TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Friday, 8 March 2013

Siku ya wanawake duniani:Uelewa wa masuala ya jinsia bado kikwazoMkurugenzi Mtendaji wa Mtandano wa Jinsia Tanzania(TGNP) Usu Mallya
WAKATI dunia nzima inaadhimisha siku ya wanawake  ambayo hufanyika Machi, 8 ya kila mwaka, Wanawake  Wakatoliki Tanzania(WAWATA)  wametaka wanawake nchini kuchukua hatua ya kuombea amani ya Tanzania,  huku Mtandao wa Jinsia Tanzania ( TGNP)  ukisema  uelewa wa masuala ya jinsia bado ni kikwazo katika kupambana na ukatili wa kijinsia.


Akizungumza na Blogu hii, Mwenyekiti wa Wanawake Katoliki Tanzania ( WAWATA) Bi. Olive Luena  amesema wananawake wana changamoto ya kuliombea taifa ambalo kwa sasa liko katika kipindi kigumu cha mahusiano kati ya dini na dini na watu kujichukulia sheria mkononi.

Bi. Luena amesema wanawake wote bila kujali dini zao wafunge na kuombea taifa amani ili iweze kuwepo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.

“Wanawake tukae pamoja, tumlilie Mungu aliokoe taifa letu lisiingie katika machafuko ambayo dalili zake zimeanza kuonekana na kuleta hofu kwa watu wetu,” amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi  Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania Usu Mallya anaeleza kuwa ukosefu wa uelewa wa masuala ya kijinsia ni kikwazo kikubwa cha kupambana na tatizo la ukatili wa kijinsia katika ngazi ya jamii hadi kitaifa.

“Kuna changamoto kubwa ya kukosekana kwa uelewa mpana wa dhana ya usawa na haki za kijinsia ambayo imesababisha hata mgawanyo wa rasilimali katika maeneo mbalimbali kutozingatia hali halisi na mahitaji ya kijinsia , mfano uandaaji wa bajeti za kiserikali, ujenzi wa miundombinu, utoaji wa huduma za kijamii kama maji, afya na  chakula,”anasema.


Anasema kutokana na changamoto hizo wanatumia fursa ya siku ya wanawake kupaza sauti zao kudai haki ya kuangalia suala la usawa wa kijinsia, wanawake wanapata haki zao za msingi hasa katika suala la matibabu, uzazi salama, elimu, maji salama, ushiriki wa kutosha katika nafasi za ajira ngazi zote na ushiriki sawa katika nafasi za maamuzi na ulinzi wa kutosha kutokana na kukithiri kwa ukatili wa kijinsia.
Mallya anasema “tumetambua kuwa uelewa wa masuala ya kijinsia ni pamoja na kuyaingiza kwenye katiba mpya kama sheria mama ya nchi, kuweka mikakati ya kuingiza masuala ya wanawake katika sera, mipango na bajeti kila mwaka,”.

Naye  Mkurugenzi wa Mfuko wa wanawake Tanzania (TWF) Mary Rusimbi  anabainisha  kuwa uelewa wa masuala ya kijinsia  kwa wanawake na wanaume umeongezeka , ingawa bado wanaonekana kurudi nyuma na kuruhusu ukatili wa kijinsia kuendelea kufanyika nchini kuanzia majumbani, sehemu za kazi na maeneo mengine.
Anasema jambo la kufanya, ni asasi mbalimbali nchini ziungane  na kuwa kitu kimoja katika kuhakikisha kuwa zinaendelea kutoa elimu kuanzia vijijini ili kujenga uelewa zaidi kwa jamii.

Anasema  ni muhimu wanawake wawe wahitaji na kuunganisha nguvu zao ili mabadiliko makubwa yaweze  kutokea. Wasipokuwa ni wahitaji nani atawasemea?

