CHAMA cha Wanahabari
Wanawake Tanzania (TAMWA) kimetaja mambo ya msingi ya kuzingatiwa katika
mchakato wa Katiba Mpya ili ujio wa katiba hiyo uweze kutokomeza mila kandamizi
na vitendo vya kikatili kwa wanawake.
Kauli hiyo
imetolewa jijini Dar es Salaam na mshauri wa masuala ya jinsia na mwanaharakati
wa haki za binadamu, Gemma Akilimali alipokuwa akitoa mada katika kikao cha
wahariri kutoka vyombo anuai vya habari nchini kilichofanyika makao makuu ya
TAMWA Sinza.
Akizungumza,
alisema vyombo vya habari havina budi kusimama kidete na kuhakikisha fursa ya
ujio wa katiba mpya inayoandaliwa hivi sasa inaweza kuondoa vikwazo na
mazingira ambayo yalikuwa kandamizi kwa wanawake.
“Tunataka
katiba Mpya ibatilishe sheria ambazo bado ni kandamizi; iendelee kubatilisha
sheria zote za ubaguzi wa jinsia, ikiwa ni pamoja na kukataza mwendelezo wa
tabia, taratibu na mila zenye kubagua na kudhalilisha wanawake na watoto wa
kike chini ya mfumo dume unaotawala jamii zetu,” alisema Bi. Akilimali.
Akifafanua
zaidi, alisema katiba haina budi kutamka wazi kuwa elimu itolewe bila kikomo
kwa jamii hiyo huku akishauri pia ibainishe kuwa nafasi za uongozi ziwe na haki
sawa ili kuleta usawa katika makundi yote hasa wanawake.
Aidha
alisema katiba mpya iwajibishe serikali kutekeleza mikataba yote ya kimataifa
iliyoridhia kuhusu haki za wanawake ikiwa ni pamoja na kuendeleza misingi
inayolinda utu wa mwanamke na uwepo wa mahakama ya kifamilia.
Mambo
mengine ambayo mwanaharakati huyo alitaka yawekwe wazi katika katiba hiyo, ni
pamoja na haki ya kunufaika na kumiliki rasilimali za nchi, haki za uzazi
salama, haki za huduma za msingi, haki za wanawake walemavu, haki za mtoto wa kike
na iwepo tume maalumu itakayo hakikisha uzingatiaji wa haki za wanawake katika nyanja
mbalimbali.
Alisema madai
yote hayo yamekuwa vikwazo kwa fursha nyingi kwa wanawake, hivyo vyombo vya
habari vinaweza kuendeleza mjadala huo wa madai ili kumsaidia mtoto wa kike
ambaye amekuwa akiminywa na mfumo uliopo kwa muda mrefu.
*Imeandaliwa
na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment