TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
BABU WA SAMUNGE
AITABIRIA MAKUBWA TANZANIA
MCHUNGAJI Ambilikile Mwaisapila wa
Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) amesema Mungu ameendelea
kujifunua kwake na kumuonyesha kuwa Tanzania itakuwa kioo cha Afrika na baadaye
kioo cha dunia.
Ametoa kauli hiyo jana asubuhi (Jumanne,
Septemba 24, 2013) mbele
ya Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Samunge, wilayani
Ngorongoro mkoani Arusha wakati msafara wa Waziri Mkuu uliposimama nyumbani
kwake ili kumsalimia akiwa njiani kurejea mjini Arusha.
Mchungaji Mstaafu
Mwaisapila maarufu kama Babu wa Samunge alisema kuna mambo mengi ambayo
yameandikwa kwenye Biblia lakini hayakutokea Israeli na sasa yatafanyika hapa Samunge.
“Mungu ametupenda sana, yanakuja mambo makubwa na wala hayako mbali. Kama mimi
ni mzee na nitayaona, kwa hiyo mtarajie kuwa hayako mbali kutokea,” alisema
huku akishangiliwa.
Alisema katika
mafunuo aliyopewa na Mungu ameonyeshwa kwamba watu wengi zaidi watafurika
kijijini Samunge kuliko ilivyokuwa hapo awali. Alitumia fursa hiyo kuishukuru
Serikali kwa misaada iliyotoa wakati wa ‘kugawa kikombe’ ikiwemo mahema, maji
na ulinzi.
Waziri Mkuu
ambaye yuko mkoani Arusha kwa ziara maalum ya kusikiliza matatizo ya ardhi
yanayowakabili wakazi wa wilaya ya Ngorongoro, katika tarafa za Ngorongoro,
Loliondo na Sale alisema anakubaliana na utabiri wa Mch. Mwaisapila kwani
Tanzania imejaliwa gesi nyingi na mafuta mengi ambavyo vitabadili sura ya Taifa
hili.
“Mungu ametupa
gesi nyingi sana, katika miaka miwili tutakuwa na umeme kila mahali. Tuna makaa
ya mawe ambayo ni nishati kubwa na sasa tuna fursa ya kupata nishati ya umeme
kutoka ardhini (geo-thermal) katika Ziwa Natron,” alisema.
Alisema Tanzania
imekuwa kimbilio la kila mwekezaji na sababu kubwa ni amani na utulivu uliopo
nchini.
Aliwaeleza
wakazi wa Samunge kwamba mapema mwakani mkandarasi wa barabara atakuwa katika
eneo lao kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya lami ambapo awamu ya kwanza
itaanzia Wasso hadi Mto wa Mbu kupitia Samunge.
Akitoa ombi
maalum kwa niaba ya vijana mbele ya Waziri Mkuu, Bw. Elias Kalumbwa alisema
wanaomba kuchimbiwa bwawa ili waweze kujiajiri kupitia kilimo cha mbogamboga na
matunda.
Bw. Kalumbwa
ambaye amesomea masuala ya wanyamapori alisema eneo la kuchimba bwawa lipo
katika mto wa msimu unaopita kijijini hapo. “Eneo la kuchimba bwawa lipo katika
mto wetu, vijana tunaweza kujiajiri endapo tutapata bwawa ili tufanye kilimo
cha umwagiliaji maji,” alisema huku akishangiliwa.
Naye Bibi Martha
Sereri (70) alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanaomba jimbo la Ngorongoro
ligawanywe kwa sababu ni kubwa sana kiasi kwamba inamuwia vigumu mbunge wao
kufika maeneo yote. Aliomba pia wapatiwe
walimu wa sayansi na hisabati kwa ajili ya shule 10 za sekondari zilizopo
kwenye tarafa yao.
Aliomba wapatiwe
mikopo ya matreka ili waweze kuongeza ukubwa wa mashamba yao. “Tunaomba mikopo
ya matrekta na plau, haya mashamba umeyaona njiani yamelimwa na Wakenya.
Ukikodisha trekta kila ekari unatozwa sh. 100,000/-. Je tutafika wapi?
Mkitukopesha matrekta mtakuwa mmetusaidia zaidi,” alisema.
Akijibu hoja
hizo, Waziri Mkuu alisema hoja zao ni za msingi na kwamba suala la vijana
kupatiwa bwawa ni jambo linalowezekana kupitia mipangpo ya maendeleo ya kilimo
ya wilaya (DADPS).
“Andaeni andiko
lenu, inabidi litoke kwa wananchi na siyo Serikalini. Mkituletea ni jambo
linalowezekana kwani liko ndani ya mipango ya wilaya.”
Akijibu hoja
kuhusu ukubwa wa jimbo, Waziri Mkuu aliwaambia wakazi hao kwamba inawezekana
kuongeza jimbo isiwe suluhisho la matatizo yao kwa sababu ya jiografia ya eneo
lao.
“Kuongeza jimbo
inaweza isiwe jibu la kila kitu kwani matatizo mnayopata yanatokana na
jiografia ya eneo lenu, kutoka Ngorongoro, Loliondo hadi huku Sale. Mimi
nadhani tuangalie pia uwezekano wa kuwapa Halmashauri ili kusogeza huduma kwa
wananchi. Tutaangalia njia zote mbili na kuona ipi italeta majibu ya haraka
kwenu,” alisema.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATANO, SEPTEMBA 25, 2013.
No comments:
Post a Comment