Mama Rusimbi anasema siku za nyuma Wizara ndio ilikuwa ina kazi kubwa ya kwenda kuelimisha jamii, lakini kwa sasa kuna asasi nyingi  ambazo zimekuwa mstari wa mbele katika kutoa elimu, zinahitajika kutumia fursa walizonazo na kuongeza kasi ya uelewa hasa katika maeneo ambayo  bado hayajapata elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya kijinsia.
Lakini anawakumbusha watunga sera na waandaji wa bajeti, kuweka mkakati wa pamoja utakaolenga kuwaletea wanawake maendeleo.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Msaidizi wa Umoja wa Mataifa na Mkurugenzi Mkuu wa  Shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya Watu (UNFPA) Dk. Babatunde Osotimehin anaeleza kuwa duniani kote wanawake na wasichana wanakabiliwa na vitendo mbalimbali vya ukatili wa kijinsia  ikiwa ni pamoja na ubakaji,ukeketaji, ndoa za utotoni na ukatili wa kingono.

“Tukiwa miongoni mwa jumuiya ya kimataifa tuna jukumu la kuhakikisha ukiukwaji wa haki za binadamu unatokomezwa,”anasema.
Anasema hii ni changamoto kubwa ambayo inaweza kufanyiwa kazi ikiwa tu wanawake wataungana na kuwa na lengo moja la kuhakikisha kuwa wanawake na wasichana wanakuwa salama dhidi ya vitisho vya ukatili wa kijinsia.
“Hii ni fursa yetu ya kuleta mabadiliko chanya kwa maisha ya mamilioni, hatuwezi kupoteza fursa hii,”anasema.
Aidha, Afisa tawala na Mratibu wa Masuala ya Jinsia na Ukimwi wa Wizara ya Katiba na Sheria Joyce Mloe anasema bado kuna changamoto kubwa  kuhusiana na uelewa wa masuala ya kijinsia kwa jamii, watu wanafikiri yanahusu wanawake pekee kumbe ni jambo la watu wote.

“Kuna umuhimu mkubwa wa kutolewa kwa elimu ya kutosha kuhusiana na masuala ya jinsia, na sisi kama Wizara ya Katiba na Sheria tunaendelea na mkakati wetu wa kuelimisha jamii, kuhusu sheria mbalimbali na masuala ya jinsia kupitia vyombo vya habari,”anasema.

Anasema Wizara imeanzisha dawati maalum ambalo huwa linatoa huduma za kisheria kwa wananchi wenye matatizo mbalimbali

Mloe  anasema wanawake waungane kusimamia haki zao hasa kwa kujitokeza katika mchakato wa ukusanyaji wa katiba mpya na kuzungumzia sheria zote kandamizi ili hatimaye ziweze kurekebishwa.
Hata hivyo, bado makundi yaliyoko pembezoni hayatanufaika ipasavyo huduma zilitolewazo na Wizara hiyo kwa vile huduma zao nyingi zipo mjini. Nilipohoji vipi kuhusu walioko pembezoni watahudumiwaji ikiwa wengine hawana redio na runinga.
Kwa mujibu wa Mloe anasema kuwa elimu ya sheria na huduma za sheria na haki za binadamu zitafika maeneo ya vijijini kwa kutegemea zaidi kutoa elimu yao kupitia vyombo vya habari.
Hata hivyo, Siku  ya  wanawake duniani  imekuwa ikitumiwa  na wanawake kukaa kwa pamoja na kujadili changamoto ambazo zimekuwa zikiwakabili  wanawake ikiwa na lengo ya kuzitafutia ufumbuzi ili hatimaye waweze kupata haki zao.
Maadhimisho ya mwaka huu yanaoongozwa na kauli mbiu inayosema “Uelewa wa masuala ya jinsia katika jamii:Ongeza kasi”.
Uelewa wa masuala ya jinsia katika jamii huelezwa bado ni kikwazo kikubwa katika maendeleo ya wanawake Tanzania kutokana na mfumo uliojenga tangu enzi za mababu. Ni asilimia ndogo ya watu wanauelewa wa kutosha kuhusiana na masuala hayo lakini asilimia kubwa ya makundi yaliyokuwa pembezoni hayaelewi kutokana na mfumo unaoelezwa kuwa ni Ubepari.
Ili uelewa uweze kufika, wanawake wote walioko katika makundi yao ni kutumia fursa walizonazo kuelimisha wengine. Inawezekana ikiwa wanawake watakuwa na umoja.


No comments:

Post a Comment