TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday, 13 February 2014

Emmanuel Okwi ruksa kuchezea yanga - FIFA Shirikisho la Soka Dunia (FIFA), limemruhusu mshambuliaji Emmanuel Okwi kuichezea Yanga.

Barua ya Fifa iliyotua ofisi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ilisema kuwa suala la malipo ya Simba kwa Etoile du Sahel hayausiani na Emmanuel Okwi kucheza mpira. 


Rais wa TFF, Jamal Malinzi amesema kuwa taarifa hiyo ya Fifa imemruhusu mshambuliaji huyo acheze mpira iwapo ametimiza vigezo vyote vya usajili ikiwemo ITC. 

"FIFA  wametuletea taarifa leo saa nne asubuhi na wametaka Okwi aruhusiwe kucheza mpira kama anakidhi vigezo vyote, sasa vigezo ni pamoja na ITC na ITC Okwi anayo, hivyo ni ruksa kucheza mpira."alisema 

Simba ilimuwekea pingamizi FIFA  mshambuliaji huyo raia wa Uganda asicheze Yanga, kwa kuwasilisha pingamizi hilo mwaka jana ikiwa imeandikwa kwa lugha ya Kiswahili ambapo Fifa iliirudisha kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), kuomba itafsiriwe kwa lugha ya Kingereza ili waweze kuielewa kwa ufasaha. 

"Sisi tulimzuia kwa sababu Simba wamemuwekea pingamizi Okwi asicheze Yanga, ndio maana tulimsimamisha. Usajili wake CAF upo cleared kabisa hauna matatizo yoyote, CAF haijatoa leseni yake kwa vile wanasubiri Fifa itoe hukumu, imehofia isije ikatoa leseni alafu ikajikuta inaingia kwenye mkanganyiko na FIFA." alisema 

 Hata hivyo hukumu hiyo ya Fifa ni njia nyeupe kwa Okwi kuichezea Yanga kwenye michuano ya kimataifa ikiwemo mchezo wao dhidi ya Ahl Haly ya Misri.

Awali, Okwi aliyekuwa mchezaji wa Etoile du Sahel ya Tunisia, aligoma kuwachezea Waarabu hao baada ya kushindwa kuheshimu makubaliano ya kimkataba, na baada ya mgomo uliochukua miezi kadhaa SC Villa ambayo ndiyo iliyomkuza Okwi kabla ya kumuuza Simba, iliomba Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kumruhusu arudi Uganda ili asipoteze kiwango chake. 


Licha ya Fifa kutoa hati ya uhamisho (ITC) kuiruhusu SC Villa kumtumia, baadaye majogoo hao wa Uganda walimuuza kwa Yanga jambo ambalo limezua kesi. 

Baada ya kusajiliwa kwa Okwi Yanga, Simba kupitia mwenyekiti wake Ismail Aden Rage, walipinga usajili huo wakidai haujafuata sheria kutokana na nyota huyo kuwa katika kesi dhidi ya Etoile. 

TFF ilibaini utata katika usajili wa Okwi, na baada ya kupitia makubaliano ya Fifa na Villa iliona hakuna jibu la moja kwa moja kutoka Fifa ambalo lingewaruhusu Villa kumuuza Okwi katika klabu nyingine yoyote kwavile aliruhusiwa kwenda SC Villa kwa kibali maalumu.

Source. Michuzi Blog

No comments:

Post a Comment