Katika mkutano huo na wahariri TGNP imeainisha baadhi ya mafanikio
na changamoto ambazo mtandao huo umezipata, ikiwa mbioni kufanya tamasha
la mwaka huu ambalo litafanyika Septemba 3 hadi 6 2013, Katika viwanja
vya TGNP Mabibo.
TGNP inatarajia kutumia Tamasha la Jinsia kuwapa
wanawake fursa ya kushiriki mijadala ya wazi na kupaaza sauti zao,
tamasha hili litashirikisha wanawake, wanaume, Vijana na watoto zaidi ya
5000 kutoka mikoa yote ya Tanzania na nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya
na Amerika.
TGNP imebainisha kuwa kupitia Tamasha hilo, wanawake
na wanaume wanaoshiriki wanapata fursa ya kujijengea uwezo wa kutumia
mbinu za kiraghibishi katika, uchambuzi wa sera , bajeti ya kijinsia,
kujadili kwa pamoja na watendaji wa serikali kuu na za mitaa walioalikwa
namna bora ya utoaji huduma ambazo zitamfikia kila mwananchi.
Pamoja na mijadala hiyo ya wazi, kutakuwa na
mahakama ya wananchi (Popular tribunal) itakayoendeshwa na Chama cha
Majaji Wanawake (TAWJA), watunga sera, wanasheria, wanaharakati
waliobobea kwenye masuala ya Kisheria na wananchi walioathiriwa na mfumo
kandamizi na kukosa msaada wa kisheria au kuathika na hukumu
zilizotolewa.
Aidha siku inayofuata kutakuwepo na Bunge la wananchi
ambalo litaongozwa na wanazuoni na wataalamu wa sheria na wananchi wote
watapata fursa ya kushiriki kikamilifu.
Mijadala mingine italenga katika masuala ya haki ya
uchumi kwenye upatikanaji wa huduma za msingi za jamii kama maji, afya,
elimu, miundombinu na haki ya jamii katika umiliki wa rasilimali ardhi.
Aidha, suala la Katiba mpya litapewa kipaumbele katika mijadala
itakayofanyika ikiwepo kuendelea kudai ushiriki ulio sawia katika fursa
na michakato iliyosalia kufikia kupata katiba mpya ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment