Na Mwandishi wetu
Mamlaka ya Usafiri wa
Anga kupitia Mfuko wa Mafunzo watoa ufadhili kwa wanafunzi watano kusomea
Urubani na Uhandisi wa usafiri wa ndege Afrika Kusini.
Akizungumza katika
hafla ya kuwaaga wanafunzi hao Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga,
Fadhil Manongi amesema kuwa kutokana na uhaba wa Marubani na Wahandisi katika
tasnia ya usafiri wa anga Mamlaka ilianzisha mfuko kwa ajili ya kugharamia
mafunzo hayo.
Aliongeza kuwa
wanafunzi hao wamepatikana kupitia michakato mbalimbali ambapo jumla ya
wanafunzi 272 waliomba nafasi hizo ambapo waliochaguliwa ni watano na watasoma chuo cha 43 Air School
kilichopo Port Elizabeth nchini Afrika Kusini.
Aidha, Manongi alisema
kuwa mafunzo hayo yatachukua muda wa miaka miwili na yanagharimu jumla ya Dola
za Kimarekani 310,000 ambapo kila moja atatumia dola 62,000 ambazo ni zaidi ya
shilingi milioni mia moja za Tanzania.
Mpaka sasa mfuko una jumla
ya Dola za Kimarekani 250,000 ambazo zimetokana na michango na misaada ya wadau
mbalimbali katika sekta ya usafiri wa anga.
Kwa upande wake Kaimu
Mwenyekiti wa Kamati ya Mfuko wa mafunzo Gaudence Temu amesema kuwa upungufu wa
Marubani na Wahandisi ndiyo changamoto iliwasukuma wadau wa usafiri wa anga
kuanzisha mfuko huo ambao lengo lake ni kuwawezesha wazawa wengi zaidi kumudu
gharama za kusoma kozi za urubani.
Pamoja na hayo
wanafunzi hao wameombwa kuwa wazalendo kwa kurejea nchini na kutumikia taifa
lao mara watakapohitimu mafunzo yao badala ya kutokomea na kunufaisha mataifa
mengine.
Wanafunzi waliopata
ufadhili huo ni pamoja na Herman Mushi, Doris Bariki, James John Castico, Linus
Mtimba na Calvin Massao
No comments:
Post a Comment