TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday 21 June 2012

Waathirika wa mabomu Mbagala kuu kulipwa fidia zao


Serikali imesema inatarajia kuanza kulipa fidia ya sh bilioni 2,200,000,000 kwa wanananchi 1,788 wa Kata ya Mbagala Kuu waliokuwa wamepeleka malalamiko ya mapunjo ya fidia iliyotolewa kwa mara ya kwanza iliyotokana na mlipuko wa Mabomu yaliyotokea katika kambi ya Jeshi Mbagala mwaka 2009.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Said Meck Sadik alisema jana kuwa baada ya kupokea malalamiko ya wananchi hao ilifanyika tathmini na ndipo ikapatikana idadi ya majina hayo.

“Tathmini iliyofanyika ilikuwa ni kwa wananchi 2132 waliokuwa na madai ya sh biloni 2,236,037,741 na baada ya kupitiwa upya na uhakiki kufanyika jumla ya wananchi 1,788 wamethibitishwa kustahili malipo hayo yenye jumla ya sh bilioni 2,200,000,000” alisema.

Aidha alisema kuwa timu hiyo ya wataalamu iliyopitia madai hayo ilibaini kuwa madai ya wananchi 344 waliokuwa na madai yao ya sh 36,037,741 hayakustahili kwa sababu mbalimbali.

Alisema kuwa majiya ya watakaolipwa yatabandikwa kwenye mbao za matangazo kwenye ofisi za mitaa na Kata ya Mbagala Kuu na kwamba zoezi la ulipaji linatarajiwa kuchukua siku 20-30 na litaanza Juni 25 katika mtaa wa Mbagala Kuu na litaendelea na mitaa mingine.

Mkuu huyo alisema kuwa amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke kutoa matangazo kwa njia ya vipaza sauti kwenye maeneo husika ili kuwafahamisha wananchi juu ya zoezi hilo.

Alisema kwa kuwa walipaji ni wengi wanakadiria kwamba kila siku watahudumiwa watu 100. Katika fidia ya awali jumla ya sh bilioni 8 zililipwa kwa wananchi hao ambapo kwa sasa zitalipwa bilioni 2.2 zitakazofanya fidia hiyo kufikia zaidi ya bilioni 10.


No comments:

Post a Comment