TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 2 December 2013

Jambazi auawa kwa kupigwa risasi Tabora

Na Mwandishi wetu
Igunga.

Watu sita wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamevamia maduka ya wafanyabiashara katika kijiji cha Ziba kata ya Ziba wilaya ya Igunga mkoani Tabora na kufanikiwa kupora fedha.

Majambazi hao ambao walikuwa na silaha zinazosadikiwa kuwa ni bunduki aina ya shortguni walivamia kijijini hapo na kuanza kufyatua risasi hewani.

 Kwa mujibu wa jeshi la polisi wilaya ya Igunga lilisema kuwa tukio hilo lilitokea jana majira ya saa 3:30 usiku katika kata ya Ziba wilayani Igunga ambapo majambazi hao walivamia maduka ya wafanyabiashara hao.

Aidha majambazi hao baada ya kuanza kufyatua risasi hizo  walimfyatulia risasi katika mguu wa kushoto na kumjeruhi mfanyabiashara Malanda Issa(50)mkazi wa Ziba na kumpora fedha kiasi cha shilingi mill 1.5.

Askali polisi kutoka wilayani Igunga  baada ya kufika katika eneo la tukio  walianza kupambana na majambazi hao kwa kurushiana risasi ambapo walimfyatulia risasi mgongoni jambazi mmoja na kufanikiwa kumuua.

Baada ya jambazi huyo mmoja kufyatuliwa risasi na askali polisi na  kuuliwa majambazi wengine walifanikiwa kukimbia na kutokomea kusikojulikana.

Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Igunga wamelipongeza jeshi la polisi kwa kupambana na majambazi hao na kufanikiwa kuuwa jambazi huyo mmoja.

Wananchi hao walisema kuwa  kuuawa kwa jambazi huyo ni fundisho kwa majambazi wengine na kusema itasaidia kupunguza matukio ya ujambazi na utekaji wa mabasi katika wilaya ya Igunga ambao umekuwa ukiwatesa wananchi hao mara kwa mara.

Kwa upande wake kamanda wa polisi mkoa wa Tabora kamishna msaidizi Peter Ouma alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa jeshi la polisi linaendelea kuwasaka majambazi hao waliokimbia.

Kamanda Ouma aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi ili kuweza kuwakamata majambazi hao na kuwafikisha katika vyombo vya sheria.

No comments:

Post a Comment