TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Monday 2 July 2012

Kampuni feki ya Solar panel yabainika Dar


Na Mwandishi wetu
Chama cha Wadau wa Nishati Jadidifu (TAREA) kimewahimiza wananchi kuwa makini dhidi ya watu wanaowauzia vifaa vya umeme jua mtaani wakidai kuwa ni promosheni kwa vile vingi vimebainika kuwa ni feki.

Agizo hilo linafuatia baada ya wananchi wa mikoa ya Kilimanjaro, Manyara  na Arusha kulizwa hasa baada kuuziwa vifaa vinavyojulikana kama solar panel na baadaye kugundua kuwa havifanyi kazi.

Akizungumza na blogu hii jijini Dar es Salaam Katibu Mtendaji wa Tarea Injinia Mathew Matimbwi alisema katika kijiji cha Magadini na Simanjiro wananchi waliuziwa vifaa hivyo na mtu mmoja aliyejitambulisha kwa jina la moja la Bernad na kuwaeleza kuwa wachaji masaa 8 kisha watumie lakini walivyofanya hivyo havikufanya kazi.

Alisema mfanyabiashara huyo alitoa namba ya simu hii 0759953583 akidai anatoka katika kampuni ya vifaa hivyo inayoitwa SOLAR AFRIQUE akidai Ofisi zake zipo Ubungo Plaza Dar es Salaam na Mwanza.

“Jambo la ajabu mfanyabiashara huyo akipigiwa simu hapokei inaita tu na kukata na namba za simu za kampuni zinazoonekana kwenye risiti ambazo amekuwa akizitoa pia hazipokelewi,” alisema Injinia Matimbwi.

Alisema wananchi hao baada ya kuona vifaa havifanyi kazi walimpa risiti na vile vifaa Mwalimu mmoja anayefahamika kwa jina la Emmanuel Madauda ambaye alikuwa na safari za kuja Dar es Salaam ndipo wale wananchi wakamwomba aje navyo kwenye kampuni hiyo ambayo imeandikwa kwamba iko Dar es Saalam na Mwanza.

Hata hivyo, baada ya Mwalimu huyo kufuatilia pale Ubungo Plaza alielezwa hakuna Kampuni kama hiyo na hivyo kupewa orodha na kampuni zilizoko pale na ndipo kuelekezwa akaulizie TAREA ili wamsaidie.

Mwalimu huyo alibeba risiti mbili zenye majina ya wananchi waliouziwa vifaa hivyo feki  kama ushahidi ili aje kuulizia kwenye kampunii hiyo ikiwezekana warudishe fedha zao.

Kwa mujibu wa Mwalimu Madauda alisema  Bernad ambaye ndiye mfanyabiashara huhisiwa kwamba ni raia wa Kenya kutokana na lafudhi ambayo alikuwa akiongea ila amekuwa akiuza bidhaa hizo nchini kwa madai kuwa ni za hapa nchini wakati hiyo Kampuni haipo.

Matimbwe alisema mbaya zaidi vifaa hivyo wananchi wa mikoa hiyo wamekuwa wakiuziwa kwa bei ya shilingi 40,000 wakielezwa ni bei ya promosheni lakini ukweli haviuzwi kwa bei hiyo wala haviuzwi kimoja kimoja kama ambavyo wananchi wameuziwa.

Alisema kutokana na tukio hilo wananchi wanatakiwa kujifunza kutokana na makosa na kwamba watazungumza na tume ya ushindani ili kushughulia tatizo hilo ili ikiwezekana wahusika wachukuliwe hatua kwa kuuza bidhaa feki.

No comments:

Post a Comment