Katibu Mkuu wa BASATA Geofrey Mwingereza |
Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa
kushirikiana na Kampuni ya Reggae Production House iliyo chini ya Msanii
Mkongwe wa reggae Innocent Nganyagwa limeandaa programu maalum kwa ajili ya kurudisha
hadhi ya muziki wa reggae nchini.
Programu hiyo ambayo itafanyika makao
makuu ya BASATA yaliyoko Ilala Sharif Shamba jijini Dar es Salaam Jumatatu ya
Tarehe 28/09/2015 kuanzia saa 4:00 hadi saa 6:30
Mchana kupitia Programu ya
Jukwaa la Sanaa, itakuwa mahsusi kwa ajili ya kuurudisha muziki wa reggae
jukwaani, kujadili mwelekeo wa muziki huu na kuja na mikakati bora ya
kuurudishia hadhi yake.
Ieleweke kwamba katika siku za karibuni
muziki huu wa reggae umekuwa umeganda na kutokupiga hatua kubwa hali ambayo
imewafanya wadau wa muziki kukosa burudani ambayo wamekuwa wakiipata huko nyuma
kupitia kwa wasanii wakongwe kama Innocent Nganyagwa, Innocent Garinoma,
Justine Kalikawe na wengineo.
Changamoto kubwa si tu ni muziki huu
kutochezwa kwenye vyombo vya habari bali pia kuna changamoto ya wasanii wenyewe
kutokubadilika na kutengeneza muziki unaokwenda sambamba na soko pia hitaji la
mashabiki.
Ni nia ya BASATA kuona wasanii na wadau
wote wa muziki nchini wanahudhuria programu hii mahsusi kwa lengo la kujadiliana
kwa pamoja hatma ya muziki wa reggae, kupata historia ya jinsi ulivyokuwa huko
nyuma, kutazama na kuburudika Jukwaani na muziki wa mmoja wa wasanii wakongwe
wa muziki huu.
BASATA linaamini kwamba baada ya
programu hii wasanii wa reggae na wadau kwa ujumla watakuwa na mwanzo mpya
katika kurudisha hadhi ya muziki wa reggae nchini na kuhakikisha unaendelea
kudumu.
Sanaa ni Kazi, tuikuze, tuitunze na
kuithamini
IMETOLEWA NA KITENGO CHA HABARI BASATA
No comments:
Post a Comment