Na Gazeti la Tanzania Daima
RAIS Jakaya Kikwete, Rais wa Awamu ya Pili Alhaji Ally Hassan Mwinyi,
Rais Awamu ya Tatu Benjamin Mkapa na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni
ya IPP, Dk. Reginald Mengi wametunukiwa nishani kwa kutambua mchango wao
katika kuboresha afya ya mama na mtoto nchini.
Nishani hizo zilizokabidhiwa jana na Makamu wa Rais, Dk. Gharib
Bilali, zimeandaliwa na Taasisi ya Madaktari Waliosoma Vyuo Vikuu nchini
(THPI).
Wengine waliokabidhiwa nishani hiyo ni pamoja na mke wa rais, Mama
Salma Kikwete kupitia Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA), madaktari
na wauguzi waliofanya vizuri katika hospitali zao wanazozihudumia.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri wa Uwekezaji na Uwezeshaji, Dk.
Mery Nagu, alisema kama mama hatakuwa na afya yenye usalama, taifa nalo
halitakuwa salama kwa kuwa taifa lenye afya linatokana na mama mwenye
afya.
Kwa upande wake, Dk. Mengi alisema Watanzania wana uwezo mkubwa wa
kutatua matatizo ya wenzao, hivyo ni vyema kila mwenye uwezo kuelekeza
nguvu zake kuwasaidia wasio na uwezo hasa wa kupata matibabu.
“Tuna uwezo mkubwa sana wa kusaidiana, na kama kuna baraka ulizopata
wewe unatakiwa uwapelekee na wenzako, na Mtanzania si mnyonge na akiwa
mnyonge atakuwa amejitakia, hivyo tunastahili maendeleo na kusaidiana,”
alisema Mengi.
Pia aliahidi kusaidia ujenzi wa wodi ya akina mama pindi taasisi ya THPI itakapoanza kujenga.
Naye Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Telesphory Kyaruzi, alisema kuwa
taarifa ya jarida la Umoja wa Mataifa, Global Health and Deplomacy
inaonyesha kuwa kina mama wajawazito 368,000, hufariki dunia kutokana na
matatizo ya ujauzito duniani.
“Vifo vya mama wajawazito nchini kwa mwaka 2005 vilikuwa 578, kwa
vizazi hai 100,000, na kufikia 454 kwa vizazi hai 100,000. Kwa mwaka
2012 vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano vilikuwa 122 kwa
watoto hai 1,000, mwaka 2004 mpaka 81 kwa watoto hai 1,000 mwaka 2012,”
alisema Dk. Kyaruzi.
Aliongeza kuwa vifo vya watoto chini ya mwaka mmoja vilikuwa 68 kwa
watoto hai 1,000 kwa mwaka 2004 hadi 51 kwa watoto hai 1,000 kwa mwaka
2012.
No comments:
Post a Comment