TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 19 February 2014

BFT yamtema Kidunda kwenye timu ya Taifa


Seleman Kidunda
SHIRIKISHO la Ngumi Tanzania(BFT) limewatema baadhi ya mabondia maarufu katika timu ya Taifa akiwemo Seleman Kidunda na badala yake limechukua wachezaji wengi chipukizi katika timu hiyo.  


BFT imechagua wachezajii sita kwa ajili ya kambi ya mazoezi ya Uturuki kwa ajili ya maandalizi ya michezo ya Jumuiya ya Madola itakayofanyika Glasgow, Scoatland kuanzia Julai 23-Agosti 3, mwaka huu.


Kati ya mabondia waliochaguliwa ukimwondoa Nasser Mafuru aliyepata nafasi hiyo wengine wote ni chipukizi kwasababu hawakuwahi kushiriki mashindano makubwa ya kimataifa.

Waliotemwa ni Bondia Seleman Kidunda ambaye aliwahi kushiriki mashindano ya Olimpiki mwaka 2012 London, Uingereza na yale ya Jumuiya ya Madola mwaka 2010.
 Wengine ni Hashim Simon, Joseph Martin, Sunday Elius, Revocatus Omary, Gerald Maechichi na Haruna Swaga.


Msemaji wa BFT Salum Viduka ametaja mabondia sita  walioteuliwa katika timu hiyo kuwa ni Hamad Furahisha wa Magereza, Ezra Paulo wa Kigoma, Mohamed Kidari wa Tanga, Ally Boznia wa Tanga, Mohamed Hakim wa Kawe na mkongwe mmoja ambaye ni Nasser Mafuru.


“Mabondi hao na Kocha mmoja Jonas Mwakipesile ndio watakaoenda katika kambi iliyoahidiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, kujiandaa na mashindano ya Jumuiya ya Madola,”alisema.


Alisema timu iliyochaguliwa imetokana na mashindano ya kitaifa ya Mandela yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, na kuongeza kuwa sababu kubwa ya kuwatema mabondia hao maarufu ni kutokana na kushindwa kushiriki kwenye mashindano hayo kwa ajili ya kupima uwezo wao. 
  

Viduka alifafanua kuwa awali, uongozi mpya ulipoingia madarakani uliwaeleza mabondia wote kurudi katika timu zao, ambapo walitaka washiriki kwenye mashindano ya Mandela na mabondia wengine wa mikoani ili wapambane  na wale wanaofanya vizuri wachaguliwe.


Alisema matokeo yake mabondia hao maarufu hawakushiriki, ni mmoja tu ndiye aliyejitokeza na wengine wakidharau.


Kwa mujibu wa Viduka, mabondia waliochaguliwa kwenda kwenye kambi hiyo ni wachache hivyo inaweza kuwa vigumu kuleta ushindani na kurudi na ubingwa hivyo wanafanya mchakato wa kuzungumza na Kamati ya Olimpiki kwa ajili ya kuongeza wengine sita na makocha wengine wawili.

No comments:

Post a Comment