TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday 13 November 2013

Kontena la pembe za ndovu lanaswa

 Na Gazeti la Tanzania Daima
Asha Bani 

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, amekamata kontena la futi 40 likiwa limesheheni pembe za ndovu kisiwani Unguja, Zanzibar jana alasiri.

Akizungumza na Tanzania Daima  kwa simu kutoka kisiwani humo, Waziri Kagasheki alisema kuwa kontena hilo lilikuwa likitokea Bandari ya Dar es Salaam na kwamba watu wawili wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi wakilisaidia Jeshi la Polisi.

Waziri Kagasheki alisema kuwa hadi sasa haijulikani mzigo huo una thamani kiasi gani na kwamba unasadikiwa kumilikiwa na raia wa China.

Alisema kuwa operesheni hiyo ni endelevu ili kuwabaini wahusika wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ya ujangili.

Tukio hilo linakuja zikiwa ni wiki mbili tangu waziri huyo kukamata pembe za ndovu 706 jijini Dar es Salaam zikimilikiwa na raia wa China.

Pembe hizo 706 ni sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi za wanyamapori hapa nchini.

Wachina hao walikamatwa katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni wilayani Kinondoni chini ya operesheni iliyoongozwa na Waziri Kagasheki, ambaye aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tarish Maimuna.

Waliokamatwa na shehena hiyo ya pembe za ndovu ni raia watatu wa China, ambao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa Guandung, ambao wamefikishwa mahakamani wiki iliyopita.

No comments:

Post a Comment