Na Mwinyi Sadallah, Mwananchi
Zanzibar.
Jina la Tanzania limechafuliwa tena baada ya meli ya mizigo ya Gold Star iliyosajiliwa nchini kukamatwa ikiwa na tani 30 za dawa za kulevya aina ya bangi zenye thamani ya Pauni za Uingereza 50 milioni (Sh125 bilioni).
Tukio hilo limetokea miezi miwili baada ya
Watanzania wawili kukamatwa na dawa za kulevya zenye uzito wa kilo 150
na thamani ya Sh6 bilioni kwenye Uwanja wa Oliver Tambo, Afrika Kusini.
Habari zilizothibitishwa jana na Mkurugenzi wa
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar (ZMA), Abdi Omar zilisema kwamba
meli hiyo ilikamatwa juzi ikiwa na mzigo huo wa bangi.
Alisema baada ya kupokea taarifa za kukamatwa kwa
meli hiyo kutoka kwa Polisi wa Kimataifa (Interpol), ofisi yake
iliwasiliana na wakala wake aliye na ofisi zake Dubai, Falme za Kiarabu,
Kampuni ya Philtex ambayo alisema inafanya kazi ya kusajili meli kwa
niaba ya Serikali na kuthibitisha kuisajili.
Alisema meli hiyo ilisajiliwa mwaka 2011 kwa kazi ya kubeba mizigo chini ya Kampuni ya Gold Star.
Alisema kutokana na tukio hilo, Kampuni ya Gold
Star imekiuka masharti ya Sheria ya Usajili wa Meli na ile ya Umoja wa
Mataifa zinazozuia meli kubeba dawa za kulevya na kuongeza kwamba ofisi
yake itafanya uchunguzi na kuchukua hatua.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Kitengo
cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa alisema naye amesikia kupitia
kwenye mitandao kwamba hajapata taarifa za kina... “Leo ni Jumapili ni
ngumu pia kupata taarifa rasmi kuhusiana na hili.”
“Kesho (leo) tutawasiliana na Polisi wa Kimataifa
(Interpol) ili kufahamu undani wa suala hili. Kuanzia hapo ndipo tutajua
nini kinachoendelea, kama waliokamatwa ni Watanzania au la na hiyo
bangi waliitoa wapi.”
Msemaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na
Majini (Sumatra), David Mziray alisema: “Sina taarifa za tukio hilo,
labda tuwasiliane kesho.”
Kama sinema
Taarifa zilizopatikana jana kwenye mitandao
mbalimbali ya kimataifa zinasema meli hiyo ilinaswa maofisa Forodha na
askari wa doria wa Italia waliokuwa Pwani ya Sicily, Bahari ya
Mediterania.
Msemaji wa Idara ya Ushuru Italia, alisema: “Meli
hiyo ilikamatwa baada ya kupatikana kwa taarifa za kiitelijensia kuwa
imebeba dawa hizo, lakini hatukutarajia kama kungekuwa na mzigo mkubwa
kiasi hicho na hata wahusika kuipiga moto.
Chanzo:http//mwananchi.co.tz/habari
Chanzo:http//mwananchi.co.tz/habari
No comments:
Post a Comment