Mwimbaji
mkongwe wa muziki wa bongo fleva Bushoke amekuja tena kivingine kwa kuamua
kurekodi nyimbo zake tatu nchini Uganda akiwa amewashirikisha wasanii mbalimbali
wa nchini humo.
Nyimbo zake
tatu mpya ambazo hupigwa zaidi katika runinga mbalimbali nchini zinajulikana
kama bingili, nakupenda na mama wa nghamba ambazo amejaribu kuwashirikisha
wasanii mbalimbali wa Uganda wakiwemo Ngoni. Zote hizo zitaingia katika albam yake
mpya itakayoitwa katerero.
Akizungumza
kwa njia ya simu na blog ya jamii Bushoke alisema katika albam yake hiyo
itakuwa na nyimbo kumi ambapo nyingine atashirikiana kuimba na baba yake mzazi Maximilian
Bushoke nchini Afrika ya Kusini.
Alisema nyimbo
ambazo zimebakia atarekodi katika studio ya baba yake huko Afrika ya Kusini inayoitwa
Bushoke records na kwamba kwa sasa wameona ni bora wafanye kazi kwa pamoja , kwa vile pia baba yake
alishawahi kuimba muziki kwa muda mrefu siku za nyuma.
Msanii huyo
ambaye alivuma sana miaka michache iliyopita na nyimbo zake kama Mume bwege,
barua na nyimbo nyingine kadhaa amekuwa na mvuto mkubwa kwa mashabiki wengi wa
Tanzania kutokana na uimbaji wake wenye ujumbe kwa jamii.
Kama ambavyo
inajulikana kwamba mashabiki wengi walianza kumtambua katika anga ya muziki
baada ya kutoa wimbo ‘mume bwege’ akijaribu kutoa ujumbe kwa jamii jinsi
ambavyo baadhi ya wanaume wakitendewa ubaya na wake zao kwa kugeuzwa kuwa
bwege.
Lakini
unajua ni kwanini msimu huu ameamua kurekodi muziki wake nje ya Tanzania?
Anataka kuhakikisha anatimiza ndoto za kuufanya muziki wake utambulike sio tu
katika ukanda wa Afrika Mashariki bali pia katika ukanda wa Kimataifa.
“Unajua
nataka nitimize malengo yangu ya kuhakikisha kuwa muziki ninaoimba unafika
mbali ndio maana pia nimeamua kushirikiana na wanamuziki wa kimataifa ili
kuleta ladha tofauti,”.
Kuna nyimbo
mbili Bushoke ameziimba kwa kuchanganya lugha mbili yaani Kiswahili na Kiganda.
Hivyo anaamini kuwa muziki wake utaendelea kupendwa na mashabiki mbalimbali
kama ilivyokuwa kwa nyimbo zake ambazo tayari ameshazitoa siku za nyuma.
Anawaeleza
mashabiki wake kuwa wakae mkao wa kula kwani muziki anaouleta safari hii una
vionjo tofauti. Amejaribu kuimba kwa lugha mbalimbali ili ujumbe uweze
kuwafikia wengi.
“Mashabiki
wangu nawapenda sana na naamini mtanipokea vizuri katika muziki wangu ambao
tayari nimeanza kuutoa, nataka niwaletee mambo mazuri ili muweze
kuburudika,”anasema.
No comments:
Post a Comment