TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 25 July 2012

TBS yaeleza juhudi ilizofanya katika kupambana na bidhaa feki


Shirika la Viwango Tanzania (TBS) ni shirika ambalo lilianzishwa mwaka 1975 chini ya sheria namba 3, ikarekebishwa na sheria namba 2 ya mwaka 2009. Kazi kubwa ya shirika hilo ni kuandaa viwango vya bidhaa mbalimbali kama vile chakula, vinywaji, vifaa vya umeme, ujenzi na bidhaa za ngozi.

Pamoja na hayo, pia wamekuwa wakiangalia bidhaa za elektroniki na bidhaa nyingine, na hupima bidhaa hizo kwa kutumia maabara zake za kupima viwango mbalimbali.

Shirika hilo kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na dawa, Polisi, Sumatra na Mamlaka nyingine za udhibiti wa bidhaa wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na watu wanaouzia watu bidhaa feki sokoni na kutoa elimu kwa jamii kuepukana na matumizi ya bidhaa hizo ili kuepukana na athari.

Katika mahojiano na Ofisa Masoko Mwandamizi wa TBS Daud Mbaga anaeleza kuwa, ili kuhakikisha ubora wa bidhaa sokoni shirika hilo hutumia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutoa nembo ya ubora kwa bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi ambazo zinakuwa zinakidhi matakwa ya viwango

Pia, hutoa nembo ya ukaguzi wa bidhaa za nje ndani ya mipaka ya Tanzania mathalani meli inapokuwa imefika bandarini bidhaa huchukuliwa na kupimwa kuona kama bidhaa hiyo iko kwenye kiwango sahahi.
Lakini ikiwa wamegundua bidhaa ambazo wanazikagua haifai kuuzwa katika soko la Tanzania, hawaruhusu kabisa  kuingia nchini na hatua wanayoichukua ni kuharibu bidhaa hiyo ili kuwa fundisho kwa wafanyabiashara wengine.

Vile vile, wamekuwa na utaratibu wa kukagua bidhaa ndani ya nchi inapotoka. Utaratibu huu ni mpya na ulianzishwa mapema mwaka huu ili tu kuhakikisha kuwa bidhaa zinazouzwa sokoni ni za ubora unaohitajika.
Mbaga anaeleza kuwa chini ya utaratibu huo Makampuni matatu ikiwa ni pamoja na SGS, Inrettech na Bureau Veristers yamepewa dhamana ya kufanya ukaguzi huo.


“Ina maana kuwa bidhaa kama haifai hukataliwa huko huko katika nchi na kama ikibainika zina ubora basi hupakiwa na kuletwa katika soko la Tanzania,” anaeleza Mbaga.

Anasema utaratibu huo mpya umekuja kutokana na changamoto zilizokuwepo siku za nyuma kwenye mifumo iliyotangulia kwani ilikuwa imeruhusu uwepo wa bidhaa hafifu sokoni. 

Mfumo huo licha ya kuongoza bidhaa katika kiwango kikubwa lakini pia inasaidia kupunguza msongamano bandarini na pia unamsaidia mfanyabiashara kuokoa muda.

“Mfumo huu unamuhakikishia mlaji ubora wa bidhaa anayokula na thamani ya pesa zake hivyo ni matumaini yetu kuwa utaendelea kufanya vizuri, na hivyo kuwawezesha watanzania kupata bidhaa inayohitajika katika kiwango cha kimataifa,”anasema.

Anasema uzuri wa mfumo huo ni kwamba hauruhusu bidhaa bandia kupenya katika soko la Tanzania kwani mwingizaji akija na bidhaa zake lazima aonyeshe vibali vyote muhimu kwamba shehena anayotaka kuileta Tanzania ni halali.

Si hayo tu bali wana mfumo mwingine wamekuwa wakiutumia katika kuzifanya bidhaa ziwe na ubora na mfumo huo ni ule wa kukagua kiwanda na kukipa cheti cha ubora dhidi ya bidhaa zake. Akitolea mfano wa bidhaa kama vile pikipiki ambazo nyingi hutoka China, bia ya Heineken ambazo hutoka Uholanzi hupewa cheti za ubora wakiwa katika viwanda vyao kisha kuruhusiwa kuingizwa nchini.

Pamoja na kuanzisha mifumo hiyo ya uboreshaji wa bidhaa Mbaga anasema TBS hukabiliwa na changamoto nyingi na zaidi licha ya juhudi zao bado kuna upenyezo mkubwa wa bidhaa feki sokoni.

Anasema Tanzania ni nchi kubwa sana na ina mipaka ambayo siyo rasmi. Mipaka hiyo imekuwa ikitumika kupitisha bidhaa feki jambo ambalo wananchi wengi wamekuwa wakiona pengine TBS imeshindwa kufanya kazi vizuri.

