Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) ni
shirika lisilo la kiserikali lenye dira ya kuwa na jamii ya Tanzania yenye usawa
na haki kijinsia, wanawake walio na maendeleo maisha endelevu na haki ya
kijamii. Ni shirika tetezi la haki za binanadamu, hususani haki za makundi
yaliyoko pembezoni, ya wanawake, ya walemavu, ya wasichana, ya vijana, ya watu
waishio na VVU/UKIMWI nk. Dhamira yake ni ukombozi wa wanawake kimapinduzi.
Kuhusu Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike,
‘INTERNATIONAL DAY OF THE GIRL CHILD, ni siku ya kimataifa itakayosherekewa
Oktoba 11 ulimwenguni kote. Siku hii itasherekewa kwa mara ya kwanza duniani
baada ya kupitishwa na kutangazwa na Umoja wa Mataifa kupitia mkutano wake mkuu
wa tareha 19/12/2011.
Hii ni siku ya kutambua haki za wasichana na changamoto
maalumu zinazowakabili kama wasichana ulimwenguni. Hii imetokana na kampeni za
miaka mingi za wanaharakati wa Kanada na Amerukani. Siku hii, imetengwa maalumu
kwa ajiri ya wasichana kufanya utetezi na kuchukua hatua wao wenyewe na kwa
ajiri ya wenzao. “Tokomeza ndoa za utotoni”; ndio kauli mbiu ya siku
hiyo.
Lengo na madhumuni makuu ya siku ya mtoto wa
kike ni kutangaza, kuhamasisha na kuongeza uelewa na ufahamu juu ya, na
kutetea haki za mtoto wa kike ulimwenguni. Uamuzi wa Umoja wa Mataifa
kutangaza siku hii ni ishara ya kutambua changamoto zao na uwezo walionao
wasichana. Pia Umoja wa Mataifa umeonesha dhamira yake ya kutokomeza mawazo
mgando, ubaguzi, ukatili na tofauti za tabaka katika masuala ya kiuchumi
yanayopelekea wasichana kupata vipato visivyo sawia.
Kwa kuungana na wenzetu
duniani, TGNP, tumeamua kuisherekea siku hiyo katika semina yetu ya
jinsia(GDSS) ya Juma tano tarehe 10/10/2012 hapa viwanja vya TGNP Mabibo karibu
na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji. Muda wa sherehe utakuwa
ni masaa 2 tu. Tutaanza saa 9:00 alasiri na kumaliza saa 11:00 jioni.
Mada ya siku hiyo; “Tokomeza ndoa za utotoni:kuza vipaji vya wasichana”.
Pia kutakuwepo na jopo la wazungumzaji.
Aidha napenda kukuhabarisha kuhusu jukwaa la wazi
kwa jamii maarufu kama ‘Semina ya Jinsia na Maendeleo (GDSS). Semina hii
hufanyikia viwanja vya TGNP Mabibo karibu na Chuo cha Taifa cha Usafirishaji
Mkabala na Soko la Mabibo. Kwa kawaida, semina hii/jukwaa hili huendeshwa mara
moja kwa wiki na huwa ni siku ya Juma Tano saa 9 alasisri mpaka 11 jioni (kwa
masaa mawili tu). Kulingana na Muktadha wa wakati huo, kwa kutumia mbinu
mbalimbali, mada raghbishi hutolewa kwa wanajamii ambapo masuala mbali mbali
huibuliwa kwa mjadala na baadaye kumalizia na mkakati wa nini kifanyike. Jukwaa
hili linatoa fursa kwa wanajamii wote, wanawake kwa wanaume, vijana na makundi
yote ya kijamii wakiwemo watu wenye ulemavu, waishio na VVU/UKIMWI, wanaharakati
wa haki za binadamu na za wanawake. Bila kujali jinsi, umri, dini, itikadi za
kisiasa, wanajamii huweza kukutana na kujadili mada mbalimbali za maendeleo na
kutoa kero zao. Pia katika semina hizi washiriki hupashana habari mbalimbali,
hujengeana uwezo, hujifunza, na kujenga mtandao wa vuguvugu la ukombozi wa
wanyonge na makundi ya pembezoni.
Hivyo, tunapenda kukualikeni, wadau wote na jamii yote, kuja kuhudhuria na
kushiriki pamoja na Mtandao wa Jinsia Tanzania katika
sherehe za siku ya kimataifa ya mtoto wa kike.
Mwaliko huu unatokana na kutambua juhudi na harakati
zenu katika kutetea haki za binadamu hususani makundi ya pembezoni, mfano
wasichana katika ukombozi wa maendeleo yao.
Kuhudhuria na kushiriki kwenu, kutawezesha
mafanikio ya semina hiyo na siku ya mtoto wa kike duniani. Pia naomba
kuzingatia kuwa usafiri wa kuja na kurudi ni wa kujitegemea. Huduma ya mkalimani
wa viziwi itatolewa.
Wenu katika harakati
za kutetea haki za wasichana na kuinua vipaji vyao.
No comments:
Post a Comment