KLABU
inayoshiriki Ligi ya Daraja la Kwanza ya Lipuli ya Iringa imemshutumu Makamu
Mwenyekiti wa Simba, Joseph Itang’are ‘Mzee Kinesi’ kwa kitendo cha ubadhirifu.
Mwenyekiti
wa Lipuli, Abu Changawa aliwaeleza waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa
ubadhirifu huo umetokana na Kinesi kuuza tiketi 2,000 kienyeji zilizotokana na
vitabu 10 vilivyoongezwa kinyume cha vile vya awali walivyokubaliana kwenye
mechi ya kirafiki waliyocheza mwishoni mwa wiki iliyopita.
Changawa
alisema awali walikubaliana kuuza vitabu 30 ambapo kwa kila kimoja kilikuwa na
tiketi 50 na vyote viliisha dakika 20 za kwanza za mchezo.
Alisema
baada ya viongozi wenzake kufanya uchunguzi walibaini kuwa tiketi zimeisha,
lakini bado kulikuwa na idadi ya watu waliokuwa wakiingia uwanjani ndipo
wakaanza kufanya uchaguzi wanaingiaje wakati tiketi ziliisha.
Katika
uchunguzi wao, alidai walibaini kuna vitabu vitano viliongezwa tofauti na vile
vya mwanzo bila kushirikishana ambavyo viliuzwa kiholela. Baada ya kufuatilia,
alisema akaelezwa kuwa tiketi hazijaisha isipokuwa kuna kitabu kimoja kilikuwa
kimebaki.
“Haiwezekani
mechi moja vikauzwa vitabu vya aina mbili tofauti hilo ni jambo
linalonisikitisha, kuona kiongozi mkubwa kama Makamu Mwenyekiti wa Simba,
anafanya ubadhirifu, tutajifunza nini kwao sisi kama timu ndogo?” Alihoji
Changawa.
Alisema
kitendo hicho anakifananisha na ujambazi na wao hawako tayari kuona kinaendelea
kwa viongozi wa klabu kubwa kwa sababu ni fedheha.
Alisema
pia walikubaliana kuwa mapato yatakayopatikana kutokana na mechi hiyo baada ya
kukatwa gharama mbalimbali, kile kinachobaki wagawane asilimia 50 kwa 50.
Kwa
mujibu wa Changawa, mapato yaliyopatikana ni Sh milioni 3.1, na hivyo baada ya
makato mengine, waliondoka na Sh 700,000.
Alisema
kutokana na ubadhirifu, tiketi zenye thamani ya Sh milioni nne zimepotea na
kudai kuwa walifikiri wangepata fedha nyingi ili kuwapa wachezaji posho,
ilishindikana kutokana na kupata kiasi kidogo.
“Tumebaki
na lawama ndani ya klabu yetu wakifikiri kuwa tulipata fedha nyingi na
tumekula, lakini ukweli ni kwamba tulifanyiwa ubadhirifu, ndio maana
tumeshindwa kuwalipa wachezaji wetu posho,” alidai.
Changawa
aliongeza kuwa waliomba kucheza na Simba kwa sababu walikuwa wakihitaji msaada,
lakini kutokana na kitendo hicho hawataki tena kucheza mechi ya kirafiki na
klabu hiyo.
Kwa
upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Simba, Mzee Kinesi alidai kuwa yeye
hakuhusika na tiketi isipokuwa Mhasibu wa Simba na yule wa Lipuli ndio walikuwa
wanasimamia.
Alisema
shida iliyokuwepo kwa klabu hiyo yaani Lipuli toka awali walifikiri kuingiza
kiasi cha Sh milioni nne, lakini haikuwezekana kwa vile kiwango walichokuwa
wakitoza kilikuwa Sh 2,000, na kudai kuwa kama wangetaka hivyo wangetoza
kiingilio Sh 3,000 au 4,000.
Aliongeza
kuwa hakuna maandishi waliyowekeana kuwa ziuzwe tiketi kadhaa, kwa vile vitabu
walivyokubaliana ndivyo ambavyo vilikuwa uwanjani na si vinginevyo.
Tayari
Lipuli imepeleka malalamiko yao kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba,
Zakaria Hans Pope na Mwenyekiti Ismail Aden Rage. Kwa mujibu wa Changawa, timu
hiyo itaondoka leo kwenda Morogoro kwa ajili ya kushiriki kwenye mashindano ya
Ligi ya Daraja la Kwanza yatakayoanza Septemba 14.
No comments:
Post a Comment