Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wakifuatilia mada anuai |
Baadhi ya washiriki wa semina hiyo |
Mkurugenzi wa Mashirika yasio ya Kiserikali toka wizara hiyo, Marcel Katemba akisoma hotuba ya Katibu Mkuu |
Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania(TGNP) Kushoto, Mkurugenzi wa mashirika yasiyo ya kiserikali toka wizara hiyo, Marcel Katemba na mgeni wakifuatilia mafunzo |
VIONGOZI wakuu na watendaji wa idara mbalimbali kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto nchini leo wamepewa mafunzo ya namna ya kuandaa bajeti kwa kuzingatia usawa wa kijinsia.
Mafunzo hayo ya siku nne yanayofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yameandaliwa na Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) kupitia taasisi yao ya Chuo cha Jinsia (GTI), ambapo washiriki hao kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto wanawezeshwa kuandaa bajeti kwa mtanzamo wa kijinsia.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP, Usu Mallya alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yanasaidia kujenga stadi na maarifa kwa viongozi na watendaji wakuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto kuzingatia masuala ya jinsia kwenye bajeti ya Wizara hiyo.
Alisema ni mafunzo yanayounganisha utashi wa kisiasa kwa kuzingatia masuala ya jinsia na usawa serikalini, ili kupunguza mapengo yaliyopo inabidi kuwekeza fedha na rasilimali anuai.
alisema nadharia iliyopo kwenye sera inaweza kutekelezeka endapo kutakuwa na uwezeshaji wa rasilimali na fedha ili kuhakikisha huduma za kijamii zinatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya makundi yote yaani wanawake na wanaume.
Aidha aliongeza kuwa mara nyingi mahitaji ya kundi la wanawake yamekuwa yakisahaulika jambo ambalo lina onesha kuna kila sababu ya kuwawezesha watendaji wizara husika kiuchambuizi wa sera na bajeti kwa mlengo wa kijinsia na kuainisha mapungufu kama hayo ili yaweze kufanyiwa kazi.
Alisema kundi la wanawake bado limekuwa na changamoto hasa katika huduma za afya, elimu na yinginezo ambazo zinaongeza mzigo kwa wanawake. Ameitaka Serikali kuongeza uwekezaji katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia, na kuongeza idadi ya wanawake katika vyombo vya uamuzi ili kuleta usawa wa kijinsia.
Alisema Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ndiyo wizara yenye dhamana katika usimamizi wa masuala ya kijinsia nchini Tanzania na usimamizi wa sera ya jinsia na uratibu wa vitengo vyote vya jinsia...hivyo ni muhimu kwa watendaji wake kuwa na uelewa kwa kutosha, uwezo wa kirasilimali na rasilimali watu ili watendaji hao waweza kufanya ufuatiliaji wa kutosha katika utekelezaji wa masuala anuai kwenye bajeti.
Alisema wakati TGNP ikijiandaa kuadhimisha miaka 20 ya utendaji wake licha ya uwepo wa changamoto kadhaa, yapo mafanikio ambayo yanaonekana katika juhudi za mapambano ya harakati za kijinsia kupitia taasisi hiyo.
"Mabadiliko yoyote ya kijamii ni mchakato na miaka 20 ni mingi, tungetarajia tuwe tumepiga hatua kubwa zaidi, lakini kwanza ni vizuri kutambua juhudi zilizofanywa zimeanza kuzaa matunda kwenye maeneo mengi, miaka 20 iliyopita hata dhana ya jinsia haikuwepo kwenye mazungumzo yetu hata dhana ya mfumo dume ilikuwa haipo lakini kwa sasa wanawake na wanaume wanakaa pamoja na kuzungumzia masuala hayo," alisema Bi. Mallya.
Naye Mkurugenzi wa Mashirika yasio ya Kiserikali toka wizara hiyo, Marcel Katemba akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu alisema serikali inajitahidi katika upangaji na utekelezaji wa bajeti maeneo anuai ili kuhakikisha makundi yote yananufaika na rasilimali za taifa.
Akifafanua juu ya kuendelea kwa hali ya unyanyasaji wa kijinsia katika baadhi ya maeneo licha ya juhudi za kupambana na vitendo hivyo alisema serikali inaendelea na utoaji wa elimu ya uelewa juu ya masuala ya haki, kwani jamii ikielewa vitendo kama hivyo vitakoma mara moja.
*Imeandaliwa na www.thehabari.com
No comments:
Post a Comment