TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Tuesday 4 March 2014

MWANANCHI:Sitta apiga jaramba kuongoza Bunge

Mwenyekiti wa Muda wa Bunge Maalumu la Katiba, Pandu Ameir Kificho, akizungumza na mjumbe wa Bunge hilo, Samuel Sitta (kushoto), ndani ya Ukumbi wa Bunge, Dodoma jana. Picha na Emmanuel Herman.

Dodoma. Siku moja baada ya kuteuliwa na CCM kuwania uenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta amesema ameanza kupitia sheria na kanuni zitakazomwezesha kuliongoza huku akiahidi kutenda haki kwa wajumbe wote iwapo atachaguliwa.
Akizungumza mjini Dodoma jana, Sitta alisema: “Nawashukuru wote waliokuwa wakiniunga mkono na niseme wazi kuwa nitatenda haki kwa wajumbe wote wa Bunge Maalumu la Katiba.”
Alisema kazi kubwa aliyonayo baada ya uteuzi huo ni kuhakikisha kuwa anazipitia sheria na kanuni zinazoongoza bunge hilo na sheria nyingine kwa kuwa ndizo nyenzo zake za utendaji kazi.
Akizungumzia mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho na mchuano uliokuwapo kati yake na Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge alisema: “Hii ni hatua ya awali na ya kawaida tu ndani ya CCM. Mara nyingi chama changu kikiona kuna mambo yanayoleta msuguano, basi huamua kuteua jina moja kwa ajili ya kugombea. Wameteua majina mawili kwa demokrasia kabisa. Ninakishukuru chama changu kwa kuniteua na kwa sasa najiandaa na uchaguzi.”
Suluhu: Nitafanya maajabu
Kwa upande wake, Mjumbe wa bunge hilo aliyeteuliwa na CCM kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti, Samia Suluhu Hassan aliwaambia waandishi wa habari jana kwamba ana uwezo mkubwa wa kuliongoza Bunge Maalumu la Katiba na hana shaka katika uteuzi wake.
Samia ambaye pia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), alijisifu akisema ana rekodi nzuri ambayo haitiliwi shaka kwa weledi wake na haoni tatizo kwa yeye kupewa nafasi hiyo.
“Nina rekodi nzuri ya kuongoza Serikali kwa muda mrefu na sijapata doa lolote, kwa hiyo sioni ugumu wowote,” alisema.
Samia aliwahi pia kuwa Waziri wa Ajira na Wanawake na baadaye, Waziri wa Utalii katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kabla ya kuwa Waziri wa Nchi, katika Ofisi ya Makamu wa Rais.
Kinana na mchakato
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alizungumzia mchakato uliompitisha Sitta kuwania nafasi hiyo na kusema ulilenga kuzuia mgawanyiko ndani ya chama.
Hata hivyo, alisema Chenge aliamua kwa hiari yake kujitoa baada ya kukubaliana na Sitta walipoitwa na uongozi wa chama kwa ushauri.

 Akizungumza katika mahojiano maalumu mjini Dodoma, Kinana alisema: “Kiutaratibu, yeyote ilimradi awe mjumbe wa Bunge la Katiba, angeweza kujitokeza kugombea uenyekiti. CCM, walijitokeza wawili walionyesha nia; Sitta na Chenge.

Chanzo.Gazeti la Mwanachi
    

No comments:

Post a Comment