Anasema uelewa wa wananchi kuhusiana na hilo bado pia ni mdogo. Ni kweli kwamba kuna wengine wanaona bidhaa hizo zikipitishwa lakini hawana ushirikiano wa kutosha na Polisi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na shirika hilo.

“Tunaonyesha juhudi kubwa katika kuzuia njia za panya lakini tatizo lipo kwa wananchi kwani hawana ushirikiano wa kutosha na zaidi kwa wamekuwa wakitoa lawama kwamba pengine kazi imeshindikana lakini ukweli sivyo,”anasema.

Mbaga anasema mifumo wa TBS, TFDA, TRA na bandari haijaweza kufanya kazi kwa asilimia 100 kutokana na matatizo kama hayo, lakini anaamini kuwa juhudi bado zinaendelea kufanyika na kupitia utaratibu mpya waliojiwekea watashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya bidhaa feki.

Lakini tatizo lingine kubwa linaloelezwa kuwa ni changemoto kubwa kwao ni kuongezeka kwa mahitaji ya bidhaa kwa wananchi zaidi ya uwezo wa kutosheleza mahitaji hayo. Anasema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilichukulia kama faida kwao.

Wamekuwa wakiingiza bidhaa nyingi feki ili kuwaridhisha wananchi na kwasababu wananchi wengi wamekuwa hawana uelewa kuhusiana na bidhaa hizo wamekuwa wakinunua bila matatizo na kuonyesha nia ya kuzihitaji zaidi.

“Mahitaji makubwa ya wananchi hufanya wafanyabiashara kuwa na moyo wa kuendelea kuuza bidhaa ambazo hazina ubora matokeo yake kunakuwa na mwanya wa uingizaji wa bidhaa hizo kiholela na wengine ndio hutumia njia za Panya,”anasema.

Kama wananchi wangekuwa na uelewa kuhusu zipi ni bidhaa feki ili wasinunue na kuamua kutowaunga mkono wafanyabiashara katika ununuzi wa bidhaa hizo ni wazi hata wafanyabiashara wasingeweza kuzileta kwa wingi  kwani wangeona kuwa ni bidhaa ambazo hazinunuliki.
Kwasababu hiyo, wapo wananchi wengi tayari wamepata hasara kwasababu wameuziwa bidhaa zisizokuwa na ubora unaohitajika na wengine wamejikuta wakiuziwa vifaa mbalimbali ambavyo havifanyi kazi kwa bei rahisi.
Mfano mzuri ni hivi karibuni kuna baadhi ya wananchi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara waliuziwa vifaa vya umeme jua vinavyojulikana kama ‘Solar panel’ na kuelezwa kuwa wavichaji kwa masaa 8, na kumbe walovyofanya vile na kuviwasha ili wavitumie walikuta haviwaki kabisa.
Mkazi mmojawapo aliyelia kwa kuuziwa kifaa hicho cha umeme jua ni Hilary Nyandoa kutoka kijiji cha Magadini Simanjiro ambaye alifikisha malalamiko yake katika Ofisi za Tarea  jijini Dar es Salaam kuwa aliuziwa kifaa hicho na wafanyabishara wanaopitisha bidhaa mtaani (Wamachinga) kikiwa na anwani zinazodai zinatoka katika kampuni moja ya Dar es Salaam iliyoko Ubungo Plaza.
Lakini mara baada ya uchunguzi wa Tarea ikabainika kuwa hakuna kampuni kama hiyo katika Ofisi za Ubungo Plaza, na walipokuwa wakijaribu kupiga namba za simu ili kueleza dukuduku lao, zilikuwa zikiita bila kupokelewa.
Kutokana na matatizo kama hayo, jamii inahitajika kuwa makini pindi inapochagua bidhaa sokoni, lakini pia kuwa makini dhidi ya wale wafanyabiashara wanaowapitishia mtaani wakidai wanauza kwa bei ya promosheni kwani kuna hatari ya kuuziwa bidhaa ambazo hazifanyi kazi.

Hata hivyo, Mbaga anasema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiuza bidhaa zisizo na ubora kwa kuangalia kipato cha wananchi jambo ambalo halitakiwi kwani kufanya hivyo ni kuwaonea kwasababu vifaa wanavyouziwa haviwezi kumudu kwa muda mrefu.

Anasisitiza umuhimu wa jamii kuamka na kuwa makini pindi wanapochagua bidhaa kwani wanahitajika kuangalia zile ambazo zina nembo ya TBS kwani zinakuwa zimeruhusiwa kuuzwa sokoni.

No comments:

Post a Comment