Na Thehabari.com, Kishapu
WASWAHILI
wanasema 'maji ni uhai' na maisha bila maji ni kadhia. Kimsingi
mwanadamu anahitaji maji safi na salama katika kuendesha maisha yake ya
kila siku. Na kukosekana kwa huduma ya maji safi na salama eneo fulani
huchangia kiwango fulani cha ugumu wa maisha kwenye familia.
Hali hii ndiyo inayowakumba wakazi wa baadhi ya
vijiji vya Kata ya Kishapu, Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga. Tabu ya
maji katika vijiji kama Lubaga, Isoso, Mwanuru pamoja na Kishapu
yenyewe ni msamiati wa kawaida. Vijiji hivi hupata hauweni katika msimu
wa masika pekee ambapo maji hutiririka hata kwenye mito ya msimu
(masika).
Lakini mbali na familia kutaabika kusaka maji umbali
mrefu kwa ajili ya matumizi ya kila siku, lipo kundi ambalo huathirika
zaidi na kero za maji kwa kuwa kundi hilo ndilo linalotegemewa kutafuta
maji katika familia kwa matumizi anua. Kundi hilo ni wanawake na watoto
wakiwemo wanafunzi.
Makundi haya ndiyo yenye majukumu ya kutafuta maji
kwa matumizi ya nyumbani (kwenye familia) wakati wote kulingana na mfumo
wa kifamilia na tamaduni za wakazi wa maeneo haya. Kadri ya msimu wa
ukame katika vijiji hivyo unavyozidi kushamiri ndivyo umbali wa
kuyafuata maji kwa matumizi uendelea kuongezeka.
Kwa hali hii akina mama na wanafunzi hutembea kati
ya kilimita tano hadi 10 kufuatilia maji kwa matumizi ya familia,
kulingana na umbali wa kijiji chao kwenda kwenye chanzo kikuu (ambacho
hata hivyo si cha uhakika) cha maji yaani Mto Tungu. Chanzo hiki cha
maji nacho hukauka kipindi cha kiangazi na hali kuwa ngumu zaidi.
Enock Manyenye Shimba ni Ofisa Mtendaji wa Kijiji
cha Lubaga, anasema huduma ya maji wanayotegemea licha ya kupatikana
umbali mrefu haitosherezi kwa matumizi. Anasema Kijiji hicho hutegemea
maji ya Mto Tungu ambao upo umbali wa kati ya kilimeta tano hadi kumi.
"Kijiji chetu ni Kikubwa wapo baadhi ya wanakijiji hulazimika kutembea
hadi kilimeta 10 kutafuta huduma hii...licha ya kuwa haitoshelezi kwa
matumizi," anasema Shimba.
Anaongeza kuwa kadri ya msimu wa kiangazi
unapochanganya maji katika Mto Tungu nayo huadimika hivyo wananchi
kutegemea kuchimba visima vya muda ndani ya mto huo ili kupata masalia
ya maji ardhini chini ya mto huo. "Hali hii huwa sio kazi nyepesi maana
wananchi huchimba na kufukia visima hivi kila maji yanapoisha kwenye
eneo la kisima...kwa sababu visima hivi huwa vifupi unakuta kikichimbwa
kisima kinaweza kutumia muda mfupi na maji kukauka eneo hilo kisha
tunachimba eneo lingine," anasema Shimba.
Shimba anasema kundi la wanawake na wanafunzi ndio
watafutaji maji wakubwa katika familia nyingi za Kijiji cha Lubaga na
maeneo ya jirani na kijiji hicho. Anaendelea kusema kuwa hata visima
ambavyo hutumika hutoa maji kidogo kidogo jambo ambalo husababisha uwepo
wa foleni kwa wanavijiji maeneo ya visimani.
Kiongozi huyo wa kijiji cha Lubaga anasema mwaka
2010 wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu kijiji chao kilipewa ahadi ya
kuchimbiwa visima virefu vya maji na Mbunge wa Jimbo la Kishapu,
Seleiman Nchambi ahadi ambayo anasema hadi leo wanaifuatilia lakini bado
haijatekelezwa. "Ahadi hii nimeikuta hata katika nyaraka za ofisi ya
kijiji lakini bado haijatekelezwa," anasema Shimba akizungumza na
mwandishi wa makala haya kijijini hapo.
Hata hivyo kwa akinamama ambao umri umeenda zaidi
kilio cha maji huwa maradufu. Ester Bundera (60) ni mkazi wa Kijiji cha
Isoso, anasema katika kijiji hicho shida ya maji ni kubwa hasa miezi ya
kiangazi. Anasema wao hulazimika kuyafuata maji hadi mji mdogo wa Mhunze
ulipo Mto Tungu umbali ambao ni takribani kilometa 10 kwenda tu.
