“NINGEKUWA
na uwezo ningewakusanya wasanii wote wa muziki wa injili nikawaambia hebu tuimbe pamoja na kutoa albam
ya pamoja, lakini ni jambo gumu kufanya hivyo,”
ndivyo asemavyo msanii wa muziki
wa injili Martha Mwaipaja.
Ni msanii
kijana ambaye amekuwa akifanya huduma ya uimbaji sio tu katika kumnufaisha
yeye, akiwa amelenga kuwapa watu ujumbe wa Mungu.
Anasema kwa
kusikiliza muziki wa injili watu wengi wamekuwa wakiponywa kiroho na kubadilika
matendo yao, kwa kuacha mabaya, na kumgeukia Mwenyezi Mungu.
Hilo kwake
linampa faraja kubwa hasa kuona kuwa muziki wake umekuwa ukiwabadilisha watu.
Wasikilizaji au mashabiki wake wamekuwa wakimuunga
mkono katika kununua na kusikiliza na hatimaye kuelimika na kubadilika
kimatendo.
Anasema
alianza kuimba muziki akiwa ni mtoto mdogo. Alilelewa katka mazingira ya kidini
ambayo yalimjenga kimaadili.
Msanii
huyo amekuwa akiimba nyimbo zake kwa
mtindo wa taratibu na kwa unyenyekevu. Kwa watu ambao wamekuwa wakimfuatilia wanatambua
kipaji cha pekee alicho nacho mwimbaji
huyo.
Anasema mara
nyingi unaweza kuwa unawaza kufanya jambo fulani lakini lisifanikiwe. Katika
historia yake ya muziki jambo ambalo alitamani kulifanya ni kushirikiana na
wanamuziki wanzake wa muziki wa injili na kufanya huduma ya pamoja.
Hiyo ilikuwa
ni ndoto ambayo bado anahisi kuwa ni jambo gumu kukubalika kwa wasanii wenzake.
Wengi
wamekuwa wakifanya kazi peke yao wakitegemea kunufaika, jambo la kufanya
pamoja, labda ingekuwa kwa wimbo mmoja lakini kutoa albam moja ni kitu kigumu.
Mwimbaji
huyu ambaye ni mwenyeji wa Mbeya anasema hafanyi sanaa bali ni huduma.
Akimaanisha kuwa anachokiimba amelenga
kiwaponye watoto, vijana, wazee na watu wote wanaomsikiliza.
Licha ya
kuwa alianza huduma hiyo akiwa ni mtoto lakini rasmi alianza kuimba muziki
mwaka 2011 na wakati huo alikuwa ni kijana mwenye umri wa miaka 21.
Ndani ya
mwaka huo alifanikiwa kutoa albam inayofahamika usikate tamaa yenye nyimbo nane
kama vile wewe ni baba, tulipotoka ni mbali, asante Yesu, Bwana ni nuru, mimi
ni mpitaji, na mataifa yote yamshukuuru Mungu.
Anajivunia
kuwa albam hiyo imempa matunda makubwa ingawa hakupenda kusema ni matunda gani
, lakini zaidi akilenga kwamba watu wengi wamebarikiwa kupitia nyimbo hizo.
Karibu
nyimbo zake zote zilikuwa zikifanya vizuri katika chati za muziki wa injili na
hivyo kumtambulisha kitaifa na kimataifa.
“Nashukuru
Mungu albam yangu ya kwanza iliweza kufanya vizuri kwasababu nilikuwa
nikialikwa kufanya huduma ya injili kupitia uimbaji sehemu mbalimbali hapa
nchini, lakini pia, nimefanya huduma Kenya, hii inanipa faraja kubwa kuona kuwa
watu wanabarikiwa,”anasema Martha.
Wapo baadhi
ya wasanii hasa wanaoimba muziki wa kidunia wamekuwa wakitoa wimbo mmoja mmoja,
wakidai kuwa ndio unalipa kwa vile wamelenga zaidi kwenye biashara.
