Shirika la
Viwango Tanzania (TBS) ni shirika ambalo lilianzishwa mwaka 1975 chini ya
sheria namba 3, ikarekebishwa na sheria namba 2 ya mwaka 2009. Kazi kubwa ya
shirika hilo ni kuandaa viwango vya bidhaa mbalimbali kama vile chakula,
vinywaji, vifaa vya umeme, ujenzi na bidhaa za ngozi.
Pamoja na
hayo, pia wamekuwa wakiangalia bidhaa za elektroniki na bidhaa nyingine, na
hupima bidhaa hizo kwa kutumia maabara zake za kupima viwango mbalimbali.
Shirika hilo
kwa kushirikiana na Mamlaka ya Chakula na dawa, Polisi, Sumatra na Mamlaka
nyingine za udhibiti wa bidhaa wamekuwa mstari wa mbele katika kupambana na
watu wanaouzia watu bidhaa feki sokoni na kutoa elimu kwa jamii kuepukana na
matumizi ya bidhaa hizo ili kuepukana na athari.
Katika
mahojiano na Ofisa Masoko Mwandamizi wa TBS Daud Mbaga anaeleza kuwa, ili
kuhakikisha ubora wa bidhaa sokoni shirika hilo hutumia njia mbalimbali ikiwa
ni pamoja na kutoa nembo ya ubora kwa bidhaa zinazozalishwa nje ya nchi ambazo
zinakuwa zinakidhi matakwa ya viwango
Pia, hutoa
nembo ya ukaguzi wa bidhaa za nje ndani ya mipaka ya Tanzania mathalani meli
inapokuwa imefika bandarini bidhaa huchukuliwa na kupimwa kuona kama bidhaa
hiyo iko kwenye kiwango sahahi.
Lakini ikiwa
wamegundua bidhaa ambazo wanazikagua haifai kuuzwa katika soko la Tanzania,
hawaruhusu kabisa kuingia nchini na
hatua wanayoichukua ni kuharibu bidhaa hiyo ili kuwa fundisho kwa
wafanyabiashara wengine.
Vile vile,
wamekuwa na utaratibu wa kukagua bidhaa ndani ya nchi inapotoka. Utaratibu huu
ni mpya na ulianzishwa mapema mwaka huu ili tu kuhakikisha kuwa bidhaa
zinazouzwa sokoni ni za ubora unaohitajika.
Mbaga
anaeleza kuwa chini ya utaratibu huo Makampuni matatu ikiwa ni pamoja na SGS,
Inrettech na Bureau Veristers yamepewa dhamana ya kufanya ukaguzi huo.
“Ina maana
kuwa bidhaa kama haifai hukataliwa huko huko katika nchi na kama ikibainika
zina ubora basi hupakiwa na kuletwa katika soko la Tanzania,” anaeleza Mbaga.
Anasema
utaratibu huo mpya umekuja kutokana na changamoto zilizokuwepo siku za nyuma kwenye
mifumo iliyotangulia kwani ilikuwa imeruhusu uwepo wa bidhaa hafifu sokoni.
Mfumo huo
licha ya kuongoza bidhaa katika kiwango kikubwa lakini pia inasaidia kupunguza
msongamano bandarini na pia unamsaidia mfanyabiashara kuokoa muda.
“Mfumo huu
unamuhakikishia mlaji ubora wa bidhaa anayokula na thamani ya pesa zake hivyo
ni matumaini yetu kuwa utaendelea kufanya vizuri, na hivyo kuwawezesha
watanzania kupata bidhaa inayohitajika katika kiwango cha kimataifa,”anasema.
Anasema
uzuri wa mfumo huo ni kwamba hauruhusu bidhaa bandia kupenya katika soko la
Tanzania kwani mwingizaji akija na bidhaa zake lazima aonyeshe vibali vyote
muhimu kwamba shehena anayotaka kuileta Tanzania ni halali.
Si hayo tu
bali wana mfumo mwingine wamekuwa wakiutumia katika kuzifanya bidhaa ziwe na
ubora na mfumo huo ni ule wa kukagua kiwanda na kukipa cheti cha ubora dhidi ya
bidhaa zake. Akitolea mfano wa bidhaa kama vile pikipiki ambazo nyingi hutoka
China, bia ya Heineken ambazo hutoka Uholanzi hupewa cheti za ubora wakiwa
katika viwanda vyao kisha kuruhusiwa kuingizwa nchini.
Pamoja na
kuanzisha mifumo hiyo ya uboreshaji wa bidhaa Mbaga anasema TBS hukabiliwa na
changamoto nyingi na zaidi licha ya juhudi zao bado kuna upenyezo mkubwa wa
bidhaa feki sokoni.
Anasema
Tanzania ni nchi kubwa sana na ina mipaka ambayo siyo rasmi. Mipaka hiyo
imekuwa ikitumika kupitisha bidhaa feki jambo ambalo wananchi wengi wamekuwa
wakiona pengine TBS imeshindwa kufanya kazi vizuri.