"Hapa kijijini kwetu upo mto mdogo unaojulikana kama
Nkonze ambao hutoa maji msimu wa masika tu tena kwa shida...maji haya
huyapata kwa kuchimba visima vidogo vidogo mtoni kutokana na kutoka
kidogo kidogo huwa ni ya kugombea, lakini kuanzia mwezi wa saba mto huu
visima vyake hukauka hivyo kulazimika kwenda Mto Tungu," anasema.
Bi. Anastazia Christopher ni Mwenyekiti wa Kitongoji
cha Karume kilichopo Kijijini Isoso, akielezea shida ya maji ambayo
wanakijiji hicho huyapata katika Mto Nkonze anasema familia zisizo weza
kuvumilia foleni na vurugu za kuchota maji yanayotoka taratibu visimani
hulazimika kwenda mtoni usiku muda ambao wakazi wengi huwa wamepungua
jambo ambalo ni hatari kiusalama.
"Wanawake ndio wachotaji wa maji wakubwa pamoja na
watoto wao hulazimika kwenda vizimani majira ya saa mbili na saa tatu
usiku muda ambao panakuwa pametulia na kuanza kuchota maji...unajua huku
kwetu wanyama kama fisi ndio ambao hututishia hivyo unaweza kuomba
vijana wakusindikize kisimaji majira kama hayo," anasema Bi.
Christopher.
Aidha anasema matumaini ya kupata huduma ya maji
safi na salama kijijini hapo sasa yanazidi kuyeyuka, kwani ulikuwepo
mradi unaodaiwa kufadhiliwa na UNDP ambao ulisambaza mabomba hadi
kijijini hapo, lakini umekwama kwa zaidi ya miaka 10 tangu uanze bila
kufanya kazi. Kwa sasa mabomba yaliokuwa yametandazwa yanang'olewa na
Serikali na kupelekwa maeneo mengine kitendo ambacho anasema kinazidi
kuwakatisha tamaa. Anasema kijiji hicho pia ni miongoni mwa vijiji
vilivyoahidiwa kuletewa maji na Mbunge Nchambi ahadi ambayo bado
ijatekelezwa.
Hata hivyo kilio cha maji hutofautiana kutoka kijiji
kimoja hadi kingine kutokana na umbali wa kijiji husika na chanzo cha
maji wanachokitegemea. Kwa msingi huo hali ya huduma ya maji ni mbaya
zaidi katika Kijiji cha Kishapu, ambacho wananchi hutegemea maji ya
mabwawa ya mvua ambayo si safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Kipindi cha kiangazi ukame unapokausha mabwawa wanakijiji hulazimika
kusafiri hadi eneo la Mto Tungu kupata huduma ya maji. Umbali kutoka
katika kijiji hicho hadi mtoni Tungu ni takribani ya zaidi ya kilometa
30 jambo ambalo ni kero zaidi kwa wanakijiji. Na wanaoshindwa kufuata
maji ya bure katika mto Tungu hulazimika kununua kwa wachuuzi wa maji
ambao huyafuata machimboni Mwadui.
Bi. Khadija Said ni mmoja wa wakazi wa Kishapu,
anasema kero ya huduma ya maji eneo lao ni zaidi. Wananchi wakati
mwingine hulazimika kutumia maji ya madibwi ambayo si safi na salama
kutokana na hali ngumu. Vilio vya maji katika vijiji mbalimbali vya Kata
ya Kishapu havipo kwa wazazi tu. Wanafunzi nao baada ya kurudi shuleni
jioni hulazimika kuanza shughuli ya kusaka maji kwa ajili ya matumizi.
Unapopita maeneo ya Mto Tungu nyakati za jioni
utakutana na baadhi ya wanafunzi ambao ama wanakuwa wanachota maji au
kufua sare zao za shule eneo la mto huo. Kundi hili hujulikana kirahisi
kwa kuwa huwa wamevaa nusu sare za shule, yaani kwa wanafunzi wa kiume
baadhi huwa wamevaa suruali za shule na shati la nyumbani, huku wa kike
wakiwa na sketi za shuleni na juu vazi la nyumbani.
Biashara ya maji kwa baadhi ya vijiji ni kubwa na
inafanywa na wanaume kwa kutumia matoroli. Wachuuzi hawa wa maji hutumia
toroli lenye uwezo wa kubeba madumu manne ambayo kila dumu linauwezo wa
kuchukua lita 20. Wachuuzi hawa huuza maji yao kwa madumu manne kwa
pamoja, yaani shilingi 1,000 kwa madumu manne. Lakini licha ya kundi
hili kuwa mahiri kwa uchotaji maji ya biashara si wanaotoa msaada wa
maji katika familia zao. Jukumu hilo lipo kwa watoto na akina mama kwa
matumizi ya nyumbani.
