TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday 16 January 2014

Mapya Yaibuka Ndoa Iliyovunjwa na Mahakama Nkasi, Yadaiwa Mume ‘Alimbaka’ Mwanafunzi…!

Nkasi-Rukwa

SAKATA la ndoa iliyovunjwa na mahakama ya Mwanzo Wilaya ya Nkasi, Mkoa wa Rukwa limeingia katika sura mpya baada ya uchunguzi zaidi kubainika kuwa mume aliyeiomba mahakama ivunje ndoa yake, Ndebile Kazuri alimkatisha mke masomo ya elimu ya msingi mkewe baada ya kumtia ujauzito akiwa darasa la sita.


Kwa mujibu wa vyanzo vya habari ambazo mwandishi wa habari hii amevipata vinaeleza kuwa Kazuri ambaye hivi karibuni ameiomba mahakama hiyo kuvunja ndoa yake na Bi. Maria Tarafa kwa madai mke wake anakiburi na mdokozi wa vitu ndani ya nyumba yao, alimkatisha masomo na baadaye kumuoa mwaka 2004.

Taarifa zinaeleza kuwa Kazuri alimkatisha masomo Bi. Tarafa, mwezi Machi akiwa Shule ya Msingi Isale iliyopo Wilayani Nkasi huku akiwa na umri wa miaka 15 na alijifungua mtoto akiwa na umri wa miaka 16.
Taarifa zinasema baada ya kutiwa ujauzito Bi. Tarafa wazazi wa mumewe walizungumza kifamilia na kukubaliana wasimshtaki kwa kuwa atafungwa na mama na mtoto kukosa huduma za baba. Baada ya hapo walikubaliana amuoe hivyo mume huyo alilipa mahari na kumuoa binti huyo wa darasa la sita akiwa na umri wa miaka 16.

Akizungumza na Thehabari.com, kuzungumzia madai hayo Bi. Tarafa amekiri kuwa ni kweli kwamba alikatishwa masomo na Kazuri mwaka 2003 akiwa darasa la saba, lakini kwa kuwa baba yake mzazi na baba mzazi wa Kazuri walikuwa marafiki sana waliyamaliza wenyewe na kukubaliana watoto wao waoane.

Alisema aliunganishwa na mumewe Kazuri mwaka 2004 akiwa na umri wa miaka 16 baada ya mumewe huyo kulipa mahari (ng’ombe) kwa familia ya mzee Tarafa.

“…Inaniuma sana kwa kitendo ambacho ananifanyia kwa sasa kwani alinikatisha masomo, kanipotezea muda wangu na kaniongezea mzigo wa watoto wane na anataka niende kuishi nao peke yangu baada ya kwenda kuongopa mahakamani,” alisema Bi. Tarafa.

Alisema sababu alizozitoa mahakamani si za kweli kwani amekuwa akimpiga na kumnyanyasa ndani ya ndoa yake na kumtaka aondoke kwake na kwenda kuishi kwao. Alisema kuna kipindi mtalaka wake huyo aliwahi kumfukuza akiwa na watoto wawili na kurudi nyumbani kwao lakini baadaye alikuja kuomba radhi na kutaka apewe mke wake aende kuishi naye.

Kazuri alifungua kesi katika Mahakama ya Mwanzo, Namanyere Wilaya ya Nkasi Oktoba 28, 2013, kesi namba 26/2013 iliyosikilizwa na Hakimu aliyetajwa kwa jina la B. Stanley; na Novemba 18, 2013 hakimu huyo baada ya kuisikiliza kesi aliamuru ndoa ivunjwe.

Mahakama ilivunja ndoa hiyo na kuamuru Bi. Tarafa aondoke na watoto wawili kati ya wanne waliozaa na mumewe kipindi wakiishi kama mke na mume bila kueleza namna watoto hao watakavyo pata huduma toka kwa baba yao.

Katika hukumu yake mahakama iliamuru watoto wa miaka 7 na 9 watabaki kwa baba yao na wenye miaka chini ya saba kubaki na mama yao. Mahakama hiyo ya mwanzo pia iliamuru mke apewe magunia 9 ya mahindi kati ya 10 ambayo walizalisha wote na bati 7 zilizokuwa nyumbani kwao.

Hata hivyo alipotafutwa Kazuri kuzungumzia madai hayo kwa njia ya simu hakuweza kupatikana kwani taarifa ambazo zimetufikia ni kwamba, kwa sasa anashikiliwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Nkasi kwa kitendo cha kuvunja nyumba ya mtalaka wake na kumtishia kumdhuru huku akimtaka aondoke kwake ilhali mvutano ukiendelea.

*Imeandaliwa na www.thehabari.com kwa kushirikiana na TAMWA.
 

No comments:

Post a Comment