Wengi
wanapotoa wimbo mmoja hutegemea kupata shoo ambazo humlipa zaidi. Wanasema
albam hailipi, ndio maana hawatoi.
Kwa upande
wa muziki wa injili ni tofauti kidogo, licha ya kuwa wamelenga kutoa huduma kwa
asilimia wengi ni lazima watoe albam.
Mashabiki wa
muziki wa injili hupendelea kununua albam ya msanii mmoja,mmoja kutokana na
kuvutiwa na jinsi anavyoimba na anavyopokea uponyaji.
Martha ana
albam ya pili kwa sasa inayofahamika kama ombi langu kwa Mungu ambayo nayo
huendelea kufanya vizuri sokoni. Ndani yake kuna nyimbo nane kama jaribu kwa
mtu, nabii wa mtu ni wa karibu, Yesu ni mzuri,
kweli nimetambua, kaa nami tena, nani ajuae na sifa zivume.
Anasema “nawomba
mashabiki wangu waendelee kuniunga mkono katika huduma hii, kwa sasa albam
yangu iko sokoni, natumai kwamba kwa kusikiliza nyimbo zangu mtazidi
kubarikiwa,”.
Akizungumzia
zaidi kuhusu album yake hiyo mwimbaji huyo ambaye alifunga ndoa mapema mwaka
jana na mchungaji wa Kanisa la Udhihirisho John Said, amesema anamshukuru Mungu kwani
tayari kila anapoenda kwenye huduma watu tayari wamekuwa wakibarikiwa na
kukutana na Mungu kupitia nyimbo hizo mpya kama ilivyokuwa kwa album yake ya
kwanza iitwayo ''usikate tamaa''
Hata hivyo,
kutokana na kuendelea kufanya vizuri katika anga ya kimataifa kwa mwaka huu
nyota yake iling’ara baada ya
kupendekezwa kwa mara ya kwanza kuwania tuzo za injili za Afrika ziitwazo
Africa Gospel Music Awards(AGMA) ambazo zilitarajiwa kutolewa jijini London. Kitendo
cha kupendekezwa kwenye tuzo hizo, zilionyesha kukubalika kwake kwenye ukanda
wa Afrika na hata Ulaya licha ya kuwa wakenya wengi na wasanii wa Afrika
walionekana kufanya vizuri zaidi.
Martha
mwenye sura ya upole anazungumzia suala la kuokoka kuwa si kazi ngumu bali
kuutunza wokovu ndiyo kazi.
Aliwahi
kusema kuwa si jambo la ajabu kusikia
mtu amesimama madhabahuni na kutangaza kuwa ameokoka na kupigiwa makofi na
waamini kutokana na uamuzi huo. Lakini siri ya wokovu hubaki moyoni mwa
mhusika.
Anasema
maisha yake yote anategemea wokovu kwani ndiyo dira yake ya kumwezesha
kufanikiwa kwa kila jambo, atakuwa
karibu na Mungu hivyo itakuwa rahisi kujibiwa mahitaji yake atakayokuwa
anayomba kutoka kwa Muumba wake.
“Mungu
anasema ukimheshimu naye atakuheshimu, sipendi niwe kama bango la kuwaelekeza
watu kwenda kwenye uzima wa milele halafu mimi niende jehanamu. Nawaomba
waimbaji wenzangu tuwe mfano kwa jamii
inayotuzunguka,”anasema.
Anawaeleza waimbaji wenzake kuwa na umoja ili
kudhihirisha ukweli kwamba wao ni watumishi wa Mungu wanaositahili kuigwa
na jamii inayowazunguka.
Martha
anategemea kupata mtoto wake wa kwanza siku za karibuni hivyo anamwomba Mungu
awe pamoja naye katika kuisimamia na
kuitengeneza familia yake mpya.
Mwisho.
well said
ReplyDelete