TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday 20 December 2013

Pendekeza majina ambayo Rais Kikwete atayafirikia katika uteuzi wa wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete ameyaalika na kuyakaribisha makundi mbali mbali katika jamii kupendekeza majina ya watu ambao Rais atayafikiria katika uteuzi wa Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba.

Rais Kikwete ametoa mwaliko huo kulingana na mamlaka anayopewa katika Kifungu cha 22(1) (c) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba (Sura ya 83) na aliutangaza rasmi mwaliko huo katika Gazeti la Serikali Na. 443 la Ijumaa iliyopita, Desemba 13, 2013.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam leo, Ijumaa, Desemba 20, 2013 na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, mwaliko huo ambao pia utatangazwa katika magazeti ya kawaida, makundi yaliyokaribishwa kutoa mapendekezo yametakiwa kuwasilisha kwa Rais orodha ya watu wasiopungua wanne na wasiozidi tisa kwa kila kundi.

Makundi hayo ambayo yametajwa katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ni Taasisi zisizokuwa za Kiserikali, Taasisi za kidini, Vyama vyote vya siasa vyenye usajili wa kudumu, Taasisi za elimu ya juu, Makundi ya watu wenye ulemavu, Vyama vya wafanyakazi, Vyama vinavyowakilisha wafugaji, Vyama vinavyowakilisha wavuvi, Vyama vya wakulima na Makundi mengine yenye malengo yanayofanana.

Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa katika kuwasilisha mapendekezo ya majina yao, makundi yaliyoalikwa yanalazimika kuonyesha umri, jinsia, uzoefu, sifa na sehemu ya makazi ya mtu anayependekezwa ikiwa ni pamoja na kuzingatia usawa wa kijinsia.

Katika mwaliko wake, Rais Kikwete ameelekeza kuwa orodha ya majina ya wanaopendekezwa, iwasilishwe kwa maandishi ama kwa kupelekwa na mtu kwa mkono ama kwa kutumia huduma ya Posta.
Orodha hizo ziwasilishwe kupitia anuani zifuatazo:

1.      Katibu Mkuu Kiongozi
Ofisi ya Rais, Ikulu,
S.L.P. 9120,
Dar Es Salaam

ama
2.      Katibu Mkuu Kiongozi,
Ofisi ya Rais,
S.L.P. 4224,
Zanzibar

Taarifa ya Balozi Sefue inasema kuwa tarahe ya mwisho ya kupokea orodha ya majina yanayopendekezwa ni Januari 2, 2014.
           
“Mwisho”

No comments:

Post a Comment