TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Thursday, 27 June 2013

Obama atakiwa kusisitiza uhuru Afrika

 Huku Rais Barack Obama akianza safari yake barani Afrika, Shirika la Haki za Binaadamu la Human Rights Watch limemtolea wito kutumia ziara hiyo kuunga mkono vyombo vya habari na makundi huru ya wanaharakati barani humo. 

Kupitia taarifa yake iliyosambazwa kwa vyombo vya habari, Human Rights Watch imesema kwamba Rais Obama anafanya ziara kwenye bara ambalo vyombo vingi vya habari na makundi ya kutetea haki yanakandamizwa na serikali husika, ingawa haikuzitaja nchi tatu anazozitembelea Rais Obama kuwa ni miongoni mwao.

Rais huyo wa Marekani anazitembelea Senegal, Afrika ya Kusini na Tanzania, ikiwa ni miaka mitano tangu atoe hotuba maarufu mjini Accra, Ghana, ambapo alizungumzia umuhimu wa asasi za kijamii na uandishi huru wa habari kwa jamii za kidemokrasia.

Daniel Bekele, mkurugenzi wa Human Rights Watch kanda ya Afrika, amesema kwamba lazima Rais Obama atumie ziara hiyo kutambua ujasiri wa waandishi wa habari na wanaharakati wa Kiafrika ambao wanasema ukweli licha ya vitisho na ukandamizaji, na pia awatake maraisi wenzake kufanya hivyo hivyo.

"Lazima awaambie wazi viongozi wa Kiafrika kwamba vyombo vya habari na makundi ya wanaharakati ni muhimu kwa maendeleo na lazima wakubalike." Amesema Bekele.


Hali mbaya kwenye Pembe ya Afrika

 Shirika hilo la haki za binaadamu limesema kwamba vyombo huru vya habari vimekuwa vikizidi kukabiliwa na kitisho katika nchi nyingi za Afrika, likipigia mfano hali ilivyo kwenye nchi za Pembe ya Afrika hasa Ethiopia, Eritrea na Somalia katika siku za hivi karibuni.

Kwenye eneo hilo kuna matukio mengi zaidi ya waandishi wa habari kushambuliwa, kuteswa na hata kuuawa, ambapo wengine wengi wamekimbia mashambulizi na kesi zenye mashiko ya kisiasa.

Tangu mwaka 2011, Ethiopia, kwa mfano, imekuwa ikitumia sheria za kupambana na ugaidi kukabiliana na waandishi wa habari, na kufikia sasa imeshawatia hatiani waandishi 11.

Nchini Burundi, sheria mpya ya vyombo vya habari inakosolewa kuuchafua vibaya uhuru wa habari, kwa inahujumu haki ya kulindwa kwa vyanzo vya habari, inawapangia waandishi wa habari mada maalum ambazo wanaweza kuziripoti na inaweka adhabu kali ya kutozwa fedha kwa wale wanaovunja sheria hiyo.

Ukandamizaji kila pahala
Hali inayofanana na hiyo inatajwa na Human Rights Watch kwamba ndiyo iliyoko kwenye nchi nyengine kadhaa za Kiafrika, zikiwemo Sudan ya Kusini, Uganda, Mali, Zimbabwe na Rwanda.

Hata Afrika ya Kusini kwenyewe, moja ya nchi ambazo Rais Obama anazitembelea, kile kinachoitwa Mswaada wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa za Serikali, ama "Mswaada wa Usiri" kwa jina jengine, unatajwa kuwa kigingi kingine kwa uhuru wa habari barani Afrika.

Human Rights Watch imemtaka Rais Obama sio tu kuzungumzia mafanikio ya bara la Afrika kwenye ziara yake, bali pia anapaswa kutuma ujumbe wa kuheshimiwa kwa haki za binaadamu kama kigezo muhimu kwa maendeleo ya muda mrefu ya Afrika.
 Source:DW Swahili
Mwandishi: Mohammed Khelef/HRW
Mhariri: Josephat Charo

No comments:

Post a Comment