Anasema
uelewa wa wananchi kuhusiana na hilo bado pia ni mdogo. Ni kweli kwamba kuna
wengine wanaona bidhaa hizo zikipitishwa lakini hawana ushirikiano wa kutosha
na Polisi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na shirika hilo.
“Tunaonyesha
juhudi kubwa katika kuzuia njia za panya lakini tatizo lipo kwa wananchi kwani
hawana ushirikiano wa kutosha na zaidi kwa wamekuwa wakitoa lawama kwamba
pengine kazi imeshindikana lakini ukweli sivyo,”anasema.
Mbaga
anasema mifumo wa TBS, TFDA, TRA na bandari haijaweza kufanya kazi kwa asilimia
100 kutokana na matatizo kama hayo, lakini anaamini kuwa juhudi bado
zinaendelea kufanyika na kupitia utaratibu mpya waliojiwekea watashiriki
kikamilifu katika mapambano dhidi ya bidhaa feki.
Lakini
tatizo lingine kubwa linaloelezwa kuwa ni changemoto kubwa kwao ni kuongezeka
kwa mahitaji ya bidhaa kwa wananchi zaidi ya uwezo wa kutosheleza mahitaji
hayo. Anasema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakilichukulia kama faida kwao.
Wamekuwa
wakiingiza bidhaa nyingi feki ili kuwaridhisha wananchi na kwasababu wananchi
wengi wamekuwa hawana uelewa kuhusiana na bidhaa hizo wamekuwa wakinunua bila
matatizo na kuonyesha nia ya kuzihitaji zaidi.
“Mahitaji
makubwa ya wananchi hufanya wafanyabiashara kuwa na moyo wa kuendelea kuuza
bidhaa ambazo hazina ubora matokeo yake kunakuwa na mwanya wa uingizaji wa
bidhaa hizo kiholela na wengine ndio hutumia njia za Panya,”anasema.
Kama
wananchi wangekuwa na uelewa kuhusu zipi ni bidhaa feki ili wasinunue na kuamua
kutowaunga mkono wafanyabiashara katika ununuzi wa bidhaa hizo ni wazi hata
wafanyabiashara wasingeweza kuzileta kwa wingi kwani wangeona kuwa ni bidhaa ambazo hazinunuliki.
Kwasababu
hiyo, wapo wananchi wengi tayari wamepata hasara kwasababu wameuziwa bidhaa
zisizokuwa na ubora unaohitajika na wengine wamejikuta wakiuziwa vifaa
mbalimbali ambavyo havifanyi kazi kwa bei rahisi.
Mfano mzuri
ni hivi karibuni kuna baadhi ya wananchi katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na
Manyara waliuziwa vifaa vya umeme jua vinavyojulikana kama ‘Solar panel’ na
kuelezwa kuwa wavichaji kwa masaa 8, na kumbe walovyofanya vile na kuviwasha
ili wavitumie walikuta haviwaki kabisa.
Mkazi
mmojawapo aliyelia kwa kuuziwa kifaa hicho cha umeme jua ni Hilary Nyandoa
kutoka kijiji cha Magadini Simanjiro ambaye alifikisha malalamiko yake katika
Ofisi za Tarea jijini Dar es Salaam kuwa
aliuziwa kifaa hicho na wafanyabishara wanaopitisha bidhaa mtaani (Wamachinga)
kikiwa na anwani zinazodai zinatoka katika kampuni moja ya Dar es Salaam
iliyoko Ubungo Plaza.
Lakini mara
baada ya uchunguzi wa Tarea ikabainika kuwa hakuna kampuni kama hiyo katika
Ofisi za Ubungo Plaza, na walipokuwa wakijaribu kupiga namba za simu ili
kueleza dukuduku lao, zilikuwa zikiita bila kupokelewa.
Kutokana na
matatizo kama hayo, jamii inahitajika kuwa makini pindi inapochagua bidhaa sokoni,
lakini pia kuwa makini dhidi ya wale wafanyabiashara wanaowapitishia mtaani
wakidai wanauza kwa bei ya promosheni kwani kuna hatari ya kuuziwa bidhaa
ambazo hazifanyi kazi.
Hata hivyo,
Mbaga anasema wafanyabiashara wengi wamekuwa wakiuza bidhaa zisizo na ubora kwa
kuangalia kipato cha wananchi jambo ambalo halitakiwi kwani kufanya hivyo ni
kuwaonea kwasababu vifaa wanavyouziwa haviwezi kumudu kwa muda mrefu.
Anasisitiza
umuhimu wa jamii kuamka na kuwa makini pindi wanapochagua bidhaa kwani
wanahitajika kuangalia zile ambazo zina nembo ya TBS kwani zinakuwa
zimeruhusiwa kuuzwa sokoni.
No comments:
Post a Comment