JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
taarifa kwa umma, kuhusu tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye
vyombo mbali mbali vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani
Karagwe mkoa wa Kagera.
Mnamo tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na
Ustawi Wa Jamii ilipokea taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya
kuwepo kwa mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola,
katika hospitali ya Wilaya ya Nyakahanga. Aidha,taarifa hiyo ilibainisha kuwa
mgonjwa huyo alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka (6|) kutoka katika
kijiji cha Nyakatundu wilayani Karagwe. Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa
kali, kulegea, kutokwa damu puani, kutapika damu, na kukojoa damu.Maelezo
kutoka kwa mama mzazi zilieleza kuwa mtoto huyu alianza kuugua kuanzia tarehe
30 Agosti 2012, ambapo alipatiwa dawa ya Septrin baada ya hospitali binafsi
kuonyesha kuwa ana ugonjwa wa“Typhoid”.
Uchunguzi wa awali katika hospitali ya Nyakahanga
ulionyesha kuwa mtoto huyu alikuwa anasumbuliwa na uambukizo kwenye haja ndogo
(Urinary Tract Infection).Vile vile alifanyiwa uchunguzi wa kimaabara na Vipimo
vya malaria, Hepatitis na Typhoid havikuonyesha kuwepo kwa magonjwa haya.
Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka mgonjwa na mama
yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa ajili ya uangalizi
zaidi.
Aidha mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za wataalamu
kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na timu ya mkoa wa
Kagera imeweza kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina pamoja na kuchukua sampuli
za damu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika maabara ya Taifa ya uchunguzi wa
magonjwa na Maabara za nje ya nchi, ili kubaini kama ameathirika na ugonjwa wa
Ebola. Timu hiyo ya wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya mgonjwa huyu kwa sasa
imeimarika ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na kukojoa damu kumekoma
pia, uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha kuwa hana dalili zozote
za ugonjwa wa Ebola.Vile vile hakuna taarifa ya mtu mwingine yeyote kwenye
familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au cha jirani kuwa na dalili za
ugonjwa huo.
Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;
• Imepeleka timu ya wataalamu mbali mbali kutoka
Wizarani na mkoa kwa lengo la kwenda kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu kuwepo
kwa ugonjwa huo.
• Imetoa elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea
ugonjwa wa Ebola pamoja na dalili za ugonjwa huu, kwa wananchi na watumishi wa
afya katika hospitali ya Nyakahanga
• Kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya
Nyakahanga pamoja na maeneo ya mipakani
• Kutoa matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza
sauti na kupitia radioni (Radio Karagwe) kuhusu ugonjwa huu. Aidha, vipeperushi
pia vimetolewa.
Hitimisho
Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa
hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa
nchini.Aidha, Wizara ya Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu
iwapo utatokea hapa nchini.
Kwa sasa timu za wataalum zipo katika mikoa ya
Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha, kutoa elimu juu ya ugonjwa
huu kwa wataalamu na kwa wananchi na vilevile kufuatilia ugonjwa huu sehemu za
mipakani.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa
taarifa haraka kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za afya, mara wanapoona
dalili za ugonjwa huu.
Imetolewa na: kitengo cha Mawasiliano Wizara ya
Afya na Ustawi wa Jamii
Tarehe 6 Agosti, 2012
No comments:
Post a Comment