TANGAZA NASI LEO 0712709630,0756631636 BARUA PEPE gmkojera@gmail.com

Wednesday, 19 June 2013

Wanafunzi kidato cha Sita wabebeshwa mzigo wa ualimu wa Sayansi Rombo

Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Nduweni Sekondari, Venance Mramba.

Baadhi ya wanafunzi Sekondari ya Nduweni wakiwa darasani 
KITENDO cha upungufu wa walimu wa sayansi nchini hasa katika shule za sekondari zinazomilikiwa na serikali kimezidi kuibua changamoto maeneo mbalimbali nchi. Shule ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto hiyo kwa kiasi kikubwa ni sekondari za kata ambazo uwingi wake umechochea zaidi changamoto hiyo.

Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro ni miongoni mwa maeneo ambayo yanakabiliwa na changamoto hiyo ya uhaba wa walimu wa sayansi kama ilivyo kwa mikoa tofauti ya Tanzania. Hata hivyo walimu wakuu wa shule zenye changamoto wamebuni mbinu mbadala kukabiliana na hali hiyo.

Zoezi la uhamasishaji ujenzi wa shule za sekondari za kata limekuwa na mafanikio kiasi kikubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rombo, kwani hadi sasa wilaya hiyo imefikisha jumla ya sekondari 41 zilizo chini ya serikali ikiwa ni jitihada za wananchi kwa kushirikiana na viongozi wao.

Mwandishi wa makala haya amefanikiwa kutembelea shule sita tofauti za sekondari za kata wilayani Rombo na kufanya mazungumzo na walimu wakuu, walimu na wananfuzi ambao wanatoa picha halisi ya uhaba wa walimu wa sayansi. Miongoni mwa shule zilizotembelewa ni pamoja na Sekondari za Nduweni, Tanya, Urauri, Holili na Ngaleku.

Victus Kiwango ni Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Tanya iliyopo wilayani Rombo. Mwalimu huyu anasema uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi ni moja ya tatizo zinaloikabili shule hiyo. Kiwango anasema shule yake haina kabisa walimu wa masomo ya Kemia, Fizikia na Baiolojia hivyo hulazimika kutumia walimu wa kukodi kwa vipindi tofauti.

Anasema shule hiyo hutegemea wanafunzi kadhaa waliomaliza kidato cha sita ambao huwakodi na kufundisha masomo hayo pale wanapopatikana ili wanafunzi waweze kupata chochote na hatimaye baadaye kufanya mitihani ya sayansi. "...Hapa shuleni kwetu (Tanya Sekondari) masomo ya sanyansi ndio tatizo, mfano hatuna kabisa walimu wa masomo ya Kemia, Fizikia pamoja na Baiolojia hivyo huwa tunakodisha na shule kuwalipa," anasema Kiwango. 

Hata hivyo kero na kilio cha uhaba wa walimu kinasikika tena katika sekondari ya duweni wilayani humo. Mwalimu Mkuu Msaidizi wa sekondari hiyo, Venance Mramba anasema tatizo la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi linaiathiri shule hiyo kitaaluma. Anasema shule miaka yote shule hiyo imekua ikianzia ufaulu wa daraja la pili.

Anatolea mfano katika matokeo ya mwisho ya kidato cha nne (juzi), ilifanikiwa kufaulisha mwanafunzi mmoja kwa daraja la pili na wanne kwa daraja la tatu. Anaongeza kuwa katika matokeo hayo wanafunzi 25 walipata daraja la nne na wanafunzi 70 wakiambulia sifuri, kati ya idadi ya wanafunzi 102 waliofanya mtihani huo wa mwisho wa taifa.

"Tatizo kubwa la kufaulu ni uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi ikiwemo hesabu na mengineyo, uhaba wa vifaa vya ufundishaji na kujifunzia pamoja na upungufu wa vitatu vya masomo yote," anasema mwalimu Mramba katika mahojiano na mwandishi wa makala haya.

Anaongeza ili kukabiliana na upungufu wa walimu wa sayansi shule hiyo huajiri kwa muda wanafunzi waliohitimu kidato cha sita na kuwasaidia kuwafundisha wanafunzi masomo hayo. Hata hivyo anasema bado kuna changamoto kubwa katika kuwatumia walimu hao wahitimu wa kidato cha sita, kwani hawana mbinu za kufundishia jambo ambalo bado ni kikwazo katika shule hiyo.

Benson Samizi ni Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Sekondari ya Holili iliyopo katika Wilaya ya Rombo. Mwalimu huyu anasema japokuwa hali ya kitaaluma shuleni hapo si mbaya sana lakini shule inakabiliwa na upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi kama ilivyo katika shule nyingine wilayani hapo.

Mwalimu Samizi anasema shule hiyo haina kabisa walimu wa masomo ya Fizikia na Hesabu na hulazimika kukodi walimu wa muda ili kuwaandaa wanafunzi. Shule hii haina maabara japokuwa ina vitabu vya kutosha vya masomo ya sayansi. Akizungumzia ufaulu wa kidato cha nne kwa mwaka 2011, anasema shule ilipata mwanafunzi mmoja aliyekuwa na daraja la kwanza na wengine wawili waliopata daraja la pili, huku wanafunzi watatu wakipata daraja la tatu.

Samizi anaendelea kubainisha kuwa katika matokeo hayo jumla ya wanafunzi 55 walipata daraja la nne na 18 kuambulia patupu (sifuri) kati ya watahiniwa 80 waliofanya mtihani wa mwisho wa taifa kuhitimu kidato cha nne mwaka 2011.  

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Sekondari ya Urauli, iliyopo Tarakea wilayani Rombo, Sim Silayo anasema mbali na biashara zinazofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya eneo hilo kuathiri taaluma kimaudhurio, upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi ni kero nyingine shuleni hapo.

Mwalimu Silayo anaeleza kuwa shule hiyo haina kabisa walimu wa masomo ya Fizikia, Kemia na Baiolojia; hivyo uongozi wa shule kulazimika kukodi walimu wa muda wa masomo ya sayansi wakiwemo baadhi ya wanafunzi waliohitimu kidato cha sita wanaosubiri kuendelea na masomo yao ya juu. Aidha anaongeza kuwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2007, yenye jumla ya wanafunzi 464 haina maabara wala vitabu vya kutosha licha ya kukabiliwa na changamoto zingine mbalimbali.

Yehova Mashalo ni mwanafunzi wa kidato cha nne Shule ya Sekondari Tanya anasema wapo wanafunzi wengi ambao hukata tamaa kuchukua masomo ya sayansi tangu wakiwa madarasa ya chini kutokana na kukosekana kwa walimu wa masomo hayo. Kwa upande wake Joice Kimaro mwanafunzi wa kidato cha tatu shule ya Sekondari Tanya anaongeza kuwa kutojitosheleza kwa walimu wa sayansi shule za sekondari hasa za kata inakatisha tamaa wanafunzi kupenda masomo hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rombo, Judethadeus Mboya anasema halmashauri yake inajitahidi kuongeza idadi ya walimu kila mwaka ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa walimu. Anasema kwa uwiano wa kawaida Wilaya ya Rombo haina upungufu mkubwa wa walimu, lakini una upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi.

Anasema kwa sasa wilaya ina jumla ya walimu 800, huku kwa mwaka huu pekee ikiwa imeajiri walimu 134 wakiwemo wa masomo ya sayansi. "...Kwa suala la upungufu wa walimu Wilaya ya Rombo ni tofauti na maeneo mengine, hapa kuna upungufu wa walimu wa masomo; kama Hesabu, Fizikia, Kemia na Baiolojia nitatizo," anasema Mkurugenzi Mboya.

Hata hivyo anakiri kutokana na suala la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi zipo shule ambazo zimelazimika kutumia walimu wa kukodi na kutumia wanafunzi waliomaliza kidato cha sita ili shule iweze kwenda mbele. Anasema kuwa lengo kubwa la halmashauri hiyo ni kuhakikisha inatatua changamoto hiyo kila inapotokea nafasi.    

Kwa upande wake Katibu wa CWT Wilaya ya Rombo, Erasmo Mwingira anasema vijana wa kidato cha sita ambao hutumiwa na baadhi ya shule kuokoa jahazi la masomo ya sayansi wamekuwa hawafundishi zaidi ya kuwakaririsha wanafunzi kujibu mitihani jambo ambalo anatahadharisha huenda likawa na madhara makubwa kwa elimu yetu Tanzania. 

"Kujua kusoma na kuandika si kigezo cha kumfundisha mtu...vijana hawa wa kidato cha sita hawana mbinu za ufundishaji, wanachokifanya ni kuwakaririsha wanafunzi," anasema Mwingira. Pamoja na hayo mdau huyu wa elimu anaishauri serikali kutojitoa katika jukumu la kuendesha shule za kata kwa kuwaachia wazazi kwani shule hizo ziko katika hali mbaya na zinahitaji kuongezewa fedha za uendeshaji.

No comments:

Post a Comment