BARAZA la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (BAWACHA),
limewataka Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi, Mathias Chikawe,Waziri wa
Jinsia Wanawake na Wanawake, Sophia Simba na Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini (IGP) Ernest Mangu, kuacha kufanya siasa huku wimbi la kutekwa na
kupotea kwa watoto likiwa linaendelea kwa kasi.
Mbali na kuwataka viongozi hao kuacha mbwembe katika kushughulikia
utekwaji wa watoto, pia baraza hilo limemtaka Mangu kutumia nguvu za
askari wake kukabiliana na watekaji na wauaji wa watoto, kama
alivyofanya wakati wa kukabiliana na maandamano ya wapinzani wakati
wakipinga Bunge Maalum la Katiba kuendelea na mchakato wake huku kukiwa
hakuna uhakika wa kufikia muafaka wa kupatikana kwa katiba hiyo.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa BAWACHA Taifa,
Halima Mdee, wakati akielezea madhumuni ya Chama chake kufanya ziara ya
siku 20 mikoani kwa ajili ya kuwazindua wananchi juu ya kuifahamu
katiba iliyopendekezwa kabla ya kufanyia uamuzi wa kuikubali au
kuikataa.
Mdee alisema Jeshi la Polisi lina wajibu wa kulinda raia na mali zao na
kwamba linapokaa kimya hata pale kunapokuwa na taarifa za watu
waliotenda uhalifu kunadhihirisha kuwa wanafurahia matukio hayo.
“Mmesikia mauaji ya hivi karibuni ya mtoto Gloria lakini mapema mwezi wa
tatu mwaka huu mtoto mwingine anayeitwa Joshua alitekwa na kuuawa na
wazazi wake wakasema wazi kuwa wauaji wa mtoto wake wanajulikana na sasa
wanatanua mitaani…katika hali hii kwanini tusiseme waliomuua Gloria
ndio hao hao walioachwa na polisi wakati walipomuua Joshua,” alisema
Mdee.
Aliongeza kuwa kwa upande wa Waziri Chikawe anapaswa kulisimamia jambo
hilo kwa kuwa jeshi hilo lipo chini yake na dhamana ya ulinzi wa raia na
mali zao zinasimamiwa na walio katika wizara yake.
Kuhusu Waziri Simba, alisema wizara yake ina wajibu wa kuhakikisha
mateso ya wanawake na watoto yanatokomezwa kwa kuyapigia kelele na
kuchua hatua.
Mdee alisema linapokuja suala la kushughulikia watoto waathirika wakubwa
ni wanawake ambao wanakabiliwa na matatizo mbali mbali baada ya
serikali kushindwa kusimamia vipaumbele vyao.
“Wanawake wanapata madhila yote haya kwa sababu ya mipango mibovu ya
serikali iliyopo madarakani leo wanatumia muda mrefu kutafuta huduma za
msingi hata kuwaacha watoto wakiwa hawana uangalizi wa kutosha na haya
ndiyo yanayochangia utekwaji na unyanyaswaji wa watoto,” aliongeza Mdee.
Awali Katibu Mkuu wa BAWACHA, Grace Tendega, akielezea madhumuni ya
ziara yao, alisema watafika katika mikoa sita yenye jumla ya majimbo 20.
Alisema wakiwa katika majimbo hayo watawaelewesha wananchi hususan
wanawake umuhimu wa kuijandikisha katika daftari la kudumu la wapiga
kura, daftari la wakaazi pamoja na kuhamasisha juu ya kuwa na mtazamo
sahihi wa Katiba inayopendekezwa kabla hawajaipigia kura.
Pia alieleza madhumuni mengine ya ziara hiyo ni kuwahamasisha wanawake
kuwania nafasi mbali mbali za uongozi kuanzia uchaguzi wa serikali za
mitaa utakaofanyika Desemba mwaka huu.
Chanzo: Tanzania daima
No comments:
Post a Comment