TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 20 December 2013

Ipi itakuwa klabu bingwa ya Dunia kati ya hizi?

 
Na Bbc Swahili
Timu ya Raja Casablanca kutoka Morocco imefuzu kucheza fainali za klabu bingwa ya dunia baada ya kuisambaratisha Atletico Mineiro kutoka Brazil katika mchezo wa nusu fainali.

Raja waliweza kufunga magoli mawili katika dakika 10 za mwisho katika mchezo huo.

Kwa matokeo hayo Raja Casablanca watamenyana na Bayern Munich ya Ujerumani katika mchezo wa fainali.

Raja ndio waliokuwa wa kwanza kujipatia bao lililofungwa na Mouhssine Lajour.

Mchezaji wa zamani wa Barcelona Ronaldinho alipiga kiufundi mpira wa adhabu na kuisawazishia bao timu yake ya Mineiro.

Lakini Mohaine Moutaouali aliiweka mbele timu yake ya Raja baada ya kufunga mpira wa penalti, huku Vivien Mabide akikamilisha ushindi wa magoli 3 ya Raja dhidi ya 1 la Mineiro.

 Kivutio katika mchezo ni kwa wachezaji wa Raja kumzunguka Ronaldinho mara baada ya kupigwa filimbi ya kumaliza mchezo, huku wakimbusu na jezi na viatu vyake kama kumbukumbu tosha ya kucheza dhidi ya nyota huyo wa Brazil.

Ronaldinho mwenye umri wa miaka 33 amewahi pia kuvichezea vilabu vya St-Germain ya Ufaransa, AC Milan ya Italia pamoja na Barcelona ya Hispania, huku pia akiichezea timu yake ya taifa ya Brazil.

Mchezaji huyo bora wa zamani wa mwaka, ameichezea timu yake ya taifa mara 90 na ana matumaini kuwa atakuwa miongoni mwa kikosi cha Brazil kitakachocheza fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2014, zinazoandaliwa nchini Brazil mwakani.

Kouko Guehi na Vivien Mabide wa Raja Casablanca walishangilia wakiwa na viatu vya Ronaldinho baada ya kushinda mchezo huo wa nusu fainali za kombe la klabu bingwa ya dunia dhidi ya Atletico Mineiro.

Raja sasa itapambana na mabingwa wa Ulaya Bayern Munich katika fainali itakayochezwa Jumamosi huko Marrakesh.

Hii ni mara ya pili kwa fainali hizo kutozikutanisha timu za Amerika Kusini na Ulaya katika mchezo wa fainali, tangu michuano hiyo kuchezwa katika muundo wa sasa ulioanza mwaka 2005.

No comments:

Post a Comment