TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 5 February 2014

CAF yampiga 'STOP' Chuji kuwavaa wamoroco Jumamosi, Yanga wamtenga Okwi mechi na Komorozine

SHIRIKISHO la Soka Afrika (CAF) limeikumbusha klabu ya Yanga SC kutomtumia kiungo Athumani Iddi ‘Chuji’ katika mchezo wake wa Jumamosi dhidi ya Komorozine ya Comoro, Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika, kwa kuwa bado anatumikia adhabu ya kadi nyekundu.

Ofisa Habari wa Yanga SC, Baraka Kizuguto amewaambia Waandishi wa Habari leo makao makuu ya klabu, Jangwani, Dar es Salaam kwamba, CAF iliwaandikia barua kuwakumbusha kwamba, Chuji alipewa kadi nyekundu mara ya mwisho klabu hiyo ilipocheza michuano ya Afrika mwaka juzi katika mechi dhidi ya Zamalek.

Kwa sababu hiyo, Yanga SC haitamtumia Chuji siku hiyo hadi hapo atakapomaliza adhabu yake. 
 
Aidha, Kizuguto pia amesema kwamba hawatamtumia mshambuliaji Mganda Emmanuel Okwi japokuwa CAF imempa leseni ya kucheza michuano hiyo mwaka huu, hadi hapo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litakapotoa baraka zake. 

Ikumbukwe, Okwi amesajiliwa mwaka huu Yanga SC kutoka SC Villa ya kwao, Uganda baada ya kugoma kuendelea kuichezea Etoile du Sahel ya Tunisia iliyomsajili kwa Mkataba wa miaka minne Januari mwaka jana kutoka Simba SC ya Tanzania pia.

Okwi alifungua kesi Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) akilalamika kutolipwa mishahara na Etoile ndipo akaruhusiwa kujiunga na SC Villa.

Hata hivyo, baada ya Villa kumuuza Yanga ikidai ina haki zote, TFF imeandika barua FIFA kutaka ufafanuzi kama inaweza kumuidhinisha Mganda huyo kucheza timu ya Jangwani na wakati huo huo imeizuia klabu hiyo kumtumia hadi majibu yapatikane. 

Pamoja na hayo, hadi sasa Etoile haijalipa Simba SC dola za Kimarekani 300,000 za manunuzi ya mchezaji huyo na Wekundu wa Msimbazi nao wamefungua kesi FIFA.     

Yanga ilinusa na kutolewa Raundi ya Kwanza katika Ligi ya Mabingwa mwaka 2012 na Zamalek ya Misri, mechi ya kwanza wakilazimishwa sare ya 1-1 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Februari 18, na marudiano Machi 3, wakifungwa 1 – 0 Cairo.

Miaka miwili baadaye, Yanga SC wanarejea kwenye michuano hiyo mikubwa kwa ngazi ya klabu Afrika na watafungua dimba nyumbani Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Jumamosi na Komorozine ya Comoro katika Raundi ya Awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
 
Chanzo.Binzubeiryblog

No comments:

Post a Comment