TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday 17 January 2013

wakazi wa Arusha wachukua hatua kutimiza wajibu wao



                                                TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 
Tarehe: Alhamisi, Januari 17, 2013 
Imezuiliwa hadi: Alhamisi 17, Januari, 2013 
Wasiliana na: Chiku Lweno–Aboud Simu: 754588233 
Email: c.lweno-aboud@evidence4action.net 
Mama Ye! yazinduliwa: wakazi wa Arusha wachukua hatua kutimiza wajibu wao ili kuokoa maisha ya akinamama na watoto wachanga Tanzania 
Leo (Alhamisi Januari 17, 2013), Kampeni ya Mama Ye! kwa ajili ya kuokoa maisha ya akinamama na watoto wachanga wa Tanzania imezinduliwa katika Viwanja vya Makumbusho, jijini Arusha. Shamra shamra za uzinduzi huo ziliambatana na harakati kubwa za uhamasishaji uchangiaji damu kwa hiari ambapo zaidi ya wachangiaji 750 wamejitokeza kutoa damu kama mchango wao kuokoa maisha ya akina mama na wachanga. 

Mama Ye! ni wito wa utekelezaji. Ni kampeni inayomtaka kila Mtanzania kuchukua jukumu na kujituma kufanya jambo litakalo okoa uhai wa mama zetu na watoto wachanga. Kujitolea kuchangia damu ni moja ya hatua nyingi zinazoweza kuchukuliwa na wanajamii kulinda uhai wa akina mama na watoto wachanga. 

Mnamo wiki iliyopita, Evidence for Action Tanzania, Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Hospitali ya Mkoa Arusha, na Tawi la Shirika la Msalama Mwekundu wameshirikiana kwa ukaribu katika uhamisishaji na kuendesha zoezi la uchangiaji damu jijini humo. 
Dr Effesper Nkya , Meneja Mpango kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama amesema: 

“Asilimia 80 ya damu yote inayochangwa nchini hutumika kuokoa maisha ya akina mama na watoto na hata hivyo bado kuna upungufu mkubwa kikanda, na kitaifa kwa ujumla.” 

Akizindua kampeni hiyo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Jowika Kasunga, ambaye ni Mkuu wa wilaya ya Monduli, amehimiza Watanzania wote bila kujali ni wa kundi gani, kujiwajibisha na kuchukua hatua zitakazochangia kulinda uhai wa akinamama na watoto wachanga. Hasa hasa, ametoa changamoto kwa wale wanaokata tamaa na kukubaliana na imani kuwa hatma ya kifo cha mama na mtoto wakati wa kujifungua kuwa ni jambo la kawaida. 

“Leo natoa changamoto kwa wale wanaoona ni jambo la kawaida msiba kutokea. Wote tunatakiwa kulaumiwa kwa kuangalia tu, bila kuchukua hatua na kutokuwa makini kuhusiana na maisha ya akina mama na watoto. Kwa uhakika kabisa sio kwamba hatujali uhai wa mama na mtoto unapopotea--la hasha. Ila inakuwa kama tunahisi hakuna tunachoweza kufanya kubadili hali hii ya kusikitisha. Si kweli. Tuna nia ya dhati, nguvu na uwezo wa kuokoa maisha—kama ambavyo wachangiaji damu wa Arusha walivyoonyesha.” 

Kampeni ya Mama Ye! imeanzishwa na Evidence for Action (E4A), ambao ni mpango wa miaka kadhaa wenye lengo la kukuza/kuongeza uwezekano wa kuishi kwa akina mama na watoto wachanga katika nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara. Uzinduzi huo wa wito wa kuchukua hatua kupitia uchangiaji damu, unaenda sambamba na Mkutano wa Kimataifa kuhusu Afya ya Akinamama unaofanyika Arusha. Kwenye mkutano huo wataalamu mahiri duniani wanajadiliana hatua za kuchukua kupunguza vifo vya wanawake na watoto wachanga. Uzinduzi wa kampeni ya Mama Ye! ni fursa muafaka kuonyesha hadhira ya kitaifa na kimataifa ni jinsi gani jamii inaweza kuchangia katika kuokoa maisha. 
Craig Ferla, Mkurugenzi wa E4A Tanzania, amesema: 

“Wanawake wengi zaidi wa Tanzania wanavuka salama kipindi cha ujauzito na kujifungua wakiwa salama miaka ya sasa kuliko ilivyokuwa hapo nyuma, lakini bado kazi kubwa ipo mbele yetu kuokoa wengi zaidi. 

“Tunafahamu kuwa mabadiliko yanawezekana. Iwapo wewe ni dereva wa taxi unayeweza kumsaidia mjamzito kufika kliniki iliyo karibu; kama ni msichana unayesomea ukunga au ni kijana unayemhimiza dada yako kuhudhuria kliniki; wewe pia unaweza kuleta mabadiliko. Kila siku hapa Tanzania wanawake na wanaume kama wewe wanachukua hatua za kuleta mabadiliko na kuokoa maisha. 
“Wakazi wa Arusha wamejitokeza kwa wingi. Tufuate mfano wa hawa Mashujaa wa Arusha. Sasa ni zamu ya Watanzania wengine kujiunga na kampeni na kuwa Mashujaa wa Mama Ye! 

“Je wewe utafanya nini kusaidia kuokoa uhai wa akina mama na watoto wachanga?” 
Tanzania imepiga hatua katika miaka ya hivi karibuni katika kuongeza uwezekano wa kuishi miongoni mwa akina mama na watoto wachanga. Licha ya hili, kila mwaka akinamama zaidi ya elfu nane na wastani wa watoto wachanga elfu hamsini hufariki kutokana na uzazi. Wengi kati ya hawa wangeishi iwapo fursa ya kupata huduma salama ya afya ingekuwepo kwa wakati muafaka, ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa damu ya kutosha hospitalini. 


Maelezo na taarifa zaidi wasiliana au fuatilia kurasa zifuatazo 
c.ferla@evidence4action.net 
Facebook.com/MamaYeTZ 
Twitter.com/MamaYeTZ 
Ends 

No comments:

Post a Comment