Wanyama wanaofungwa na binadamu kama ng'ombe, mbuzi
na kondoo nao ukubwa na ukame huu. Wanyama hawa hulazimika kunywa maji
kwenye chanzo kimoja na binadamu (Mto Tungu) kutokana na shida ya maji.
Kutokana na usimamizi mbovu wa vyanzo vya maji Mto Tungu pia hutumika
vibaya kwa kile baadhi ya wananchi kuingia ndani ya mto na kufanya usafi
kama kufua nguo ndani ya mto.
Maxmilian Lugembe ni Ofisa Mtendaji wa Kata ya
Kishapu. Katika mazungumzo na mwandishi wa makala haya anakiri uwepo wa
shida ya maji kwa kata nzima ya Kishapu na maeneo mengine yanayoizunguka
kata hiyo. Hata hivyo anasema hali hiyo inasababishwa na jiografia ya
eneo hilo. Anasema maeneo mengi ya vijiji vya kata hiyo ni vigumu hata
hupatikanaji maji ya uchimbaji visima virefu kwa matumizi ya kawaida.
"Yapo maeneo ambayo tumejaribu kuchimba visima
virefu lakini hupati maji...ukiangalia visima vinavyochimbwa ni vile
vinavyochimbwa kwenye mto baada ya maji yanayotiririka kukauka mtoni,
hapo ndio wananchi wanapata maji. Yapo maeneo mengine tumejaribu lakini
hupati maji kabisa, eneo hili ni tatizo," anasema Ofisa huyo wa
Serikali.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Kishapu, George
Kessy anaungana na kauli ya mtendaji wake. "Ni kweli suala la maji ni
Tatizo kwa wilaya nzima ya Kishapu, tena ni kubwa sana...hivyo wapo
sahihi wananchi wanapolalamikia suala hilo. Hakuna chanzo cha maji cha
uhakika eneo hili," anasema Kessy katika mazungumzo na mwandishi wa
makala haya.
Hata hivyo anasema juhudi zinafanywa kuhakikisha
wanapata maji ya uhakika eneo hilo. "Lengo la halmashauri ni kuhakikisha
eneo letu linapata maji kutoka kwenye chanzo cha maji cha uhakika...na
mchakato umesha anza, kuna mpango wa kuleta maji kutoka Ziwa Victoria na
hili lipo kwenye mchakato," anasema mkurugenzi huyo.
Kwa upande wake Mbunge Nchambi akizungumzia ahadi za
maji alizotoa wakati wa kampeni na utekelezaji wake anasema hali ni
nzuri kiutekelezaji ukilinganisha na hali ilivyokuwa ahapo awali.
"Niliahidi maji jimbo zima la Kishapu yaani jumla ya vijiji 114, wakati
naingia madarakani nimekuta hali ni mbaya ya huduma za maji...lakini
hadi sasa tunapozungumza zaidi ya vijiji 30 vinapata maji safi na salama
huku jitihada zingine zinaendelea," anasema Nchambi.
Anabainisha kuwa ameingia madarakani na kukuta Jimbo
zima la Kishapu likipata maji kwa chini ya asilimia nne, lakini kwa
sasa vijiji vingi vimeongezeka. Utekelezaji wa ahadi zake juu ya huduma
za maji unaenda awamu kwa awamu hivyo kila kijiji kitapata maji safi na
salama. "Ahadi yangu mimi ni miaka mitano, ilani ya CCM (Chama Cha
Mapinduzi) ni ya miaka mitano, ninaenda kwa awamu yaani vijijini 10 kwa
kila mwaka kwa wilaya," alisema mbunge huyo.
Anasema upo mradi mkubwa wa Ziwa Victoria ambao
bomba lake linatokea Mkoa wa Shinyanga, mradi ambao utavinufaisha
kihuduma za maji vijiji vingine vingi kutoka Jimbo la Kishapu.
Anawashauri wananchi kuwa wavumilivu kwani juhudi zinaendelea kufanywa
kuhakikisha maji yanasambazwa katika vijiji vyote vihitaji.
Akitoa ufafanuzi juu ya zoezi la ufukuaji mabomba
yaliosambazwa kwa baadhi ya vijiji anasema, kwanza mabomba hayo si
salama kutokana na kukaa muda mrefu ardhini bila kutumika. maji
yanayotoka eneo la Kishapu yalifungwa mabomba mapya, mabomba
yanayofukuliwa kwa sasa yamekaa muda mrefu ardhini bila kutumika hivyo
si salama. Anasema utakapofika mradi wa Ziwa Victoria yatafungwa mabomba
mapya na kusambaza maji vijiji husika.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment