“Jina langu limevuma, kwenye mitaa. Jina langu lina hadhi ya ki-superstar.Jina langu linaongeza idadi ya maadui, jina langu…..” Hayo ni maneno kutoka kwenye wimbo wa Jina Langu wa msanii mahiri wa Hip Hop nchini Joseph Haule ‘Professa Jay’.
Bila shaka wimbo huu
ulimvumisha sana miaka saba iliyopita, ndio maana nimeweza kuyambuka mashairi
yake hayo, na bado ni msanii mkongwe anayeendelea kukubalika na anayejivunia
mafanikio mengi yaliyotokana na muziki wake.
Wakati anaanza muziki alikuwa ana ndoto nyingi ikiwa ni pamoja na kumiliki nyumba, gari,
studio kubwa ya kisasa na kuwekeza kwenye ujasiriamali mwingine.
Tayari amefanikiwa kwa asilimia kubwa na hiyo yote
ni kwasababu ya juhudi zake katika kuhakikisha anatoa muziki utakaoendelea
kumweka kwenye chati ya muziki wa kizazi kipya
na kuwavutia maelfu ya mashabiki wake.
Ndani ya mwaka jana ameweza kufungua studio, saluni
na tayari anaishi katika nyumba yake ya kisasa iliyoko Kimara Mbezi, jijini Dar
es Salaam.
Anasema ilikuwa ni kama ndoto na sasa imekuwa kweli,
ni studio ambayo ameiita kwa jina la kilugha yaani ‘Mwanalizombe studio’ akiwa na maana ya mwana Ruvuma, kwani asili
yake ni mkoani humo.
Kama ilivyo
kwa wanamuziki wengine nchini, lengo lake kubwa lilikuwa ni kukuza muziki wa
kizazi kipya hasa ikizingatia kwamba ndio
unaokuwa na kukubalika kwa kasi kwa kadri miaka inavyosogea.
Anasema
studio hiyo itatoa nafasi kwa wasanii tofauti tofauti wakiwemo pia wasanii
chipukizi kurekodi kazi zao ikiwa ni sehemu ya kukuza vipaji vipya
vinavyozaliwa kila siku.
Toka
aifungue mwaka jana tayari ameajiri produza mmoja anayemwamini na mwaka huu
ataendelea kuboresha baadhi ya mambo muhimu yanayohitajika katika studio hiyo.
Anasema
kwanza studio hiyo itawarekodia vijana kwa bei ambayo kila mmoja ataimudu sio
kwa ajili ya kukomoa kama ambavyo wengine wamekuwa wakifanya.
Pamoja na
studio hiyo, alifanikiwa kufanya uwekezaji kwa kufungua saluni kubwa ya kisasa
ambayo ameajiri vijana wengi wa kitanzania wenye ujuzi. Hiyo yote ilikuwa ni
mipango aliyojiwekea na kufanikiwa kutimiza.
Anasema
ataendelea kuwekeza kwenye mambo mengi zaidi kwani sio kwamba ataendelea kuimba
muziki hadi uzeeni, akiamini utamsaidia kuendesha maisha yake na familia yake
inayomtegemea huko baadaye.
Yapo mengi ambayo
ameyafanya kama sehemu ya mafanikio katika muziki wake ikiwa ni pamoja na
kujenga nyumba ya kisasa huko Kimara Mbezi nab ado ana ndoto ya kuendelea
kuboresha muziki wake ili asirudi nyuma kama ilivyotokea kwa baadhi ya
wanamuziki wakongwe wanaoendekeza starehe zaidi kuliko uwekezaji.
Aliahidi kutoa nyimbo mbili mwezi
huu ili kuwarudisha mashabiki wake kwani amekuwa kimya kidogo ingawa kwa mwaka
jana alipata shoo nyingine kwenye mikoa mbalimbali kwa kushirikiana na nguli
mwenzake Judith Wambura ‘Lady Jaydee’.
Historia yake
Bila shaka kuna baadhi ya watu hawajapata historia ya msanii huyu wa siku
nyingi. Professa Jay alizaliwa miaka 39 iliyopita jijini Dar-es-salaam. Ni mtoto wa sita kati ya
watoto tisa wa Mzee Leonard Steven Haule na Mama Rose Majanjara aliyefariki
dunia mwaka jana kwa ajali ya gari.
Alianza kuimba muziki wa
kizazi kipya mwaka 1990 mara baada ya kumaliza
masomo yake na mwaka 1992 ndipo alipoanza kuvuma rasmi.
“Nakumbuka mwaka 1992 nikiwa pamoja na mshikaji wangu KILLA B pale Chuo Kikuu cha Dar es salaam
ukumbi wa UDASA. Nakumbuka watu walikuwa kibao na nilikonga sana nyoyo za
mashabiki wa muziki huu kwa style yangu ya enzi hizo ya Tongue Twist,”alisema
hayo wakati huo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupanda jukwaani.
Prof. Jay anatazamika kama msanii aliyeweza kuwateka wazee
waweze kusikiliza muziki wake hasa kwa
kibao alichofanya wakati yupo na kundi la Hard Blasters Crew kilichofahamika
kama Chemsha Bongo.
Ndilo kundi aliloanzia na ilikuwa ni moja ya makundi yaliyofanya muziki huu
ambao hujulikana kama 'muziki wa kizazi kipya' kukubaliwa na sehemu kubwa ya watanzania.
Mwaka
1995 kundi hilo lilishinda kuwa kundi
bora la Hip Hop. Walitoa albamu ya kwanza iitwayo 'Funga Kazi' mwaka 2000. Ndio
iliyoleta mapinduzi makubwa sana ya
muziki wa Hip Hop nchini.
Ilikuwa
na nyimbo kali zilizovuma wakati huo 'Chemsha Bongo' na 'Mamsapu' ambazo
zilichangia kufanya muziki wa aina
hiyo kuwa wa kila rika na kupewa
heshima. Kabla ya hapo muziki huu ulionekana kuwa ni muziki wa wahuni.
Baadaye aliamua kuwa msanii binafsi mwaka 2001 na muda mfupi baada ya hapo akatoa albamu yake ya
kwanza iitwayo "Machozi Jasho na Damu".
Albamu hii ilivuma haraka sana na kumfanya
kupata tuzo ya kuwa mtunzi bora wa Hip Hop kwa nyimbo yake ya 'Ndio Mzee' ikifuatiwa
na Nyimbo ya "Piga Makofi na Bongo Dar es Salaam zote zilitikisa wakati
huo.
Mwaka
2003 alitoa albamu ya pili iitwayo
"Mapinduzi Halisi" ambayo nayo ilishinda tuzo ya Kili Muziki awards
na kuwa albamu bora ya muziki wa Hip Hop
nchini. Ilibeba nyimbo kama "Zali la Mentali",
"Msinitenge," na "Promota Anabeep"
Mwaka
2005 alitoa albamu ya tatu iliyoitwa
"J.O.S.EP.P.H". Jina la albamu hii lilitokana na nyimbo iliyotoka
mwanzo kabla ya kutoa albam hiyo. Nyimbo hiyo ilichaguliwa kuwa bora ya bongo
fleva kwenye Shirika la Utangazaji la BBC na Radio One awards
Pia,
imewahi kuteuliwa kuwa ni albamu bora ya Hip Hop ,Mtunzi bora wa nyimbo za Hip
Hop, na wimbo bora ya Hip Hop kwenye Kili Music Awards wakati huo kupitia
wimbo wa ‘Nikusaidieje’ na baadae Kisima muziki awards ya Kenya ikiwa ni nymbo bora ya hip hop na Video bora
ya Hip Hop kutoka nchini Tanzania.
Mwaka
2011 alitoa albam nyingine iliyoitwa Jaysco Dagama ilikuwa na nyimbo kama Kamili gado na
nyingine kibao. Anajivunia toka ameanza muziki zaidi ya miaka 20 iliyopita
amefanya shoo kwenye nchi za Marekani, Canada, Ujerumani, Ugiriki, Norway,
Sweden, nchi za Afrika Mashariki, Afrika Kusini, India, Nigeria, Ghana, Ehtiopia , Uingereza
na nyingine nyingi.
Pia, ni
balozi wa malaria. Mwaka huu amepania kuendeleza mapinduzi katika muziki wake
kwa kutoa vitu vikali ili jina lake liendelee kuvuma kwenye mitaa.
No comments:
Post a Comment