TAASISI ya HakiElimu nchini imeishauri Serikali pamoja na Chama Cha
Walimu Tanzania (CWT) kufikia makubaliano haraka iwezekanavyo, ili
kumaliza mgomo uliopo kwani waathirika zaidi na mgomo huo si wao bali ni
ni wanafunzi.
Kauli hiyo imetolewa leo jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi
Mtendaji wa HakiElimu, Bi. Elizabeth Missokia alipokuwa akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na mgomo wa walimu
unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.
Alisema kila mwanafunzi ana haki ya kujifunza na kuelimishwa, kitu
ambacho hawakipati kwa sasa kutokana na mgomo wa walimu wanaoshinikiza
Serikali iwaongeze mishahara pamoja na kuwaboreshea mazingira ya kazi
zao.
Mkurugenzi huyo alisema kauli ya Serikali kudai haina uwezo wa
kuboresha maslahi na mazingira ya kazi ya watumishi wake haileti unafuu
wa maisha kwa watumishi wa umma hivyo kushauri iangalie namna ya
kufanya kumaliza mgogoro huo.
“HakiElimu inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu
endapo tu itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi
ya walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu
na kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu
walio hoi,” alisema Missokia.
Aidha amewataka walimu kuhakikisha wanadai haki zao huku
wakiendelea kuwajibika kwa kufundisha na kuendeleza elimu yetu, kwani
wanamgogoro na Serikali na wala si wanafunzi na jamii kwa ujumla.
“HakiElimu inawakumbusha walimu kuwajibika. Wadai haki zao, huku
wakitimiza wajibu wao wa kufundisha na kuendeleza elimu yetu. Wafundishe
kwa bidii bila kinyongo, kwa kuwa wasipowajibika watakuwa wanawaumiza
wanafunzi na jamii kwa ujumla. Mgogoro uliopo ni baina yao na Serikali,
na si wanafunzi,” alisema Mkurugenzi huyo Mtendaji.
“Viongozi wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa. Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli,” alisema.
Pamoja na hayo ameliomba Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
kuingilia kati mgogoro huo na kutenga muda kujadili suala hilo kwa kina
ikiwa ni pamoja na kuishauri serikali, hasa kuhusu tahadhari za kuchukua
ili tatizo kama hili lisitokee tena.
“Bunge lina wajibu wa kuishauri na kuisimamia Serikali kuhusu sera,
utendaji na usimamizi wa elimu nchini. Inasikitisha kwamba Bunge
linakwepa kujadili tatizo hili kwa maelezo kwamba liko mahakamani.
Tunaamini kwamba mahakama italiangalia suala hili na kutenda haki,
lakini wajibu wa Bunge uko pale pale…” alisema Bi. Missokia.
Amekiri kwamba ni kweli gharama za maisha zinazidi kupanda, huku
mfumuko wa bei nao unaendelea kuwaumiza watumishi kila siku, hivyo
kuishauri Serikali kutafuta vyanzo mbadala vya mapato ili kuweza
kuwaboreshea mapato watumishi wake.
“Serikali ijijengee utaratibu wa kuboresha mazingira ya watumishi
wake, na si kusubiri kwenda mahakamani kuzuia watumishi kugoma.
Watumishi wa umma watafanya kazi kwa ari endapo tu wameridhika na
mazingira ya kazi na maslahi yao; na si kwa kutumia uamuzi wa mahakama
peke yake.”
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
Habari hii imeandaliwa na Mtandao wa Thehabari.com (www.thehabari.com)
No comments:
Post a Comment