JUMLA ya watoto 137 na wajawazito 19 hufariki dunia kila siku
nchini Tanzania kwa matatizo yanayotokana na uzazi. Vifo vya watoto
pekee wanaopoteza maisha kutokana na matatizo hayo kwa mwaka hufikia
50,000 kwa nchi nzima.
![]() |
David Lyamuya |
Takwimu hizi za kusikitisha zimetolewa leo jijini
Dar es Salaam na Meneja Mradi wa mpango wa 'Wajibika Mama Aishi', Bw.
David Lyamuya toka Taasisi ya Utepe Mweupe katika semina ya wahariri na
waandishi wa habari waandamizi.
Lyamuya alisema mbali na idadi hiyo kubwa ya
akinamama pamoja na watoto kupoteza maisha yapo matukio mengine ya vifo
ambayo hayaingizwi kwenye takwimu, hali inayoonesha huenda vifo hivyo ni
zaidi ya takwimu halisi zilizopo.
Alisema kuna kila sababu kwa mamlaka husika kwa
kushirikiana na jamii kulivalia njuga suala hilo ili kuhakikisha vifo
vya mama na mtoto vinakoma. Aidha alisema licha ya uhimizaji wa
wajawazito kuhudhuria klini bado idadi kubwa hasa vijijini
wanajifungulia nyumbani kutokana na umbali mrefu wa sehemu zinapotolewa
huduma za afya.
"...Sisi tumefanya utafiti katika Mkoa wa Rukwa
kuangalia hali ya upatikanaji huduma za afya kwa wajawazito. Yapo maeneo
mama aliyefikia hatua ya kujifungua (mwenye uchungu) hutakiwa atembee
kilomita 94.5 ndiyo anakutana na kituo cha afya, sasa mtu aliye na hali
kama hiyo hawezi kutembea umbali mkubwa kiasi hicho hivyo hulazimika
kujifungua nyumbani," alisema Lyamuya.
Aidha aliongeza kuwa taasisi ya Utepe Mweupe (The
White Ribbon Alliance) kwa sasa inaendesha kampeni ya miaka mitatu ya
"Wajibika Mama Aishi" ikiwa ni moja ya hatua ya kushawishi kila mmoja
kuwajibika kuhakikisha anakabiliana na vifo vya akinamama na watoto
vinavyotokea hasa wakati wa kujifungua.
Hata hivyo aliwataka wanahabari kuhakikisha
wanatumia nafasi zao kutoa mchango wa kuvishavishi vyombo husika na
wanajamii kwa ujumla kupambana na vifo vya akinamama na mtoto.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment