TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday, 19 June 2013

Mara waitikia wito wa Siku ya Mchangiaji Damu Duniani, Benki ya Damu Kanda ya Ziwa yafurika michango yao!


Na Craig Fela Musoma, Mara
Kuokoa maisha ya maelfu ya mama zetu na watoto wetu wachanga Tanzania inawezekana! Kwa pamoja tunaweza kabisa kubuni mbinu mpya za kufanikisha yale ambayo awali tuliyaona kama hayawezekaniki… Hivi sasa ninapoandika makala hii, benki ya damu ya Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) Kanda ya Ziwa imefurika, huku maandalizi ya kuongeza uwezo wa taasisi hii kupokea damu nyingi kwa mpigo yakiendelea, na hii ni kutokana na mwitikio mkubwa wa wakazi wa wilaya zote za mkoa wa Mara kujitokeza kwa makundi makubwa kujitolea damu kwa hiari! 


Mama Ye!ni kampeni inayohimiza wanajamii kuchukua hatua kuokoa maisha ya maelfu ya mama zetu na watoto wachanga wa Tanzania. Hii ni kampeni inayoongeza msisitizo wa Kampeni ya kimataifa ya Kupunguza Vifo vitokanavyo na Uzazi Barani Afrika (CARMMA) iliyozinduliwa Novemba 2011 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Jakaya Kikwete. Kwa pamoja tumeazimia kuona kuwa ‘Mama asife wakati analeta uhai.’
 
Kuna ambao watajiuliza kuna uhusiano gani kati ya uhai wa akina mama na uchangiaji damu, na ni kwa niniMama Ye!imeungana na NBTS na mamlaka za Mkoa wa Mara kwa ajili ya maadhimisho ya mwaka huu ya Siku ya Mchangia Damu Duniani? Kwa mtazamo wangu, jibu ni rahisi. 

Takwimu za Tanzania kwa kutumia makadirio ya Shirika la Afya Duniani zinakadiria kuwa 80% ya damu inayokusanywa hutumika kwa watoto pamoja na akina mama wenye matatizo yatokanayo na ujauzito. Inakadiriwa kuwa kutokwa na damu nyingi baada ya kujifungua  ndicho chanzo kikuu cha vifo vya wanawake wajawazito, na husababisha kifo kimoja kati ya kila vifo vitatu hadi vitano vya akina mama wajawazito nchini Tanzania. 

Aidha kuna uhaba mkubwa wa damu kwenye hospitali zetu—huku ikikadiriwa kuwa ni theluthi moja tu ya chupa 450,000 za damu zinazohitajika nchini kila mwaka ndizo zinazokusanywa. Ni wazi kabisa kuwa wapo akina mama wetu wanaovuja damu nyingi baada ya kujifungua wanaofariki kutokana na uhaba wa damu kwenye vituo vya tiba. Iwapo watavuja damu nyingi baada ya kujifungua, wanawake wanaweza kuhitaji kuongezewa damu ili kuwaokoa. Kama damu itakuwepo katika vituo vya tiba, basi akina mama hao wataokolewa. Vile vile, kama akina mama wengi wataokolewa basi watoto wachanga wengi nao wataokolewa, na hii ni kutokana na uhusiano wa karibu kati ya uhai wa watoto wachanga na ule wa mama zao.


Na la muhimu zaidi kwaMama Ye!– kuchangia damu ni kitendo kinachobeba maana nzito na cha kuonekana, ambacho kinaweza kufanywa na mtu yeyote yule ili kushiriki kuokoa maisha ya mama zetu. Ni maamuzi yanayotokana na dhamira ya mtu kuchangia damu. 

Na kama dhamira hiyo ya kuchangia damu inatokana na nia ya kuokoa maisha ya akina mama, basi inaweza kuwa chachu kwa mtu huyo huyo kuchukua hatua nyingine ambazo zinaweza kutendwa na kila mtu ili kuwaokoa akina mama na watoto wetu wachanga. Kwa mfano, kuwahimiza akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki japo mara nne; kuwawezesha akina mama kujifungulia katika vituo vya tiba ambapo kuna mhudumu mwenye ujuzi kwa kuwaandalia usafiri au kuwaangalia watoto wao pale nyumbani; na kuwafuatilia viongozi katika jamii na kujua ni hatua gani zinachukuliwa kuhakikisha uwepo wa huduma na ubora wa huduma hizo kwa akina mama na watoto wachanga.
  

Mara Oyee!!Mmetoa ujumbe wa kishindo katika wiki mbili zilizopita, kutoa matumaini kwa uhai wa mama zetu na watoto wachanga!! NBTS imethibitisha kuwa ukusanyaji wa damu katika sherehe za kitaifa kama hizi umevuka kiwango kilichokuwa kimezoeleka!! Zaidi ya watu 1,250 wamechangia damu katika sherehe za wilayani Bunda, Butiama, Serengeti, Tarime na Rorya wiki iliyopita. Wiki hii wakazi wa Manispaa ya Musoma nao pia wamejitokeza kwa makundi makubwa—Jumla ya wakazi 500 wamechangia damu katika siku mbili tu zilizopita, na wakati huo huo wakitoa ahadi zao na wito kwa wanajamii wengine kuchukua hatua mbalimbali kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga mkoani Mara. Na kwa hakika tangu maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Mchangiaji Damu Dunani ya mwaka huu yaanze katikati ya Aprili, zaidi ya chupa 5,000 za damu zimekusanywa mkoani Mara. Tembelea ukurasa wetu wafacebookkuona picha za jinsi Mkoa wa Mara ulivyoweka historia mwaka huu katika shamra shamra za Siku ya Mchangiaji Damu Duniani, nchini Tanzania!!



La muhimu zaidi ni kuwa kuna somo kubwa limetolewa na wakazi wa Mara: Hakuna sababu kwa hospitali zetu kukosa huduma ya damu ili kuokoa maisha. Na hili ni hitimisho nililolisikia mimi mwenyewe likirudiwa rudiwa na viongozi wa Mkoa wa Mara, viongozi wa NBTS, na pia Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii ambaye yuko Mjini Musoma kama mgeni rasmi wa maadhimisho haya. Vile vile, NBTS wameahidi kuweka benki ya damu kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mara badala ya damu inayokusanywa kupelekwa Jijini Mwanza kwenye benki ya kanda, takribani umbali wa kilometa 250. Aidha uongozi wa Mkoa wa Mara umedhamiria kuhakikisha kuwa mwitikio huu wa uchangiaji damu unakuwa endelevu mkoani kote.

Kile kilichoonekana kama hakiwezekani sasa kimewezekana. Wakazi wa Mara wameonyesha kuwa damu ya kutosha inaweza kukusanywa kutoka kwa wanajamii nchini kote. Akina mama wote na watoto wachanga ni lazima wahakikishiwe upatikanaji wa zawadi adhimu ya maisha. Tuichukulie hatua ya wakazi wa Mara kama chachu na changamoto ya kutuhamasisha sisi wote – wanajamii wa Tanzania, wadau wa masuala ya uhai wa akina mama na watoto wachanga, na watoa maamuzi na viongozi wa ngazi zote, kusimama na kutimiza wajibu wao binafsi kwa kuchukua hatua za kuhakikisha wanalinda uhai wa maelfu ya akinamama na watoto wetu wachanga ambao, kwa masikitiko makubwa, wengi hupoteza maisha kwa sababu zinazozuilika, tena  wanakufa katika kipindi kilichotakiwa kushangiliwa, kipindi cha kuleta uhai mpya katika jamii zetu na taifa kwa ujumla. 
(Mwisho)

No comments:

Post a Comment