WAKATI dunia
inaadhimisha siku ya wakimbizi duniani leo, Shirika la Umoja wa Mataifa la
wakimbizi(UNHCR) limesema bado kuna ongezeko la idadi kubwa ya wakimbizi au
wakimbizi wa ndani duniani huku Tanzania
idadi hiyo ikiwa imepungua.
Akizungumza
na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Mwakilishi wa UNHCR nchini
Joyce Mendes-Cole alisema ripoti ya shirika hilo imeonyesha ongezeko la
wakimbizi kutoka wakimbizi milioni 42.5 mwaka 2011 hadi kufikia milioni 45.2
mwishoni mwa mwaka jana.
Alisema “kati ya
idadi hiyo yaani milioni 45.2,
kuna idadi ya wakimbizi milioni 15.4 wakati wanaotafuta makazi wapo 937,000 na watu
milioni 28.8 ni wale wanaondoka kwenye makazi yao na kukimbilia katika maeneo
mengine ndani ya nchi yao kutokana na sababu mbalimbali,”.
Cole alisema
sababu kubwa inayochangia ongezeko hilo ni vita ambapo asilimia 55 ya wakimbizi
wote wanatoka katika nchi za
Afghanistan, Somalia, Iraq, Syria na Sudan.
Kwa upande
wa Tanzania, alieleza kuwa idadi ya wakimbizi imepungua tofauti na siku za
nyuma kutoka wakimbizi waliokuwepo 700,000 hadi kubakia 102,000 hivi leo.
Alisema
wakimbizi wengi waliokuwepo nchini tayari walisharudishwa makwao na wengine
16,000 walitafutiwa makazi katika nchi nyingine.
Aliongeza
kuwa Tanzania ni nchi ya tano duniani yenye
kambi kubwa ya kuwahifadhi wakimbizi inayofahamika kama Nyarugusu ambapo ina jumla ya wakimbizi 68,000, wengi wakitokea Jamhuri ya Kongo
ambayo ni nchi ya sita inayotoa idadi
kubwa ya wakimbizi.
Cole alisema
changamoto kubwa iliyojitokeza ni kuhusiana na wakimbizi wa Burundi wapatao
162,000 waliopewa hadhi ya uraia wa Tanzania kama wakulima katika mkoa wa
Tabora na Katavi mwaka 2009/2010 kuwa
bado hawajapewa nafasi ya umiliki wa ardhi.
Kutokana na
changamoto hiyo, alisema ni muhimu hatua ichukuliwe mapema ili kuwaruhusu kuishi kwa haki na
amani.
No comments:
Post a Comment