TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
Hakuna
biashara ya binadamu katika Tanzania – Rais Kikwete
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa hakuna shughuli za
biashara haramu ya binadamu inayofanywa katika Tanzania bali barabara za
Tanzania na ardhi yake inatumiwa kupitisha biashara hiyo.
Hata hivyo, Rais Kikwete amesema kuwa
Serikali yake itaendelea kushirikiana na nchi jirani kuhusu chimbuko la
biashara hiyo na katika kuchukua hatua za kukomesha vitendo hivyo haramu.
Rais Kikwete ametoa msimamo huo wa
Tanzania leo, Jumatano, Septemba 25, 2013, wakati alipokutana na kufanya
mazungumzo na ujumbe wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC)
ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Bwana Daniel W. Yohannes.
Ujumbe huo ulikutana na Rais Kikwete
katika Hoteli ya JW Marriott, mjini New York, ambako amefikia kwa ziara yake ya
kikazi nchini Marekani na Bwana Yohannes na wenzake walikuwa wanamwelezea Rais
Kikwete maendeleo ya ombi la Tanzania la awamu ya pili ya misaada ya maendeleo
baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza.
Katika mazungumzo hayo, Bwana Yohannes
ametaka kujua hatua ambazo zinachukuliwa na Serikali ya Rais Kikwete
kukabiliana na baadhi ya mambo yanayojitokeza kuwa changamoto katika
utekelezaji wa miradi ya MCC kupitia
Shirika la Tanzania la Millennium
Challenge Account Tanzania – MCA (T).
Baadhi ya changamoto ambazo Bwana
Yohannes amezitaja ni pamoja na nini kinafanyika kuhusu TANESCO, kuhusu juhudi
za kupambana na rushwa na jinsi gani ya kukabiliana na biashara haramu ya
binadamu.
Rais Kikwete ametoa majibu ya
changamoto zote tatu na kumweleza Bwana Yohannes kuwa biashara haramu ya
binadamu haifanyiki wala kuanzia katika Tanzania na kuwa inaanzia Ethiopia,
inapitia Kenya, Tanzania, Malawi na kwenda hadi Afrika Kusini.
“Wanakusanya watu katika Ethiopia
na kuna mtu anapewa fedha na watu hao wanaokusanywa. Wanakuja Kenya na kuna mtu
wa kuwapokea na kuwahudumia, wanakuja Arusha na hatimaye wanaingia Malawi na
Afrika Kusini. Katika Tanzania wanapita tu na kuna wakati tulipata kukamata
Waethiopia kiasi cha 19,000 na tukawarudisha kwao kwa gharama yetu,”
amesema Rais Kikwete na kuongeza:
“Kutoka Ethiopia watu hawa
wamekuwa kama mto usiokauka maji. Hivyo, sisi katika Tanzania tunafanywa kama
njia ya kupitia tu. Ni kweli wako mawakala lakini kwa hakika biashara hii
haifanyiki katika Tanzania. Inafanyika kwingine na nchi yetu inafanywa kama
njia tu. Kuna wakati nilipata kuzungumza na viongozi wa Ethiopia na Kenya
kuhusu suala hilo lakini bado tutaendelea kulifuatilia.”
Imetolewa na:
Kurugenzi ya
Mawasiliano ya Rais,
Ikulu,
DAR ES SALAAM.
25 Septemba, 2013
No comments:
Post a Comment