18 Septemba, 2013.
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
WAZIRI MKUU: SERIKALI KUIMARISHA UTAWALA BORA
WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali
itaendelea kushirikiana na wabia wa maendeleo ili kuimarisha utawala bora na
hatimaye kusaidia kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi walio katika ngazi za
chini.
Ametoa kauli
hiyo leo mchana (Jumatano, Septemba 15, 2013) wakati akifungua maadhimisho ya
siku ya soko la SULGO (SULGO Market Day) yaliyoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu
TAMISEMI kwa kushirikiana na Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo ya Ujerumani
(GZI).
Waziri Mkuu
alisema maonyesho hayo yamelenga kujenga uwezo kwenye Serikali za Mitaa ili
waweze kutoa huduma nzuri kwa wananchi kwa kuwapatia mafunzo yatakayo wawezesha
kuwa na vyanzo vya fedha, kuwekewa mifumo ya kupata fedha hizo, kuwezeshwa
kusimamia matumizi ya fedha zao na kujengewa ushikishwaji wa wananchi kuanzia
ngazi ya chini hadi ngazi ya Taifa.
“Serikali za
Mitaa ndiyo nyenzo kuu ya Serikali katika utekelezajiwa shughuli za serikali,
na fedha nyingi zinapelekwa huko ambako miradi ya maendeleo iko. Utaona kuwa
kuwa na fedha ni jambo moja lakini kuweza kusimamia matumizi ya zile fedha ni
jambo jingine kwa hiyo wametoa mafunzo
kwa watendaji wa vijiji na kata juu ya suala hili,” alisema.
Akizungumza na waadhishi wa habari
mara baada ya kukagua maonyesho hayo, Waziri Mkuu alisema amefurahi kuona
kwamba katika ngazi ya chini kabisa wananchi wamejengewa uwezo wa kutambua
sheria ndogo zinatungwa vipi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Waziri mwenye dhamana
anapokuja kusaini sheria hiyo.
Aliishukuru Serikali ya Ujerumani kupitia
taasisi yake ya GIZ ambayo imetoa Euro milioni 9.8 kwa ajili ya kusaidia mradi
huo unaotekelezwa kwa majaribio kwenye wilaya nane za mikoa ya Tanga na Mtwara.
Wilaya hizo ni Mtwara, Nanyumbu, Tandahimba na Masasi kwa mkoa wa Mtwara wakati Mkoani Tanga unatekelezwa
katika wilaya za Handeni, Muheza, Jiji la Tanga na wilaya ya Tanga.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu
kufungua maonyesho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI, Bibi
Hawa Ghasia alisema soko la SULGO ni dhana ya ushirikishwaji wa wananchi katika
kutoa maamuzi kuanzia ngazi ya chini, ngazi ya wilaya na hatimaye ngazo ya
Taifa au Serikali Kuu.
Alisema dhana hiyo imekuwa
ikiendeshwa chini ya Mpango wa Serikali wa Maboresho ya Serikali za Mitaa
(LGRP). Alisema mradi huo wa soko la SULGO ulianza Januari 2008 na unatarajiwa
kukamilika ifikapo Septemba 2014.
Naye Mkuu wa Kitengo cha
Ushirikiano kutoka Ubalozi wa Ujerumani, Bibi Claudia Imwolde-Kraemer alisema
mradi huo umelenga kuimarisha utendaji wa serikali za mitaa kwa kufuatilia
ukusanyaji wa mapato na kuweka mifumo ya uwajibikaji kwenye masuala ya fedha.
“Utekelezaji wa mradi huu ni sehemu
ya ugatuaji wa madaraka katika ngazi ya vijiji, wilayani na mikoani,” alisema.
Alisema anathamini sana muda ambao
umetumika katika kuwaelimisha watendaji wa ngazi mbalimbali na ushirikishwaji uliofanyika
katika ngazi hizo kwamba vitakuwa chachu ya kuleta mabadiliko kwenye ngazi tofauti
za kijamii.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, SEPTEMBA 18, 2013.
No comments:
Post a Comment