ambao unatuhumiwa kuunganisha watu wa kada mbalimbali, wakiwemo wawindaji, wasafirishaji na wafanyabiashara wakubwa ndani na nje ya nchi.

Hivi karibuni raia watatu wa China walikamatwa nchini Tanzania kwa kukutwa na pembe 706 ya tembo, sawa na Tembo 353 waliouawa katika hifadhi mbalimbali nchini humo.

No comments:

Post a Comment