Na Thehabari.com,
Kishapu
MBUNGE wa
Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jimbo la Kishapu mkoani Shinyanga, Seleiman Nchambi
amewaomba wapiga kura wake kuwa wavumilivu juu ya ahadi ya huduma za maji safi
na salama alizozitoa wakati akigombea jimbo hilo katika uchaguzi mkuu 2010.
Nchambi
ametoa kauli hiyo hivi karibuni akizungumza na mwandishi wa habari hizi kutoa
ufafanuzi juu ya malalamiko ya baadhi ya wapigakura wake wa Kata ya Kishapu,
ambao wamelalamikia kitendo cha kuendelea kutopata huduma za maji safi na
salama eneo lao ilhali mbunge wao aliwaahidi kuwapatia huduma hiyo.
Mbunge huyo
alikiri kutoa ahadi ya huduma ya maji jimbo zima la Kishapu na utekelezaji wa
ahadi zake unaenda awamu kwa awamu kama alivyopanga. Akifafanua zaidi alisema
aliingia madarakani na kukuta sehemu kubwa ya jimbo hilo halina huduma ya maji
safi na salama, lakini kwa jitihada zake mpaka sasa tayari amefanikiwa baadhi
ya vijiji kuvipatia maji.
"Niliahidi
maji jimbo zima la Kishapu yaani jumla ya vijiji 114, wakati naingia madarakani
nimekuta hali ni mbaya ya huduma za maji...lakini hadi sasa tunapozungumza
zaidi ya vijiji 30 vinapata maji safi na salama huku jitihada zingine
zinaendelea," alisema Nchambi akifafanua juu ya kilio cha huduma za maji
akizungumza kwa njia ya simu.
"Ahadi
yangu mimi ni miaka mitano, ilani ya CCM ni ya miaka mitano, ninaenda kwa awamu
yaani vijijini 10 kwa kila mwaka kwa wilaya," aliongeza kusema mbunge
huyo.
Awali
uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hizi kwa baadhi ya vijiji vya Kata
ya Kishapu, mkoani Shinyanga, vikiwemo vijiji vya Lubaga, Isoso, Mwanuru pamoja
na Kishapu ulibaini kuwepo na shida kubwa ya huduma ya maji safi na salama hali
inayowalazimu wananchi kutembea umbali mrefu hasa kipindi cha kiangazi kutafuta
maji.
Hata hivyo
uchunguzi ulibaini mzigo mkubwa wa kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama
katika familia unawaangukia wanawake na wanafunzi ambao hutumia muda mrefu
kusaka maji kwa ajili ya matumizi ya familia. Chanzo pekee cha maji ambacho
hutegemewa na maeneo mengi ya vijiji ni cha Mto Tungu ambao nao hukauka kipindi
cha kiangazi na wananchi kuendelea kupata maji kwa shida.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti hivi karibuni viongozi wa vijiji vya Lubaga, Isoso, Mwanuru
na Kishapu walilalamikia kitendo cha wao kuendelea kuteseka kwa huduma za maji
ilhali walipewa ahadi ya kuletewa huduma hiyo na mbunge wao kipindi cha
kampeni.
Ofisa
Mtendaji wa Kijiji cha Lubaga, Enock Manyenye Shimba alisema mwaka 2010 wakati
wa kampeni za Uchaguzi Mkuu kijiji chao kilipewa ahadi ya kuchimbiwa visima
virefu vya maji na Mbunge wa Jimbo la Kishapu, Seleiman Nchambi lakini
anashangaa ahadi hiyo haijatekelezwa hadi leo.
Naye Kaimu
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, George Kessy alikiri hali mbaya ya huduma
ya maji Wilaya nzima ya Kishapu kutokana na eneo hilo kutokuwa na chanzo cha
maji cha uhakika. Hata hivyo alisema juhudu zinafanywa kuhakikisha uongozi unaondoa
kero hiyo ya huduma ya maji kwa wananchi.
"Ni
kweli suala la maji ni Tatizo kwa wilaya nzima ya Kishapu, tena ni kubwa sana…,”
alisema Kessy.
No comments:
Post a Comment